EXCLUSIVE: Kahata ameondoka na alama zake Simba, Aziita Yanga, Azam

Wednesday June 09 2021
kahata 1
By Waandishi Wetu

FRANCIS Kahata kiungo amekuwa wa kwanza kuaga ndani ya Simba na sasa anazungumzia kwao Kenya, kwani tayari ameondoka baada ya kumalizana na mabosi wake.

Julai 2019, Simba ilimsajili Kahata akitokea Gor Mahia inayoshiriki Ligi Kuu Kenya (KPL) kwa mkataba wa miaka miwili ambao ulipaswa kumalizika mwezi ujao.

Kahata si mchezaji mbaya, lakini ushindani wa namba alioupata kutoka kwa kina Luis Miquissone, Rally Bwalya, Bernard Morrison, Clatous Chama na Hassan Dilunga, ulimweka katika wakati mgumu kikosini Simba.

kahata 4

Baadaye uongozi wa Simba uliamua kumuweka kando kwa kumuondoa kwenye kikosi cha kucheza mechi za Ligi Kuu Bara msimu huu na kumbakiza katika mashindano ya kimataifa, Ligi ya Mabingwa Afrika tu, ambako timu hiyo iliishia hatua ya robo fainali.

Nafasi yake kwenye mechi za ndani ilichukuliwa na Perfect Chikwende, raia wa Zimbabwe ambaye pia tangu afike ameshindwa kuonyesha kiwango chake kili-chotarajiwa.Mwanaspoti lilifanya mahojiano maalumu na mchezaji huyo baada ya kumalizana na Simba ikiwa ni siku chache kabla ya kurudi kwao ambapo alielezea mambo mbalimbali tangu ajiunge na Wekundu hao wa Msimbazi.

Advertisement


 MAFANIKIO NA CHANGAMOTO

Akiwa na timu hiyo, amekuwa miongoni mwa wachezaji waliopata mafanikio makubwa baada ya kushinda mataji kama Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

KAHATA PIC

Anasema kama mchezaji licha ya kuchukua mataji hayo pia amekutana na changamoto nyingi ikiwamo kuumia na kumfanya akae nje ya uwanja kwa muda mrefu.

“Kama mchezaji utakutana na changamoto nyingi ikiwamo kuumia wakati ligi inaelekea ukingoni kwa msimu wa 2019/20 ambapo mpaka msimu mpya unaanza sikuwa nimepona vizuri na nilipopona nilianza vizuri ingawa mabadiliko yaliyofanyika miezi sita iliyopita yalichangia kutokuwa na msimu mzuri kwa mwaka wangu wa pili licha ya kupata tuzo ya mchezaji bora wa mwezi,” anasema Kahata.


MABADILIKO YA LESENI

Akiwa ametoka kwenye majeraha na kuanza kurejea kwenye ubora wake, ndipo mabadiliko ya leseni yalifanyika upande wake kwa kumtoa ligi ya ndani na kumuacha michuano ya kimataifa pekee.Anasema kitendo hicho kilifan-yika pasipo kushirikishwa lolote jambo ambalo lilimvuruga kisaikolojia.

kahata2

 “Mabadiliko yaliyofanyika ni kuhusu leseni yangu, mabadiliko hayo niliyasikia mitandaoni miezi sita iliyopita nikiwa nyumbani (Kenya) ya kuwa nafaa kucheza Ligi ya Mabingwa tu kwa sababu namba ya wache-zaji wa kigeni ilizidi na niliporudi Tanzania nilimpigia simu wakala wangu kujua nini kinaendelea, baadaye alizungumza na viongozi halafu akaja kwangu kunipa sababu hiyo ya uwepo wa idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni.”Anasema mabadiliko hayo akiwa kama mchezaji yalimkosesha nafasi ya kucheza huku wenzake wakiwa wanacheza mechi nyingi zilizowasaidia kuwa fiti.


 KUPOTEZA NAMBA HARAMBEE STARS

Kiungo huyu mara kadhaa amekuwa akiitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa Kenya ‘Harambee Stars’, lakini kutokana na kutopata nafasi ya kucheza ndani ya Simba kumemfanya aondolewe kwenye kikosi hicho pia.

Kahata alikuwa kwenye kikosi cha Harambee Stars kilichocheza Fainali za Mataifa Afrika (AFCON) 2019 baada ya hapo akasajiliwa Simba.

Anasema kuwa kutopewa nafasi ya kucheza ndio sababu kubwa ya kutoitwa kwenye kikosi hicho kwani makocha wanaita wachezaji wanaocheza. “Mechi za Ligi ya Mabingwa kwa mwezi zilikuwa zinachezwa mbili tu na ikumbukwe kuwa kocha nae huwa na machaguo yake sio kila mechi utapangiwa, wenzangu walikuwa wanacheza mechi nyingine za ligi ya ndani na kuwafanya wawe fiti na waitwe timu za taifa.

“Makocha huangalia viwango vya wachezaji wanapocheza michuano mbalimbali ya timu zao, kwangu imekuwa vigumu kuitwa,” anasema na kuongeza kuwa; “Hata Kocha Gomes (Didier) alipoingia na kuanza kufundisha alishangaa sana alipokuta leseni yangu imebadilishwa, ananifahamu tangu nikiwa Gór Mahia na alinishauri nisivunjike moyo kwani anafahamu uwezo wangu na nilikuwa nafanya mazoezi ili nisimuangushe.”


 HATAMSAHAU MO DEWJI

Anasema licha ya kundoka Simba hatamsahau Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohamed ‘Mo’ Dewji katika misimu yake miwili aliyokuwa na timu hiyo. Anasema hatawasahau pia mashabiki wa soka wa Simba kwa mapenzi yao na kuwapa sapoti muda wote na popote wanapokwenda kucheza.

“Nawashukuru viongozi wa Simba chini ya Mo Dewji kwa kuniamini na kunipatia mkataba wa miaka miwili kamwe sitawasahau na mashabiki waliokuwa wanaacha kazi zao kuja kushangilia timu inapocheza jambo lililotupa hamasa ya kujituma ili kushinda mechi, wanafanya kazi kubwa sana sijawahi kuona sapoti kama hiyo labda zamani kwa mashabiki wa Gor Mahia.

Mashabiki wa ligi ya Kenya zamani walikuwa wanashangilia timu zao hususani wa Gor Mahia, kwa sasa Corona imerud-isha nyuma mpira kwa kiasi kikubwa, nitawakumbuka sana mashabiki.”


 MKATABA UMEISHA HIVI

Mkataba wake ulikuwa umalizike Julai 4, 2021 lakini baada ya kuambiwa hatakuwa sehemu ya kikosi msimu ujao aliona ni vyema aondoke tu. “Hakukuwa na mazungumzo ya kuongeza mkataba kwani Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alinipigia simu na kuniambia hawataweza kuendelea kuwa na mkataba kati yangu na wao.

“Simba ni timu ambayo wameni-patia upana mzuri kwani kwa sasa ni moja ya timu kubwa barani Afrika wamefika hatua ya robo fainali pia wamefanikiwa kuifunga timu kama Al Ahly inayoogopwa kutokana na kutwaa ubingwa wa michuano hiyo mara nyingi, kiufupi nina furaha kuwa sehemu ya timu kubwa barani Afrika licha ya kuondoka.”


 YANGA, AZAM RUKSA SASA

Kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kumalizana na Simba, hivyo ana uwezo wa kucheza timu yoyote Tanzania ama nje ya hapa, kwani hivi sasa Tanzania ni kama nyumbani hivyo anaweza kurudi kuendelea na kazi yake.

“Timu yoyote ikinitaka hata kama ni Yanga ama Azam tukifikia makubaliano niko tayari kuitumikia kwani mpira ndio maisha yangu kwa asilimia kubwa na umenifanya nibadili maisha yangu, siangalii kiasi nitakachopata bali nikiridhika ama wakala wangu akiona inafaa.

“Huwa ananishauri na pia ili niweze kurudisha kidogo ninachopata kwa jamii yangu kama vile kuwapelekea vitakasa mikono na maji kwa wakazi wa Mathare, Nairobi na pia hupeleka mipira katika timu mbalimbali za vijana ili waweze kutimiza ndoto zao,” anasema na kuongeza; “Kazi ya wachezaji ni kucheza na kufanya mazoezi nimekuwa na uhusiano mzuri na makocha wote watatu kuanzia Patrick Aussems, Sven (Vandenbroeck) na hata Gomez, wao kazi yao ni kufundisha tangu nimetoka Afrika Kusini sijafanikiwa kuzungumza na kocha kuhusu ishu ya mkataba, naondoka nikiwa vizuri na uongozi kwani huwezi kujua mbele itakuwaje.”

Akizungumzia upande wa timu za Kenya, Kahata anasema timu nyingi za huko ziliathiriwa na corona upande wa uchumi haziko vizuri na ikumbukwe kuwa mwanangu Winslet Kahata naye yupo kwenye moja ya akademi hivyo natamani azifikie ndoto zake. “Nataka mwanagu awe kama mimi au mama yake kwani naye alikuwa mchezaji timu ya Mathare na nilikutana naye nchini Norway na tulianzia uhusiano wetu naji-tahidi kuzisaidia akademi ili watoto na vijana wengi wafike wanapopataka kwani wanapitia changamoto mbalimbali,” anasema Kahata.

Imeandikwa na Loveness Bernard na Thobias Sebastian

Advertisement