EDGER buku nusura limtoe roho

Muktasari:

HAIKUWA safari rahisi kwa straika wa Mbeya City, William Edgar ‘Duma’ (20), kuishi ndoto ya kucheza Ligi Kuu Bara, baada ya timu hiyo kupanda msimu huu. Katika mahojiano yake na Mwanaspoti, Edgar anafunguka mengi, ikiwemo kwa nini alitoa chozi baada ya kuifunga Mtibwa Sugar bao lake la kwanza, mechi yake ya kwanza kwenye Ligi Kuu.

HAIKUWA safari rahisi kwa straika wa Mbeya City, William Edgar ‘Duma’ (20), kuishi ndoto ya kucheza Ligi Kuu Bara, baada ya timu hiyo kupanda msimu huu. Katika mahojiano yake na Mwanaspoti, Edgar anafunguka mengi, ikiwemo kwa nini alitoa chozi baada ya kuifunga Mtibwa Sugar bao lake la kwanza, mechi yake ya kwanza kwenye Ligi Kuu.

“Nina mengi nimepitia hadi kuishi ndoto yangu, nimejifunza kutokukatishwa tamaa na yeyote kupigania ninachokiamini ili mradi nipo hai,” anasema.


SAFARI YAKE

Edgar, aliyekuwa mchezaji wa kwanza msimu huu kufunga bao katika Ligi Kuu Bara wakati akiizamisha Mtibwa kwenye mechi iliyopigwa Uwanja wa Mabatini, Mlandizi Pwani anasema alikulia kwenye kituo cha soka, kilichokuwa kinajulikana kwa jina la Ferari kilikuwa Mbeya na sasa hakipo, baada ya hapo mwaka 2019 alijiunga na Tukuyu Stars ikiwa Daraja la Pili. “Nimelelewa katika kituo cha soka, ndio maana sikuwahi kuwa na ndoto nyingine zaidi ya kuwaza kuwa mwanasoka mkubwa ndani na nje,” anasema.


ALIPWA BUKU, AKABWA KODI

Baada ya kujiunga na Tukuyu Stars anasimulia mikasa aliyopitia, iliyomfanya acheze mechi mbili kisha akaachana nao.

“Tulikaa kambini kwa muda mrefu, baada ya kucheza mechi na RC ya Dodoma tukatoka sare ya mabao 2-2, yote nilifunga mwenyewe, viongozi wakatupa mapumziko,” anasema Edgar na akaongeza;

“Wachezaji wengi tulikuwa tunaishi Mbeya Mjini, tukaongozana na kiongozi hadi Uyole, baada ya kushuka akatugawia Sh1,000 kila mmoja, nikauliza kiongozi hii ya nini akasema hana pesa tupokee tu, hapo nilipopanga kodi ilikuwa imeisha, nilikuwa nadaiwa Sh75,000,” anasema.

Anasema aliichukua Sh1000 akarejea kwenye chumba chake, alijifungia na kuanza kulia kwa uchungu, asijue anamlipa nini mwenye nyumba.

“Mungu hamuachi mtu, nikapokea ofa ya kwenda kucheza Ndondo wilayani Chunya, nikaisaidia timu kuifungia mabao matatu, ambapo wakanilipa Sh.70,000 na kwa sababu niliwafurahisha mashabiki nikajikuta narejea nyumbani na laki na kitu hivi,” anasema.

Anasema baada ya kulipa kodi akarejea tena katika kambi ya Tukuyu Stars, ambapo alicheza dhidi ya Fountain Gate waliotoka nao suluhu.

“Tukarejea na kiongozi huyo hadi Uyole, akatugawia tena Sh1,000, nilichukia kucheza soka na sikurudi tena kambini, baada ya kumaliza mkataba nao ndipo nikajiunga na Mbeya Kwanza 2020 hadi tunapanda kuja Ligi Kuu Bara msimu huu,” anasema.


KINARA WA MABAO

Anasema aliibuka Mfungaji Bora kwa mabao 13 Ligi Daraja la Kwanza msimu uliopita (sasa Championship) kwa sasa na kitu alichokuwa anakitamani ni kucheza ligi kuu, tayari anaishi ndoto zake.

“Nilitamani siku moja nicheze ligi kuu, moyo wangu umejaa furaha ya ajabu baada ya jambo hilo kuliishi kwa uhalisia,” anasema.


SABABU YA KILIO

Anasema dakika 45 za kipindi cha kwanza, timu yake ilipocheza na Mtibwa Uwanja wa Mabatini alikuwa kama bado yupo usingizini, baada ya kufunga akagundua ndoto yake ya kucheza Ligi Kuu imetimia.

“Wakati naanza kucheza dakika za mwanzo nilikuwa na mawenge ya kutoamini kwamba ndoto zangu zimetimia, baada ya kufunga bao, akili ikafunguka na kuelewa naishi ndoto zangu,” anasema Edgar na anaongeza;

“Nilijikuta nalia kwa furaha, namshangaa Mungu kuniwezesha kutimiza ndoto yangu kwa kishindo, haikuwa rahisi, kwani nimepitia changamoto nyingi sana,” anasema.


ANAPENDA USHINDANI

Anasema alikuwa anawasikia washambuliaji kama Meddie Kagere, John Bocco na Prince Dube walivyokuwa wanashindana kuzifumania nyavu, alitamani siku moja aonje ushindani huo, tayari ameingia kwenye ulingo huo.

“Natamani nianze na mabao 10 kwa msimu huu, kwasababu napenda sana kucheza na nyavu, naamini nitapambana kulifanikisha hilo,”anasema. Ukiachana na hilo, anawataja wachezaji ambao anaangalia zaidi kazi zao na kujifunza kitu kuwa ni mshambuliji wa zamani wa Manchester United Carlos Tevez na straika wa Atletico Madrid Luis Suarez.


WASIKIE WADAU

Meneja wa timu hiyo, Ulimboka Mwakingwe ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba, anasema Edgar akijituma ni tishio jipya la kutikisa nyavu ligi kuu. “Nimemshuhudia tangu akiwa Ligi Daraja la Kwanza (Championship) ndiye aliyekuwa mfungaji bora, anajua kutumia nafasi, kutafuta mipira kuanzia katikati na pia anapenda mazoezi,” anasema.

Kwa upande wa beki wa Tiger, Zuwena Aziz anasema Egdar ana mwanzo mzuri anapaswa kulinda kiwango alichoanza nacho.