BOLI HALIMO: Makocha wa soka ambao hawakutisha kabisa walipokuwa wachezaji

Muktasari:
- Hawa hapa makocha ambao wamelishika soka la dunia na kuweka majina yao kwenye anga za juu kabisa kama moja ya makocha mahiri kabisa kuwahi kutokea kwenye mchezo huo, ambao hawakuwa tishio kabisa wakati wanacheza soka, wengi wao wakiishia kwenye timu za madaraja ya chini kabisa.
LONDON, ENGLAND: MAISHA yana siri kubwa sana. Wakati ukimtarajia mchezaji aliyekuwa na kiwango bora kabisa uwanjani kama Ricardo Kaka, Ronaldinho, Ronaldo de Lima, David Beckham, Thierry Henry kwenda kuwa makocha mahiri kabisa, mambo yamekuwa tofauti kabisa, wanaotamba kwenye tasnia hiyo ni wale wachezaji ambao hawakuwa tishio kabisa wakati wanacheza.
Hawa hapa makocha ambao wamelishika soka la dunia na kuweka majina yao kwenye anga za juu kabisa kama moja ya makocha mahiri kabisa kuwahi kutokea kwenye mchezo huo, ambao hawakuwa tishio kabisa wakati wanacheza soka, wengi wao wakiishia kwenye timu za madaraja ya chini kabisa.

12. Avram Grant
Avram Grant alianza ukocha akiwa na umri wa miaka 18 tu kwenye klabu ya huko nyumbani kwao ya Hapoel Petah Tikva. Alikuwa kwenye majukumu ya timu ya vijana kwa miaka 14 kabla ya kuchukua timu ya wakubwa na kunyakua mataji mawili ya Toto Cup. Baada ya kuzinoa Maccabi Tel Aviv, Maccabi Haifa na timu ya taifa ya Israel, Grant alikwenda Portsmouth kuwa mkurugenzi wa ufundi na kisha akachaguliwa kuwa kocha wa Chelsea na rafiki yake Roman Abramovich baada ya Jose Mourinho kufutwa kazi 2007. Alimaliza nafasi ya pili kwenye Ligi, huku Chelsea ilifungwa pia mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Baadaye alienda Portsmouth, West Ham, Ghana na Zambia aliko sasa.

11. Brendan Rodgers
Brendan Rodgers alionyesha dalili kwamba angekuja kuwa mchezaji mzuri kwenye nafasi ya beki kabla ya kustaafu akiwa na umri wa miaka 20 kufuatia kuumia goti, kipindi hicho alipohama kutoka Ballymena kwenda Reading akiwa na miaka 18 tu. Rodgers aliendelea kucheza soka la mchangani kabla ya kwenda Hispania kujifundisha ukocha. Baadaye, alitumia muda wake wa kujifunza njia za ukocha huko Hispania kabla ya kupata kazi ya kuinoa timu ya vijana ya Chelsea wakati huo wa kocha Jose Mourinho. Baadaye alikwenda Swansea, Liverpool, Celtic na Leicester City, ambako kocha alifanya vizuri na kumfanya ahusishwe na klabu kubwa kama ya Man United.

10. Leonardo Jardim
Baada ya kuzaliwa Venezuela kwa wazazi wa Kireno, Leonardo Jardim alikulia kwenye visiwa vya Madeira na kuanza kazi yake ya ukocha kama msaidizi kwenye klabu ya mtaani kwao ya Camacha wakati akiwa na umri wa miaka 27. Baada ya muda wake huo huko Camacha, alienda Chaves, timu ya daraja la tatu ya Ureno. Jardim aling’ara Beira-Mar kwenye ligi kubwa ya Ureno na kutamba pia akiwa na Braga. Baadaye aliiongoza Olympiacos kushinda Greek Super League na alikwenda kumaliza katika nafasi ya pili akiwa na Sporting CP huko Ureno na kushinda Ligue 1 akiwa na kikosi cha Monaco alichoinoa kwa miaka minne. Aliwahi kuhusishwa na Man United.

9. Jorge Sampaoli
Mzaliwa wa Argentina, Jorge Sampaoli aliiongoza Chile kushinda taji la Copa America – taji la kwanza kubwa kabisa la soka kwenye historia ya taifa hilo, alipofanya hivyo 2015. Sampaoli baadaye alikwenda kuinoa Argentina, sambamba na klabu kadhaa kubwa kabisa ikiwamo Sevilla (mara mbili), Marseille, Santos na Flamengo. Mchezaji huyo wa Newell’s Old Boys alipokuwa mtoto, Sampaoli alishindwa kabisa kuonyesha kiwango bora kwenye soka na hivyo alistaafu akiwa na umri wa miaka 19 tu kabla ya kujiendeleza kwenye ukocha na kuwa mmoja wa makocha mahiri kabisa kwenye mchezo huo wa soka.

8. Maurizio Sarri
Maurizio Sarri alitumia maisha yake yote ya uchezaji kama beki wa kati kwenye klabu ya ridhaa ya Figline na alifeli kwenye majaribio katika klabu za Torino na Fiorentina. Kazi yake ya ukocha aliianza mwaka 1990, na taratibu kocha huyo Mtaliano, anayependa kuvuta sigara, alipanda madaraja na kuwa bora kabisa. Baada ya kuipandisha Empoli kucheza Serie A, alipata kibarua cha kwenda kuinoa Napoli kabla ya kupewa kazi Chelsea, ambako alishinda taji la Europa League mwaka 2019. Alikwenda kuongeza taji la Serie huko Juventus mwaka 2020 na mwaka uliofuata alitua Lazio.

7. Gerard Houllier
Mzaliwa wa Paris, Gerard Houllier alikuwa akicheza nafasi ya kiungo ya Le Touquet na alianza kazi ya ukocha kwenye soka la ridhaa mwaka 1973. Houllier baadaye alikwenda kuzinoa Lens na Paris Saint-Germain, akishinda ubingwa wa Ufaransa msimu wa 1985/86, na aliinoa pia timu ya taifa ya Ufaransa, Les Bleus. Lakini, nyakati zake bora zaidi zinakumbukwa alipokuwa Liverpool, alikoshinda mataji mawili ya Kombe la Ligi, Kombe la FA na UEFA Cup. Aliongoza pia Lyon kubeba mataji mawili ya Ligue na kwa muda mfupi aliinoa Aston Villa.

6. Andre Villas Boas
Andre Villas-Boas aliishi kwenye jengo alilokuwa akiishi Bobby Robson alipopewa kazi ya kutunza vifaa vya klabu ya FC Porto kipindi hicho akiwa na umri wa miaka 16 tu. Baadaye Villas-Boas alifanya kazi ya kuwa kocha msaidizi wa Jose Mourinho kwenye klabu ya Porto, Chelsea na Inter. Baada ya kuinoa Academica, alikwenda kuiongoza Porto kushinda Primeira Liga na Europa League. Mafanikio hayo yakaonekana na Chelsea na kumpa kazi kabla ya kuinoa pia Tottenham, kisha kwenda kunyakua ubingwa wa Russia akiwa na Zenit Saint-Petersburg katika msimu wa 2014/15. Alichaguliwa kuwa rais wa Porto mwaka huu.

5. Julian Nagelsmann
Julian Nagelsmann alionyesha angekuwa mchezaji hatari sana utotoni, lakini beki huyo wa kati alilazimika kustaafu soka akiwa na umri wa miaka 20 tu na kushindwa kupata nafasi ya kuchezea kikosi cha wakubwa cha 1860 Munich au FC Augsburg kutokana na kuwa majeruhi. Alihamishia nguvu kwenye ukocha na kwamba alianza kumsaidia Thomas Tuchel kwenye kufanya skauti huko Augsburg. Alisomea uongozi wa biashara na sayansi ya michezo. Baada ya kutamba na timu ya vijana ya Hoffenheim, alikopachikwa jina la Mourinho mtoto, alitisha zaidi na timu za RB Leipzig, Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani.

4. Rafa Benitez
Wakati anakua, Benitez alikuwa beki matata huko Real Madrid, lakini alipata majeraha wakati anachezea Spanish University XI huko Mexico na kushindwa kuichezea timu ya vijana ya Los Blancos, Castilla kwenye ligi ya Segunda. Baadaye Benitez alikwenda kuzichezea Parla na Linares kwenye Ligi Daraja la Tatu na Nne huko Hispania, lakini alistaafu 1986 baada ya kuumia. Kazi yake ya ukocha alianza kwenye timu ya watoto ya Real Madrid, kabla ya kuzinoa Valladolid, Osasuna, Extremadura na Tenerife. Alitisha zaidi Valencia, alikobeba La Liga mara mbili na Kombe la UEFA kabla ya kuipa Liverpool taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, alizonoa pia Inter, Chelsea, Napoli, Newcastle, Everton na Celta Vigo.

3. Carlos Alberto Parreira
Carlos Alberto Parreira alikuwa kocha wa timu ya taifa ya Brazil wakati inanyakua Kombe la Dunia la nne mwaka 1994, na amekuwa kwenye kibarua cha kuinoa timu hiyo ya Amerika Kusini mara tatu tofauti. Parreira aliwahi pia kuzinoa timu za mataifa mengine kama – Kuwait, United Arab Emirates, Saudi Arabia na Afrika Kusini kwenye fainali za Kombe la Dunia. Hajawahi kucheza soka la kulipwa na badala yake alijiingiza zaidi kwenye ukocha, ambapo kazi yake ya kwanza ilikuwa kuinoa timu ya taifa ya Ghana wakati ana umri wa miaka 23. Ndiye, shujaa wake kocha wa Tanzania, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.

2. Arrigo Sacchi
Hakuwa na kiwango kizuri kuichezea klabu ya mtaani kwao, Baracca Lugo, Arrigo Sacchi akaamua kugeukia kwenye ukocha wa kuinoa timu hiyo akiwa na umri wa miaka 26. Kwanza Sacchi alianza kama muuza viatu kwa miaka kibao wakati alikuwa akizonoa Bellaria, Cesena na Rimini za ligi za chini. Alikwenda kuvutia Parma na hapo akapata dili la kutua AC Milan mwaka 1987. Aliongoza Rossoneri kushinda Serie A mfululizo na Kombe la Ulaya mwaka 1989 na 1990. Baadaye alikwenda kuinoa Italia kwenye Kombe la Dunia 1994 na kuifikisha fainali, ikipoteza kwa mikwaju ya penalti mbele ya Brazil. Anatajwa kama mmoja wa makocha wabunifu kwenye soka.

1. Jose Mourinho
Kipa mtoto wa zamani, Jose Mourinho alicheza soka kidogo sana chini ya baba yake huko Rio Ave na Belenenses, kabla ya kwenda kucheza kwa muda mfupi Sesimbra na Comercio e Industria, timu za ligi ya chini Ureno. Alistaafu soka akiwa na umri wa miaka 23 na kuingia kwenye ukocha. Alisomea sayansi ya michezo na ukocha. Kwanza alifanya kazi kama mkalimani aliyekuwa akimsaidia kocha Bobby Robson huko Sporting CP, Porto na Barcelona kabla ya kuingia kwenye ukocha na kupata mafanikio makubwa akizinoa klabu za Porto, Chelsea, Inter, Real Madrid, Manchester United, Tottenham, AS Roma na sasa Fenerbahce.