Balaa! Mabeki moto waliotupia Ligi Kuu

MABAO 19 yamefungwa na mabeki mpaka sasa katika michezo ya Ligi Kuu Bara ambapo timu zilizopo mkiani zinahaha kujinasua mkiani na nyingine zikikomaa kusalia katika nafasi za juu.

Ligi Kuu msimu huu inayoshirikisha timu 16 imekuwa ngumu na yenye ushindani mkubwa, huku Yanga ikiendeleza ubabe wa kutofungwa mechi 48 za ligi mfululizo toka mwaka jana.

Vita ya ufungaji wa mabao imekuwa kubwa kwa safu ya ushambuliaji, huku mabeki wakifunga licha ya kuwa na majukumu ya kuzuia. Mwanaspoti linakuletea mabeki waliofunga katika michezo ambayo timu zao zimecheza.


Nickson Kibababe - Mtibwa Sugar (mabao 3)

Alifunga katika mchezo dhidi ya Namungo uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2, kisha akatupia tena dhidi ya Ihefu ambao walishinda mabao 3-1, huku dhidi ya Mbeya City wakitoka sare ya mabao 2-2.


Bakari Mwamnyeto - Yanga (mabao 2)

Beki huyu amefunga dhidi ya Polisi Tanzania ambapo Yanga ilishinda mabao 2-1 na akifunga tena dhidi ya Ruvu Shooting na Yanga ilishinda mabao 2-1.


Daniel Amouh - Azam FC (mabao 2)

Amouh alifunga katika mchezo dhidi ya Yanga ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2, akafanya hivyo tena katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar ambao walishinda mabao 4-3.


Hassan Mahamud - Mbeya City (mabao 2)

Katika mchezo dhidi ya Namungo ambao walishinda mabao 2-1 na mchezo wao na Kagera Sugar uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 alifunga bao moja kila mechi.


Vedastus Mwihambi - Mtibwa Sugar ( bao 1)

Katika mchezo dhidi ya Namungo ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2 washambuliaji walisaidiwa na beki huyu kufanya jukumu la kufunga na Mtibwa kupata pointi moja.


Ibrahim Ame - KMC (bao 1)

Katika mchezo wao dhidi ya Mtibwa Sugar ambao walishinda mabao 2-1 Ame alifunga bao moja.


Abdallah Kheri - Azam FC (bao1)

Beki huyu wa wanalambalamba alifunga bao katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar na kuiongoza timu yake kupata ushindi wa mabao 4-3

Kibwana Shomari - Yanga (bao 1)

Ni miongoni mwa mabeki ambao hawakupewa nafasi wakati wa usajili ndani ya kikosi hicho cha Jangwani, lakini amekuwa na mchango mkubwa na mchezo dhidi ya Singida Big Stars akifunga bao moja kati ya mabao 4-1 ambayo timu yake ilivuna kwa walima alizeti hao.


Shomari Kapombe - Simba (bao 1)

Ni beki wa kutumainiwa muda wote ndani ya kikosi cha Simba ambaye hata ikitokea akapata majeraha ni pengo kwa wekundu hao wa Msimbazi.

Katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting ambao Simba ilishinda mabao 4-0 alifunga bao.


Malickou Ndoye - Azam FC (bao 1)

Mchezo dhidi ya Yanga ambao timu hizi zilitoka sare ya mabao 2-2 alifunga bao moja matokeo yaliyoipa timu yake pointi moja.


Djuma Shaban - Yanga (bao 1)

Ushindi wa mabao 3-0 ambao Yanga iliuvuna kwa Mtibwa Sugar Djuma alifunga bao moja.


Shafik Batambuze - Singida BS (bao 1)

Pointi tatu ambazo Singida ilivuna dhidi ya Ihefu bao moja pekee alilofunga beki huyo liliwaongezea pointi walima alzeti hao.


Shawn Oduro - Geita Gold ( bao 1)

Beki huyu wa wachimba mgodi wa Geita katika matokeo yao ya mabao 4-2 waliyoyavuna dhidi ya Tanzania Prisons alifunga bao moja.


Nichoulas Wadada - Ihefu (bao 1)

Beki wa zamani wa Azam FC katika mchezo na Coastal Union ambao timu yake ilishinda mabao 2-1 alifunga bao moja.