Azam FC wanataka ubingwa

Tuesday September 28 2021
azam pic
By Ramadhan Elias

MATAJIRI wa Ligi Kuu Bara, Azam FC ipo kamili kuanza kuusaka ubingwa ambao wameupoteza tangu msimu wa 2013/2014.

Ni miaka mingi tangu watwae ubingwa huo, wanasota kuupata na msimu uliopita walimaliza wakiwa nafasi ya tatu nyuma ya Simba iliyotetea ubingwa huo na Yanga iliyoshika nafasi ya pili.

Nao walipiga kambi yao kujiandaa na msimu mpya nchini Zambia, kambi iliyokuwa ya wiki mbili na kurejea nyumbani.

Ikiwa huko ilicheza mechi za kirafiki tatu dhidi ya Zanaco na kushinda 1-0, Kabwe Wariors ikashinda 1-0 na kufungwa 4-0 na Red Arrows.

Kocha mkuu wa timu hiyo, Mzambia George Lwandamina anasema kambi hiyo ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa huku akitamba morali ya wachezaji wake kuwa juu.

“Tulianza kwa mazoezi ya utimamu wa mwili kisha tukamaliza kwa mbinu na mifumo na katika kila hatua tulipata mechi za kirafiki na kujua nini tuongeze.

Advertisement

Nafurahi wachezaji wote wanamorali kubwa na sasa tupo tayari kwa kwa msimu mpya,” anasema Lwandamina.


UWANJA KAMA MBELE

Kuhusu Uwanja sio suala gumu kwa Azam kwani wana uwanja uliokidhi viwango vyote vinatakiwa, unatumika kwa michuano ya ndani na nje.

Uwanja huo una uwezo wa kuingia mashabiki 10,000, una nyasi bandia huku wakiwa na mwingine wa nyasi za kawaida ambao wanatumia kujifua pia.

Msimu huu Azam katika uwanja huo wamefunga mabango ya umeme ambayo yamezunguka uwanja na sasa matangazo yatakuwa yanapita kama yale ya Ulaya na sio kwa mabango ya mbao tena.

Pia taa zimefungwa nyingine mpya na za kisasa zaidi hivyo mechi zitaendelea kupigwa mchana na usiku kwa viwango vya kimataifa.


MASTAA WAPANIA

Mastaa wapya wa Azam, beki kitasa Mcameroon Yvan Mballa, kiungo mkenya Keneth Muguna na kipa Mganda Mathias Kigonya na winga Iddi Nado wamezungumza kuelekea msimu mpya huku wakionesha kupania.

“Nimekuja Azam kufanya kazi, nimejipanga kushirikiana na wenzangu kuhakikisha tunatwaa ubingwa msimu huu,” anasema Mballa. Muguna anasema; “Azam ni timu ambayo kila mchezaji Afrika Mashariki anatamani kuichezea kwani ina kila kitu. Nadhani ujio wangu hapa ni kuipa mataji na kuwapa furaha mashabiki wetu,”

Naye Kigonya anatamba kuwa; “Nataka niwaoneshe watanzania ubora wangu msimu huu, nadhani naenda kuwa kipa bora pale ligi itakapo malizika,”

Kwa upande wa Nado anasema “msimu uliopita ulikua bora kwangu, nmejipanga msimu huu kuwa bora zaidi pia natamani kuona tukibeba ubingwa,”


VIONGOZI WAMALIZA KAZI

Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdukarim Amin ‘Popat’ anafunguka maandalizi ya timu hiyo kuelekea msimu mpya huku akisema kazi imeisha na sasa wanataka ligi ianze wakiwashe.

“Tumejipanga kwa kila kitu, kikosi na benchi la ufundi wanatekeleza vyema majukumu yao na sasa tunasubiri ligi ianze tu.

Kama uongozi tumemaliza kila kitu na sasa tumejipanga kufanya na kusimamia kila linalotuhusu ili kuhakikisha hakuna matatizo ndani ya Klabu,” anasema Popat.


JESHI HILI HAPA

Azam msimu huu ina wachezaji 29 ambao ni makipa wanne, Mathias Kigonya, Wilbol Maseke, Salum Salula na Zuberi Foba. Mabeki ni Nicolaus Wadada, Bruce Kangwa, Daniel Amoah, Edward Manyama, Abdul Hamahama, Aggrey Morris, Lusajo Mwaikenda, Abdulkheri Sebo na Yvan Mballa.

Viungo ni Salum Abubakar, Mudathir Yahya, Frank Domayo, Khelfin Salum, Never Tigere, Charles Zulu, Keneth Muguna, Tepsi Evance, Sospeter Bajana, Ismail Kader, Iddi Seleman, Ayoub Lyanga, Paul Katema. Washambuliaji ni Idris Mbombo, Prince Dube na Rogers Kola.

Advertisement