Ahamada: Tatizo ni Yanga tu

MWILI jumba alionao na wasifu wake alikotoka, umemfanya Ali Ahamada kubeba matumaini makubwa ya mashabiki wa Azam FC, wanaoamini atatisha kwenye milingoti mitatu.

Hata hivyo, mwishoni mwa mwaka jana kipa hii aligeuka gumzo katika mitandao ya kijamii baada ya kufungwa mabao 3-2 walipolala mbele ya Yanga kwenye Uwanja wa Mkapa ikiwa ni mechi ya Ligi Kuu Bara.

Kipa huyo namba moja wa Azam amekuwa miongoni mwa makipa waliofungwa mabao ya nje ya 18. Na katika mchezo huo alifungwa mabao mawili na kiungo Feisal Salum 'Fei Toto', huku moja likifungwa na Stephane Aziz Ki.

Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, kipa huyo amefunguka mambo kadhaa huku akiitaja Yanga kwamba ndio tatizo la kushambuliwa kwake lilipoanza, huku akitamba wanaomzoea sasa ndio watakaomshangilia kesho, kwani anajua kilichomleta nchini;

Kumbe beki
Anasema kucheza nafasi ya kipa haikuwa ndoto yake tangu alipoanza kujifunza soka, kwani alianza kucheza ndani nafasi ya beki baadaye kiungo mshambuliaji.

“Nafasi ya kipa nilianza siku moja baada ya kukosekana kwa kipa kwenye timu yetu, niliombwa kucheza langoni kwa kuwa hatukuwa na kipa  siku ile, ila bahati nzuri nilicheza vizuri na kumvutia  kocha ambaye aliamua kunipa namba tangu siku hiyo."

Kipa huyo anasisitiza kuwa mara baada ya kujiimarisha golini hana mpango wala hafikirii kuacha nafasi hiyo kwani anaifurahia na anacheza kwa moyo wote.

Kutua Azam
“Niliingia mitandaoni na kutafuta taarifa zake, nafurahi nilipata taarifa za kuridhisha na kutosha zilizonipa picha muhimu kuhusu soka la Tanzania, nilijifunza kuwa Ligi ya Tanzania ina mashabiki wengi, Watanzania wanapenda soka na Azam ni miongoni mwa timu kubwa zenye mazingira mazuri kwa wachezaji,” anasema.

Kuhusu maisha ya Tanzania, Ahmada anasema; “Nafurahia sana maisha ya hapa hayana tofauti na nilikotoka, ni rahisi kuzoea, utamaduni wa Comoro na Tanzania siyo tofauti sana,” anasema kipa huyo ambaye anayependa kula chakula aina ya ndizi na Chapati ambavyo hata kwao vipo.

Tatizo Yanga
“Nimejifunza na kutambua dabi mbili dhidi yetu huwa ni Simba na Yanga, hizi ndizo mechi zinazopendwa kutazamwa na wengi pia zinatoa changamoto kubwa."

"Tulipofungwa mabao 3-2 na Yanga, nilichogundua ni kwamba mashabiki wanapenda furaha tu,” anasema Ahamada na kuongeza kwa Simba wamekutana nao mara moja na kuwafunga bao 1-0 na ushindi huo ulileta furaha na shangwe kuanzia kwa viongozi hadi wachezaji.

Kuhusu mastaa wa Azam; “Winga wetu Kipre Junior na Tape Edinho ni miongoni mwa sajili bora ndani ya timu ni wachezaji wazuri wanavipaji na wanavutia namna wanavyocheza hawachoshi kuwatazana kutokana na kucheza mpira wa akili na sio kutumia nguvu.” anasema Ahamada ambaye amecheza na staa Alexandre Lacazette, anayekipiga kwa sasa Olympique Lyon.

Mashuti mbali
Kipa huyo pia amezungumzia namna anavyofungwa mabao ya mbali ambapo anasema;

“Mawasiliano baina ya kipa na mabeki yanatakiwa kuwa sahihi muda wote ili kipa afanye maamuzi ndani ya sekunde na kuendelea kuliweka lango salama, lakini wakati mwingine mawasiliano ya haraka yanakosekana.

“Sasa makosa yanapotokea matokeo ya mchezaji na kipa kutokaa sawa katika kulinda lango, juhudi za wote zinatakiwa, sio kweli kwamba naogopa mashuti ya mbali au mashuti ya chini,"anasema na kuongeza kwamba kwa ushindani ulivyo kwenye msimamo wa Ligi lolote linaweza kutokea.

Aomba muda zaidi
“Nimecheza muda mrefu Ulaya na nimepata uzoefu wa kutosha, hapa Afrika ni mara yangu ya kwanza, nahitaji muda kidogo kuzoea mazingira ila napenda maisha na namna tunavofanya mazoezi na kujiandaa na mechi,” anasema.

Wasifu
Jina: Ali Ahamada
Kuzaliwa: Agosti 19, 1991
Mahali: Martigues
Nchi: Ufaransa
Uraia: Comoros/ Ufaransa
Nafasi: Kipa
Klabu: Azam FC
Jezi: Namba 30
Alikopita: Martigues, Toulouse, Kayserispor, Kongvinger, Brann na UE Santa Coloma