TFF imechemka kwa hili la Kabwili

Monday November 23 2020
tff pic

Miaka mingi, Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) limekuwa likituhumiwa kwa kutawaliwa na rushwa katika nyanja tofauti; utoaji wa uenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia, uuzaji wa haki za televisheni na mikataba mingine ya udhamini.

Kila mara Fifa imekuwa ikiahidi kuusafisha mchezo huo na jitihada kubwa zilikuwa za kuunda Kamati ya Maadili na kuweka rushwa kuwa moja ya makosa ya kimaadili.

Na kuonyesha kuwa haina mchezo na kosa hilo, Fifa na vyama wanachama vimekuwa vikitoa adhabu kali kwa wanaokutwa na kosa hilo.

Lakini rushwa ni moja ya makosa magumu kubainika, ingawa katika masuala ya haki za televisheni, utoaji wa uenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia na masuala kama ya kubeti huwa ni rahisi kutokana na kuhusisha taarifa ambazo ni lazima zikaguliwe wakati fulani.

Lakini masuala kama ya upangaji matokeo unaohusisha viongozi, waamuzi na wachezaji huwa ni vigumu. Lakini Fifa ilianzisha idara mbili ndani ya Kamati ya Maadili; ya uchunguzi (investigatory chamber) na ya kushtaki (adjudicatory), ambazo wajumbe wake wana mbinu na miongozi ya jinsi ya kubaini rushwa.

Na kwa kufuata moja ya misingi mikuu ya Fifa kuwa masuala yake, ambayo inaweza kuyashughulikia, hayaendi mahakamani, Kamati ya Maadili hufanya uchunguzi wa kutosha kuhakikisha anayechunguzwa anatendewa haki, hivyo kuondoa ulazima wa kwenda mahakamani.

Advertisement

Lakini mwongozo wa maadili, unaeleza kuwa mbali na kuadhibu kimpira, mchezo unaweza kumshtaki katika mahakama za kawaida mtu aliyetenda kosa linalofikia hali ya uhalifu kama rushwa na kughushi.

Rais wa zamani wa Fifa, Sepp Blatter aliadhibiwa na Kamati ya Maadili hata kabla ya waendesha mashtaka wa Zurich kukamilisha uchunguzi wao kuhusu muamala kutoka kwake kwenda kwa aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa), Mitchel Platini; kwanza kusimamishwa kwa siku 90 na baadaye kwa miaka kadhaa.

Mwaka jana, Fifa iliwafungia maisha waamuzi watatu wa Botswana kwa kuchukua rushwa ili kupanga matokeo.

Hivyo, haiingiii akilini kwamba Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) inasubiri Takukuru ichunguze suala la kipa wa Yanga kusema kulikuwa na njama za kumpa rushwa na yuko tayari kusema ukweli.

Huko ni kukwepa kuwajibika. TFF haijafanya jitihada zozote kulichukua suala hilo na kuona ugumu wa kufikia mwisho, kiasi cha kuamua kuiachia Takukuru iendelee.

Nilidhani taarifa ya wiki hii ya TFF, ingeeleza wamelishughulikia kiasi gani na wamefikia hatua ya kuviachia vyombo vya dola viwajibike.

Vyombo vya maamuzi vilivyoundwa nje ya utaratibu wa mahakama za kawaida, vina kazi ya kutafuta ukweli halisi wa kilichotokea na si kuwapa nafasi wanaoshtaki na wanaoshtakiwa kushindana kwa kujua sheria na taratibu za kisheria kiasi cha kesi kuishia hatua za awali.

Lengo ni kupata ukweli halisi na kuchukua hatua kuhusu ukweli huo. Ni kiasi gani ukweli huo unapatikana, ni jukumu ambalo TFF inatakiwa ishughulikie ili kuliwezesha kufanya maamuzi ya mpira kwa wakati na bila ya kuonea.

Mmoja angeuliza “Mbona nyinyi mlivyokuwepo TFF hamkufanya hivyo”, jibu linaweza kuwa rahisi; kwamba kila anayeingia pale anaendeleza pale mwingine alipoishia, kama anavyoahidi wakati wa kampeni za kutaka kuchaguliwa.

Hakuna mgombea ambaye huwa anaahidi kuwa atarudisha nyuma maendeleo, bali atayapeleka mbele tena kwa kasi kubwa kuliko yule anayeondoka.

Rushwa ni doa kubwa katika soka na huondoa ushindani wa haki na inapozidi, hata unazi unapungua na wadhamini wanakimbia.

Nadhani TFF itarekebisha taarifa yake iliyojibu hoja moja kati ya tatu ilizoziweka bayana kuhusu uvumi dhidi ya shirikisho hilo kutochukulia hatua mambo kadhaa yanayowasilishwa kwake.

Advertisement