Stars isikate tamaa bado inayo nafasi

Stars isikate tamaa bado inayo nafasi

WAPENZI wa soka kama vile wamekata tamaa kutokana na matokeo iliyoipata Taifa Stars Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumatano wiki hii, katika harakati za kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Africa (Afcon).

Baada ya kupoteza 1-0 kule Tunisi wengi waliamini Taifa Stars ingeweza kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa marudiano ikiwa nyumbani.

Bahati mbaya, Stars ikiwa nyumbani ilianza kuruhusu bao dakika ya 11 ya mchezo kwa bao safi lililofungwa na Saif- Eddine Khaoui, lakini dakika mbili baada ya timu hizo kutoka mapumziko, Feisal Salum ‘Fei Toto’ akaisawazishia Stars na kuufanya mchezo huo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Tunisia sasa inaongoza Kundi J ikiwa na alama 10 baada ya kushinda michezo mitatu na kuambulia sare moja.

Equatorial Guinea inashika nafasi ya pili ikiwa na alama sita, Tanzania nafasi ya tatu na alama zao nne huku Libya ikiburuza mkia baada ya kukusanya alama tatu katika michezo minne.

Taifa Stars bado inayona nafasi ya kutimiza lengo kama itajipanga kwa michezo miwili iliyobaki hasa kwa kuangalia msimamo wa kundi hilo namna ulivyo hadi sasa.

Mchezo unaofuata utakuwa mwishoni mwa mwezi Januari mwaka ujao, itakuwa ugenini kucheza na Equatorial Guinea ambayo inasaka ushindi kwa namna yoyote ili kujihakikishia kufuzo Afcon.

Bila kupepesha macho, Stars inapaswa kupambana ili kusaka alama tatu ugenini, ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kufuzu na endapo itapoteza basi ile safari ya matumaini kwa mara nyingine itakuwa imeishia hapo.

Endapo Stars itafanikiwa kuvuna ushindi itapanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi J ikiwa na alama saba huku Equatorial Guinea ikibaki na alama zao sita wakati mchezo wa mwisho ikipambana na Tunisia itakayokuwa imekwishajikatia tiketi.

Mchezo wa mwisho utafanyika Tanzania Marchi 30 na Taifa Stars ikiikaribisha Libya ambao kwa sasa ni vibonde lakini katika mchezo uliopita ilituchapa kwa mabao 2-1 licha ya Stars kutangulia kupata bao dakika ya 18 kupitia mkwaju wa penalti iliyopigwa na Mbwana Samatta.

Sio kazi nyepesi lakini maandalizi mazuri ndio yatakayoifanya timu kuwa na matokeo mazuri maana jambo jema siku zote hutokana na mamaandalizi mazuri.

Upande wa mashabiki huko hakuna shaka zaidi ya kutaka ushindi kwa timu yao kikubwa kilichobaki ni kwa upande wa mamlaka na wadau mbalimbali kuhakikisha inaiwekea mazingira mazuri timu.

Maandalizi mabovu siku zote yanazaa matokeo mabovu, hapa haipaswi kuwa na maandalizi ya zima moto ambayo mwisho wa siku zinatolewa sababu zisizokuwa na mashiko masikioni mwa Watanzania.

Mwanaspoti kama mdau mkubwa wa michezo nchini linachukua nafasi hii kukumbusha mamlaka na wadau kuungana kwenye jambo hili mapema iwezekanavyo ili kuiendeleza ile furaha ambayo tumekuwa nayo kwa muda mrefu katika hamasa ya mcho wa soka kwa timu ya Taifa.

Penye nia kuna njia na mchezo wa soka siku hizi kila kitu kinafanyika wazi bila makandokando, ukifungwa kila mmoja anaona hilo. Maandalizi ndio chachu ya kila jambo.