Staili za ushangiliaji zilibamba na kupotea

BURUDANI ya soka imebebwa na vionjo vingi kama mabao, ushindani, viwango vya wachezaji pamoja na aina za ushangiliaji.

Msimu wa 2018/19 ziliibuka staili nyingi za ushangiliaji, kali zaidi zilitoka kwa mastaa wa Simba na Yanga, zilizokuwa zimebamba hadi mtaani ambako ukipita utawasikia ama kuwaona mashabiki wao wakiziiga.

Mastaa waliokuwa wanashindana kwa staili za ushangiliaji wakizitikisha nyavu za wapinzani ni Heritier Makambo (Yanga) na Meddie Kagere (Simba), jamaa hao walibamba mtaani, maofisini hadi kwenye mitandao ya kijamii.

Ulikuwa ukisikia makofi ya ujazo yalikuwa yanamtambulisha Makambo kwamba tayari alishazichakaza nyavu za wapinzani wao, wakati Kagere ukiona mashabiki wake wanafumba jicho moja iliashiria kafunga bao.

Baada ya msimu wa 2019/20 Makambo kuachana na Yanga na kwenda kujiunga na Horoya ya Guinea staili yake iliendelea na kuigwa na baadhi ya wachezaji wa timu nyingine, lakini kadri siku zilivyoenda ikapotea.

Staili ya Kagere ya kufumba jicho moja iliendelea wakati anang’ara msimu ulioisha, ila kwa msimu huu imekuwa tofauti kabisa umarufu wa kushangilia kwake ni kama umepotea licha ya kwamba hadi sasa katupia mabao 11.

Mwanaspoti limebaini kupungua kwa mvuto wa ushangiliaji msimu huu, tofauti na iliyopita ambayo wachezaji walikuwa wanashindana baada ya kuzifungia timu zao mabao na kuwafanya mashabiki watambe nazo mitaani.

Ukiachana mastaa hao waliotamba zaidi, bado wapo wengine wanaocheza Ligi Kuu Bara ambao staili zao zinatamba na kupotea, huku janga la covid 19 likichangia kwa kiasi kikubwa kwani wakati linaingia ilikuwa ngumu kugusana.


MUKOKO TONOMBE - YANGA

Kiungo mkabaji kutoka DR Congo, amesajiliwa na Yanga msimu huu tayari ameonyesha staili yake ya ushangiliaji katika mabao matatu anayoyamiliki zilizompa jina la utani ‘Mwalimu’.

Mukoko akifunga anakimbilia kwenye kibendera, anawaita wachezaji wenzake kisha wanakaa chini anakuwa kama anawafundisha, baadae wanasimama na kuanza kucheza. Mwanzoni hii ilipata umarufu mkubwa lakini kwa sasa imefifia pengine ni kutokana na matokeo yasiyoridhisha ambayo timu yake imepata baadaye msimu huu na kupunguza mzuka uliokuwapo mwanzo wa msimu.


BENARD MORRISON - SIMBA

Yanga ndio ilikuwa ya kwanza kumsajili Morrison mwaka 2020, alicheza msimu mmoja tu, alikuwa na vionjo vingi ambavyo mashabiki walivipenda kama kupanda juu ya mpira, ukiachana na hiyo Msimbazi amepata kushangilia kwa kuuingiza mpira ndani ya bukta yake katikati ya miguu yake akiwakebehi Yanga waliomuanzishia utani kwamba alifanyiwa upasuaji wa henia.


STEPHEN SEY - NAMUNGO

Sey ameifungia Namungo mabao manne hadi sasa, ana staili ya aina yake tamu ya ushangiliaji na inayopendwea kuliko zote nchini. Hadi ligi za wanawake wakifunga bao wachezaji hushangilia kama Sey. Wanaiita staili ya kuwakera. Akikufunga kwanza anachomekea jezi yake kwenye bukta yake, kisha anatembea kwa maringo akipunga mkono juu kama wanavyotembea walimbwende wanapopita jukwaani.


YACOUBA SOGNE - YANGA

Upande wa straika Yacouba anayeongoza kwa mabao (7) Yanga, ana namna yake ya kuonyesha furaha mbele ya mashabiki anapokuwa amefunga bao, anatembea kwa mwendo wa ukakamavu kisha anakumbatiana na wachezaji wenzake na kurejea uwanjani, staili yake inabamba na kupotea.


WASEMAVYO MASHABIKI

Shabiki kindakindaki wa Yanga, Anwari Wambura ‘Yanga Kigelegele’ alizungumzia kupoa kwa staili za washangiliaji kwamba inatokana na matukio mbalimbali kama covid 19 na kusimama kwa ligi, hivyo moto wa wachezaji wa kuzifumania nyavu unapungua.

“Ligi ilisimama mwezi mzima kupisha msiba aliyekuwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli, kitendo cha wachezaji kukaa muda mrefu bila kucheza kinapunguza morali yao,” anasema.

Naye shabiki damudamu wa Simba, Justine Joel Mwakitalima ambaye ni Mtendaji Mkuu wa tawi la Ubungo Teminal, anasema anaamini kama straika wao Meddie Kagere angekuwa anacheza mara kwa mara kama alivyokuwa msimu miwili iliyopita angeendelea na staili yake ya kushangilia.