Njooni muige! Simba yaipa Yanga sifa ya unbeaten

ACHANA na rekodi nyingine za nyuma ulizowahi kuzisikia. Mjini leo Jumamosi gumzo la mashabiki wa Yanga ni moja tu. Kuendeleza rekodi ya kutopoteza mechi ya 49 kuifikia rekodi ya Arsenal ya England.

Mashabiki hao pamoja na viongozi wa Yanga wamekuwa wakiwakejeli Simba na Azam kwamba ; “Njooni muige.”

Staa wa Yanga, Fiston Mayele anayeongoza msimamo wa wafungaji akiwa na mabao manane, amesisitiza presha ni kubwa na ushindani ni mkali lakini lengo lao ni kuendeleza rekodi yao kwa heshima ya mashabiki.

Mbeya City ililazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Simba wiki hii nyumbani, rekodi zinaonyesha ugenini imeshinda mechi mbili tu dhidi ya timu zinazopumulia mashine za Dodoma Jiji na Ruvu Shooting.

Lakini Yanga haikumbuki lini mara ya mwisho kupoteza mechi yoyote nyumbani. Swali ni je? Yanga inaweza kufikia rekodi mpya kwenye Ligi Kuu Bara leo?

Yanga sasa imefikisha mechi 48. Rekodi hiyo ya Ligi Kuu Bara imedumu tangu mara ya mwisho mabingwa hao watetezi walipofungwa bao 1-0 na Azam Aprili 25, mwaka jana lililofungwa na Prince Dube. iko hivi;


USHINDI MICHEZO 36

Katika michezo 48 ambayo Yanga imecheza bila ya kufungwa kabla ya ule wa leo usiku dhidi ya Mbeya City ni 36 tu iliyoshinda kuanzia mara ya mwisho ilipopoteza kwa Azam FC huku 12 iliyobaki ikiisha kwa sare. Michezo iliyoshinda baada ya Azam ni (2-0) v JKT Tanzania (Mei 19, 2021), (3-2) v Ruvu Shooting (Juni 17, 2021), (3-2) v Mwadui (Juni 19, 2021), (1-0) v Simba (Julai 3, 2021), (2-0) v Ihefu (Julai 15, 2021), (1-0) v Kagera Sugar (Septemba 29, 2021), (1-0) v Geita Gold (Oktoba 2, 2021).

(2-0) v KMC (Oktoba 19, 2021), (2-0) v Azam FC (Oktoba 30, 2021), (3-1) v Ruvu Shooting (Novemba 2, 2021), (2-0) v Mbeya Kwanza (Novemba 30, 2021), (2-1) v Tanzania Prisons (Disemba 19, 2021), (2-1) v Biashara United (Disemba 26, 2021), (4-0) v Dodoma Jiji (Disemba 31, 2021).

(2-0) v Coastal Union (Januari 16, 2022), (1-0) v Polisi Tanzania (Januari 23, 2022), (2-0) v Mtibwa Sugar (Februari 23, 2022), (3-0) v Kagera Sugar (Februari 27, 2022), (1-0) v Geita Gold (Machi 6, 2022).

(2-0) v KMC (Machi 19, 2022), (2-1) v Azam (Aprili 6, 2022), (2-1) v Namungo (Aprili 23, 2022), (2-0) v Dodoma Jiji (Mei 15, 2022), (4-0) v Mbeya Kwanza (Mei 20, 2022), (3-0) v Coastal Union (Juni 15, 2022), (2-0) v Polisi Tanzania (Juni 22, 2022), (1-0) v Mtibwa Sugar (Juni 29, 2022).

(2-1) v Polisi Tanzania (Agosti 16, 2022), (2-0) v Coastal Union (Agosti 20, 2022), (3-0) v Mtibwa Sugar (Septemba 13, 2022), (2-1) v Ruvu Shooting (Oktoba 3, 2022), (1-0) v KMC (Oktoba 26, 2022), (1-0) v Geita Gold (Oktoba 29, 2022), (1-0) v Kagera Sugar (Novemba 13, 2022).

Michezo mingine waliyoibuka na ushindi ni (4-1) v Singida Big Stars (Novemba 17, 2022) na (2-0) v Dodoma Jiji (Novemba 22, 2022).

Katika michezo 12 iliyobakia ya sare ni (0-0) v Namungo (Mei 15, 2021), (0-0) v Dodoma Jiji (Julai 18, 2021), (1-1) v Namungo (Novemba 20, 2021), (0-0) v Simba (Disemba 11, 2021), (0-0) v Mbeya City (Februari 5, 2022), (0-0) v Simba (Aprili 30, 2022), (0-0) v Ruvu Shooting (Mei 4, 2022).

(0-0) v Tanzania Prisons (Mei 9, 2022), (1-1) v Biashara United (Mei 23, 2022), (1-1) v Mbeya City (Juni 25, 2022), (2-2) v Azam FC (Septemba 6, 2022) na (1-1) v Simba (Oktoba 23, 2022).


DHIDI YA SIMBA, AZAM

Kwenye kila safari ya mafanikio huwezi kukosa vikwazo ndivyo Yanga ilivyokutana na michezo migumu wa ‘Dabi ya Karikoo’ kutoka kwa Simba na ule wa Azam. Yanga ilikutana na Simba mara nne ikishinda moja (1-0) Julai 3, 2021, kisha mechi mbili zikaisha kwa suluhu Disemba 11, 2021 na Aprili 30, 2022 na sare ya 1-1 Oktoba 23, 2022.

Kwa upande wa Azam ambayo ndiyo iliyoifunga mara ya mwisho zimekutana mara tatu ikifungwa miwili (2-0) Oktoba 30, 2021, (2-1) Aprili 6, 2022 na sare moja ya 2-2 Septemba 6, 2022.


KIPIGO KIKUBWA

Ushindi mkubwa kwa Yanga katika hii ‘Unbeaten’ ni wa mabao 4-0 na Dodoma Jiji Disemba 31 mwaka jana sambamba na Mbeya Kwanza (inayoshiriki Championship) iliyofungwa pia 4-0 Mei 20, 2022.


MABAO YA KUTOSHA

Katika kipindi hicho chote safu ya ushambuliaji ya timu hiyo imefunga mabao 81 tu huku safu yake ya ulinzi iliyo chini ya nahodha, Bakari Mwamnyeto ikiruhusu mabao 18.

Mgawanyo wa mabao hayo ni kwamba tangu Aprili 25, mwaka jana Yanga ilicheza michezo saba kukamilisha msimu wa 2020/21 kati ya hiyo ilifunga 11 na kuruhusu kufungwa manne.

Msimu wa 2021/2022, mabingwa hawa watetezi walifunga 49 na kuruhusu manane na msimu huu wa 2022/23 tayari imecheza michezo 11 na kufunga 21 ikiruhusu sita hivyo kuifanya kufikisha 81 na kuruhusu 18.


POINTI NYINGI

Katika timu zilizochangia pointi nyingi za Yanga kwenye kipindi chote ni Dodoma Jiji na Maafande wa Ruvu Shooting kila moja alichangia pointi 10 katika michezo minne.

Yanga ilitoka suluhu na Dodoma Jiji Julai 18, 2021, kisha kushinda mabao 4-0 Disemba 31, 2021, (2-0), Mei 15, 2022 na (2-0) Novemba 22, 2022 huku Ruvu Shooting ikifungwa mabao 3-2, Juni 17, 2021, (3-1) Novemba 2, 2021, (2-1) Oktoba 3, 2022 na suluhu Mei 4, 2022.

Timu nyingine ni Kagera Sugar, Geita Gold, KMC, Coastal Union, Polisi Tanzania na Mtibwa Sugar ambazo zimeipa Yanga pointi zote tisa kila moja katika michezo mitatu.


YA KIPEKEE

Ushindi wa mabao 2-0 ilioupata Yanga dhidi ya Dodoma Jiji Novemba 22 mwaka huu inaifanya kutimiza mchezo wa 27 mfululizo kwa timu hiyo ugenini bila ya kufungwa tangu mara yake ya mwisho ilipofungwa na Coastal Union mabao 2-1, Machi 4, 2021 kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Fiston Mayele aliyefunga mabao yote mawili amevunja rekodi ya Dodoma Jiji ya kutokufungwa nyumbani na mchezaji wa kigeni wa Yanga tangu ilipopanda Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/20.


REKODI YA ARSENAL?

Moja ya jambo kubwa linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa Yanga ni kuifikia rekodi ya Arsenal inayoshiriki Ligi Kuu England iliyoiweka ya kucheza michezo 49 bila ya kufungwa. Rekodi hiyo iliwekwa msimu wa 2003/2004 kuanzia Mei 7, 2003 hadi ilipofika Oktoba 16, 2004.

Yanga inaweza kuifikia rekodi hiyo leo itakapocheza na Mbeya City kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa licha ya kusaka pointi tatu hata ikipata sare tu inaifikia.

Rekodi baina yao zinaonyesha Mbeya City tangu ipande rasmi Ligi Kuu Bara msimu wa 2012/13 imeifunga Yanga mara moja tu kwenye ushindi wa mabao 2-1 Novemba 2, 2016 katika michezo 18 waliyokutana.