MTU WA PWANI: Simba, Namungo hazijamaliza kazi kimataifa

Simba, Namungo msiwadharau wapinzani

WAWAKILISHI wanne wa Tanzania katika michuano ya klabu Afrika, Simba, Namungo, KVZ na Mlandege wikiendi hii watakuwa na mechi za marudiano za mashindano ya klabu Afrika.

Simba itarejeana na Plateau United kutoka Nigeria katika mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Namungo itakuwa katika Uwanja wa Azam Complex kuikabili Al Rabita ya Sudan Kusini.

Mlandege ya Zanzibar yenyewe itakuwa ugenini huko Tunisia kuikabili CS Sfaxien ya huko, wakati KVZ wao waikuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar kucheza mechi ya marudiano dhidi ya Al Amal Atbara ya Sudan.

Kati ya wawakilishi hao wanne, Simba na Namungo ndizo zinaoonekana ziko katika mazingira mazuri ya kutinga raundi ya kwanza ya mashindano zinazoshiriki kulinganisha na Mlandege na KVZ kutokana na matokeo zilizopata katika mechi za kwanza mwishoni mwa wiki iliyopita.

Simba ilipata ushindi wa bao 1-0 ugenini wakati Namungo yenyewe iliibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 lakini hali ilikuwa mbaya kwa KVZ na Mlandege ambazo zilianza kwa vipigo.

KVZ ilichapwa bao 1-0 na Al Amal Atbara ugenini huko Sudan na hali ilikuwa mbaya zaidi kwa ndugu zao Mlandege ambao waliangushiwa kichapo kizito cha mabao 5-0 nyumbani na CS Sfaxien.

Inawezekana kwa KVZ kusonga mbele katika hatua inayofuata ikiwa wataibuka na ushindi wa angalau mabao 2-0 nyumbani lakini ni miujiza tu itakayowaokoa Mlandege ambao ili wasonge mbele, wanapaswa kuibuka na ushindi wa mabao kuanzia sita ugenini huko Tunisia, jambo ambalo kiuhalisia haliwezi kutokea kwa mazingira yanayowakabili mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Zanzibar.

Hata kwa Simba na Namungo ambazo zipo katika mazingira mazuri ya kufuzu kwa hatua inayofuata zikihitaji ushindi ama sare ya aina yoyote katika mechi zao za mwishoni mwa wiki hii hazipaswi kubweteka na kuona zina urahisi wa kufanya hivyo kwa kuangalia kile zilichokivuna katika mechi zilizopita.

Zinapaswa kujiandaa kikamilifu na kuingia uwanjani kwa kupambana kana kwamba hazikupata matokeo mazuri kati mechi za mwanzo ili ziweze kupata ushindi ambao utazihakikishia kutinga katika raundi ya kwanza ya mashindano zinazoshiriki.

Mabenchi ya ufundi ya timu hizo yanatakiwa kuwaandaa vyema wachezaji wao kimbinu, kiakili na kimwili ili waweze kuwa bora zaidi ya wapinzani wao jambo litakalowawezesha kupata matokeo mazuri kirahisi katika mechi hizo.

Huenda mechi za mwanzo zilikuwa na ugumu kwao kwa vile walikua hawajapata fursa ya kutazama wapinzani wao na kubaini ubora na udhaifu wao lakini zinaingia katika mechi hizi zikiwa na utafiti wa kutosha juu ya Al Rabita na Plateau United zilivyo kiufundi ambao bila shaka utawasaidia katika maandalizi yao kuelekea mechi hizo.

Na zikumbuke kwamba wapinzani wao wamepata fursa ya kuwatazama na kufahamu ubora na udhaifu wao na bila shaka wanaufanyia kazi kuona wanawezaje kupindua matokeo ya mechi za mwanzo na kupata ushindi katika mechi hizi ili waweze kusonga mbele.

Namungo na Simba wanapaswa kuweka akilini kwamba mchezo wa soka umekuwa na matokeo ya kikatili na ya ajabu ambayo yanaweza kutokea pasipo kutegemea tofauti na matarajio ya wengi hivyo hazipaswi kuruhusu hilo kutokea mbele ya Plateau United na Al Rabita.

Iko mifano mingi ya jinsi baadhi ya timu zilipata ushindi wa kushangaza katika mechi za marudiano licha ya kupata matokeo mabaya katika michezo ya mwanzo ya mashindano mbalimbali.

Watanzania wana kumbukumbu ya mwaka 1979 ambapo Simba ilipindua matokeo kiajabu dhidi ya Mufulila Wanderers ya Zambia katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika licha ya kuchapwa kwa idadi kubwa ya mabao katika mechi ya kwanza.

Ikiwa nyumbani jijini Dar es Salaam, Simba ilifungwa mabao 4-0 na timu hiyo ya Mufulila lakini ziliporudiana huko nchini Zambia, iliwashangaza wenyeji kwa kuibuka na ushindi mnono ugenini wa mabao 5-0 ambao uliwavusha kuwapeleka katika hatua iliyofuata.

Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, mwaka jana katika mashindano ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (Chan), ilifungwa bao 1-0 hapa nyumbani Dar es Salaam lakini ikaibuka na ushindi wa mabao 2-1 ugenini ambao uliwafanya wafuzu fainali hizo.

Kuna orodha ndefu ya matokeo ya namna hiyo hivyo Simba na Namungo zinapaswa kuyatumia kama chachu ya kujiandaa vyema na kumaliza kazi iliyobakia vinginevyo zinaweza kuacha majonzi nyumbani kama zikidharau wapinzani wao.