Mtihani Taifa Stars ya Ndayiragije, namba hazidanganyi

Mtihani Taifa Stars ya Ndayiragije, namba hazidanganyi

Muktasari:

  • Stars imefikisha alama nne katika kundi J ikishika nafasi ya tatu nyuma ya Guinea ya Ikweta iliyo na pointi sita, ikiwafuata vinara, Tunisia wenye alama 10, huku Libya ikiburuza mkia katika kundi hilo kwa kuwa na pointi tatu.

MASHABIKI wa soka nchini, kwa sasa wanapiga hesabu za vidole kuhusu hatima ya timu ya taifa ya soka, Taifa Stars katika safari yake ya kufuzu ushiriki wa Fainali za Kombe la Afrika (Afcon) 2021.

Hii ni baada ya timu hiyo kupata matokeo ya sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Tunisia na kuipa kazi ya kuupanda mlima mrefu wa safari hiyo ya kwenda Cameroon zitakazopofanyikia fainali hizo.

Mlima huo kwa Stars unakuwepo kutokana na kupata msimamo wa kundi J ulivyo kwa sasa baada ya matokeo ya mechi za raundi ya nne ya mbio hizo za kuwania Afcon 2021.

Stars imefikisha alama nne katika kundi hilo ikishika nafasi ya tatu nyuma ya Guinea ya Ikweta iliyo na pointi sita, ikiwafuata vinara, Tunisia wenye alama 10, huku Libya ikiburuza mkia katika kundi hilo kwa kuwa na pointi tatu tu kwa sasa.

Kila timu kundini kwa sasa imesaliwa na michezo miwili kabla ya kujua hatima yao, Stars ikiwa na kibarua kigumu ugenini dhidi ya Guinea ya Ikweta kisha kumalizia nyumbani dhidi ya Libya, mechi ambazo ndizo zitakazoamua kama itaenda fainali hizo kwa mara ya pili mfululizo.

Mwaka uliopita, Stars chini ya Kocha Emmanuel Amunike ilienda Misri zilizopofanyika fainali za Afcon 2019, ingawa iliishia kupata aibu kwa namna ilivyochapika kwenye mechi zao zote tatu za kundi lililotoa timu zilizofika fainali, yaani Senegal na Algeria walionyakua taji kibabe.

Hesabu zilivyo ni kwamba, kama Stars itapoteza ugenini dhidi ya wenyeji wao, Guinea ya Ikweta mechi itakayopigwa Machi mwakani, maana yake biashara itakuwa imeishia hapo, kwa vile hata kama itashinda mchezo wa nyumbani baadaye mwezi huo dhidi ya Libya, hautawasaidia lolote.

Ili ndoto za Watanzania kuona Stars ikienda tena kwenye fainali za Afcon ni lazima ishinde ama ipate sare ugenini kisha kuhakikisha inashinda nyumbani dhidi ya Libya, ambayo nayo itakuwa ikiombewa mabaya kundi kwenye mechi yao dhidi ya Tunisia.

Kwa kuangalia namba zilivyo mpaka sasa kundi ni wazi, Kocha Etienne Ndayiragije na vijana wake wana kazi kubwa ya kuhakikisha wanajipanga mapema kabla ya mapema mwakani kuamua hatima ya Tanzania kama itaenda Cameroon ama la!

Ugumu wa Stars unatokana pia na rekodi ambazo timu hiyo imekuwa ikiyapata tangu iwe chini ya Mrundi huyo, aliyewahi kuzinoa klabu za Mbao FC, KMC na Azam FC, kwani kocha tangu akabidhiwe timu akimpokea Amunike, ameiongoza katika mechi 12.

Mwanaspoti linakuletea tathmini ya makocha watatu waliopita Stars akiwamo Charles Boniface Mkwasa, Salum Mayanga, Emmanuel Amunike na Etienne Ndayiragije kila mmoja katika michezo yake 12 ya awali na kuonyesha namna gani Mrundi huyo alivyo na kibarua cha kumfunika mtangulizi wake Amunike ambaye aliiongoza Stars katika mechi nane tu kisha kuipeleka Stars Afcon 2019.


ETIENNE NDAYIRAGIJE

Tangu apewe timu Julai mwaka jana, Ndayiragije ameiongoza Stars katika mechi 12, ameshinda mbili na kupoteza nne na michezo mingine sita akimaliza kwa kutoka sare.

Katika mechi hizo, kocha huyo raia wa Burundi, alishinda michezo mingine miwili ya hatua ya mtoano kwa mikwaju ya penalti, iliyoivusha Stars kwenda Chan na hatua ya makundi ya Kombe la Dunia.

Chini ya Ndayiragije Stars imefanikiwa kufunga mabao tisa na wao kuruhusu kufungwa mabao kumi katika michezo 12.

Ndayiragije alianza kibarua kwa kukutana na timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars katika mechi ya kufuzu Chan ambayo alikuwa nyumbani katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na pambano hilo la majirani wawili kumalizika kwa suluhu, matokeo ambayo yalikuja kujirudia katika mechi ya marudiano.

Baada ya hapo Ndayiragije aliingoza Stars katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Burundi ugenini ikamalizika kwa sare ya bao 1-1, na mechi ya marudiano nayo ilimalizika kwa matokeo ya aina hiyo hiyo. Baada ya hapo Stars ilinyooshwa na Sudan kwa kufungwa bao 1-0 nyumbani katika mechi ya kufuzu Chan.

Chini ya Ndayiragije, Stars walicheza mechi ya kwanza ya kirafiki na Rwanda ugenini ambayo ilimalizika kwa suluhu, baada ya hapo walirudiana na Sudan ugenini katika mechi ya kufuzu Chan walipata ushindi wa mabao 2-1, ambayo yalifungwa na Erasto Nyoni na Ditram Nchimbi na Tanzania kutinga fainali hizo zilizoahirishwa, kwa faida ya bao la ugenini.

Baada ya hapo, Stars walitupa karata yao ya kwanza kwenye Afcon wakiwa kundi J dhidi ya Guinea ya Ikweta kwenye Uwanja wa Mkapa na wakashinda mabao 2-1, Ndayiragije na kikosi chake walicheza mechi ya pili ugenini dhidi ya Libya wakapoteza kwa kufungwa mabao 2-1.

Stars wakiwa nyumbani walicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Burundi walikubali kufungwa bao 1-0, kabla ya kwenda kupata matokeo kama hayo katika mechi ya tatu ya kundi J la Afcon dhidi ya Tunisia ambao Novemba 17 walirudiana nao kwenye Uwanja wa Mkapa na dakika tisini zilimalizika kwa sare ya bao 1-1.


EMMANUEL AMUNIKE

Kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike aliichukua Taifa Stars Agosti 06, 2018 hakukaa kwa muda mrefu kwani alikiongoza kikosi hicho katika michezo minane tu. Alishinda mechi mbili, sare moja na kupoteza mechi tano. Timu yake ilifunga mabao saba na kuruhusu mabao 12.

Mechi ya kwanza Amunike kuiongoza Stars ilikuwa kufuzu Afcon dhidi ya Uganda ambayo ilimalizika kwa suluhu, baada ya hapo kwenye mashindano hayo hayo alikwenda kupasuka kwa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Cape Verde ambao alikuja kurudiana nao Dar es Salaam na kuwafunga mabao 2-0.

Stars chini ya Amunike walikubali kufungwa nyumbani kwa mara ya kwanza na Lesotho katika mchezo wa kufuzu Afcon, kabla ya kupata ushindi wa kishindo wa mabao 3-0, dhidi ya Uganda matokeo ambayo yaliwavusha mpaka kwenye mashindano ya Afcon ambayo yalifanyika Misri.

Wakiwa Misri na Amunike katika fainali za Afcon 2019, Stars walipoteza mechi ya kwanza na Senegal wakifungwa mabao 2-0, wakapoteza mechi ya pili katika kundi dhidi ya majirani zao Kenya kwa kufungwa mabao 3-2, huku mechi ya mwisho na mabingwa wa mashindano hayo msimu huo Algeria walifungwa tena 3-0.


REKODI ZA MAYANGA

Kocha wa Tanzania Prisons msimu huu, Salum Mayanga amewahi kuinoa Taifa Stars kuanzia Januari 2, 2017, katika michezo 16, aliiongoza timu kushinda mechi saba, kutoka sare saba, kufungwa mbili. Walifunga mabao 19 na wao kufungwa mabao 14.

Rekodi zinaonyesha katika makocha wanne waliopita kwa nyakati tofauti, Ndayiragije, Boniface Mkwasa, Emmanuel Amunike na Mayanga, ni Mayanga ndio ameonekana kufanikiwa zaidi kutokana na rekodi zake ziilivyo kabla ya kuondolewa katika nafasi hiyo.

Mechi ya kwanza kwa Mayanga ilikuwa ya kirafiki dhidi ya Botswana ambao walikubali kufungwa mabao 2-0, baada ya hapo akashinda tena dhidi ya Burundi kabla ya kwenda kutoka sare ya 1-1 na Lesotho katika mchezo wa kufuzu Chan.

Baada ya hapo Mayanga aliiongoza Stars katika michezo sita ya Cosafa akianza na Malawi ambao aliwafunga mabao 2-0, suluhu na Angola, sare ya bao 1-1 na Mauritius, akawafunga wenyeji Afrika Kusini bao 1-0, akapoteza dhidi ya Zambia kwa mabao 4-2, kabla ya kushinda kwa penalti 4-2, kwenye mechi ya mshindi wa tatu.

Mechi yake ya kumi ilikuwa ya kufuzu Chan dhidi ya Rwanda ambayo ilichezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza na ukamalizika kwa sare ya bao 1-1, kabla ya kurudiana nao Kigali, Rwanda na mchezo ukamalizika kwa suluhu.

Baada ya hapo Mayanga aliiongoza Stars katika mechi ya kirafiki na Botswana kwenye Uwanja wa Uhuru na ukamalizika kwa Stars kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, wakacheza mechi nyingine mbili za kirafiki dhidi ya Benin ambayo iliisha kwa sare ya bao 1-1, kabla ya kumaliza kibarua chake kwa kushindo kwa kumfunga DR Congo mabao 2-0.


BONIFACE MKWASA

Kocha wa Ruvu Shooting msimu huu, Boniface Mkwasa alikiongoza kikosi cha Stars kwa muda wa miaka miwili akianzia Juni 23, 2015 mpaka Januari 2, 2017, walicheza mechi 13, walishinda mbili, sare nne, vipigo saba, walifunga mabao nane na wao kufungwa 22.

Mkwasa alianza kibarua kwa sare ya bao 1-1 katika mechi ya kufuzu Chan ugenini dhidi ya Uganda, baada ya hapo Stars ilicheza mechi ya kirafiki na Libya na kufungwa mabao 2-1, walitupa karata yao ya kwanza kufuzu Afcon dhidi ya Nigeria wakiwa nyumbani walimaliza dakika tisini kwa suluhu.

Baada ya hapo Stars waliibuka na ushindi wa mabao 2-0, nyumbani dhidi ya Malawi katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia na siku chache baadaye walirudiana na Malawi waliokuwa nyumbani walishinda bao 1-0.

Stars ya Mkwasa ilicheza mechi mbili za kufuzu kombe la dunia dhidi ya Algeria ya kwanza iliyokuwa hapa Tanzania iliisha kwa sare ya mabao 2-2, kabla ya kwenda kuchezea kipigo kikubwa cha mabao 7-0, kwenye mji wa Bliga Algeria.

Baada ya hapo walicheza mechi ya kirafiki na Afrika Kusini ambayo Stars walikubali kufungwa mabao 2-0, Stars waliwakaribisha Chad katika mechi ya kufuzu Afcon Uwanja wa Benjamin Mkapa na wakaibuka kwa ushindi 1-0.

Stars walicheza mechi ya kirafiki na Kenya ambayo iliisha kwa sare 1-1, baada ya hapo walikwenda kucheza mechi mbili za kufuzu Afcon dhidi ya Misri wakafungwa mabao 2-0, Nigeria bao 1-0, Mkwasa alimaliza kibarua chake kwa kufungwa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Zimbabwe katika mechi iliyochezwa mji wa Harare.

___________________________________________________________________

Na THOBIAS SEBASTIAN