Morocco: Hii Namungo mbona bado kidogo tu
SIKU chache kabla ya kuanza majukumu yao ya mechi za kimataifa, ikishiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Namungo FC ilifanya mabadiliko katika benchi la ufundi kwa kumtema Hitimana Thierry na kumchukua Hemed Suleiman ‘Morocco’.
Kocha huyo kutoka visiwani Zanzibar alianza na mguu wa bahati kwani alikiongoza kikosi chake kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Al Rabita kutoka Sudan Kusini, siku chache tangu walipoupiga mpira mwingi dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu ulioisha kwa sare ya 1-1.
Baada ya kupata matokeo hayo na kukaa katika kikosi kwa muda wa wiki mbili amezungumza baadhi ya mambo ambayo amepanga kuyafanya ili kikosi hiko kuwa kama moja ya timu tishio nchini kwa muda wote ambao atakuwa akifanya kazi pamoja na changamoto anazokutana nazo.
Morocco aliyewahi kuzinoa klabu kadhaa tofauti ikiwamo Coastal Union na Mbao FC, ni mmoja wa makocha wazoefu nchini aliyewahi kuzifundisha timu za taifa za Zanzibar na Taifa Stars akisainiana na makocha mbalimbali akiwamo Emmanuel Amunike aliyeenda naye Afcon 2019.
TIMU ILIVYO
Morocco anasema kwa muda aliokaa katika kikosi hicho amegundua kikosi kinayumba kutokana na wachezaji waliokuwapo wengi wao wana uwezo lakini katika kila nafasi moja kuna wachezaji si chini ya wawili ambao wanauwezo wa kuwania nafasi hiyo kucheza.
“Timu nimeikuta katika hali nzuri kutokana na wachezaji wote waliokuwepo wengi ni wakomavu na wamecheza ligi kwa uzoefu katika timu tofauti ambazo tukiunganisha nguvu kwa pamoja tunapata kikosi kinachoweza kutoa ushindani wa kutosha katika mashindano yote msimu huu.”
“Kocha aliyeondoka ameonekana kufanya kazi na kuiacha timu katika hali nzuri kwani wachezaji walikuwa tayari kwa kushindana ila akili na hali zao zilikuwa chini kutokana na wengine kutokupata nafasi ya kucheza na kuna ambao ufiti wa miili yao umekuwa chini.
USAJILI
Morocco anasema katika dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa Desemba 15, hafikirii kusajili lundo kubwa la wachezaji kwani waliokuwa ndani ya timu wengi wao wana uwezo na muda mwingine wanashindwa kupata nafasi ya kucheza kwani katika mechi moja wanatumika 14 tu.
“Hakuna kocha ambaye anaweza kubadili kikosi chake kwa timu ambayo huwa inapata matokeo mazuri kwa maana hiyo kuna wimbi kubwa la wachezaji ambao watakuwa hawapati nafasi ya kucheza huku wakiwa na uwezo wa kupewa nafasi hiyo,” anasema Morocco na kuongeza;
“Zoezi kubwa ambalo nadhani linaweza kufanyika katika kikosi changu ni kupunguza zaidi wale wachezaji ambao hawataweza kuendana na kasi ya timu lakini kushindwa kupata nafasi ya kutumika mara kwa mara hata kama tumefanya mabadiliko,” anasema.
SHIDA
“Hakuna kizuri ambacho kinakosa kasoro’ ni kauli ambayo aliingeza kocha Morocco kuwa mbali ya kikosi hicho kuwa na wachezaji wazuri lakini kuna baadhi ya mapungufu ambayo anaendelea kuyafanyia kazi mara kwa mara anapokuwa mazoezini.
“Shida ya kwanza ambayo imekuwepo kabla ya kufika hapa Namungo wamekuwa wakitengeneza nafasi nyingi za kufunga katika kila mechi lakini mastraika au washambuliaji wamekuwa wakishindwa kuzitumia kwa kufunga mabao mengi ambayo pengine wangekuwa nayo zaidi ya hivi sasa,” anasema.
“Ukiachana na shida hiyo ya kukosa mabao ambayo naifanyia kazi wakati huu na naimani watabadilika na mambo kuwa mazuri nimebaini tatizo lingine wachezaji wengi hawana utimamu wa kimwili na kucheza huku wakiwa hawapo fiti kucheza katika kiwango cha juu muda wote.
KOMBE LA FA
Namungo msimu uliopita walicheza fainali na Kombe la Shirikisho (ASFC), dhidi ya Simba na ilipoteza ila walipata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa kutokana na sheria ya wakati huo kuwabeba ambayo ilisema kama bingwa wa ligi atacheza fainali ya (ASFC), mwanafainali mwenza ndio ataiwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Morocco anasema mashindano hayo ya ASFC ni njia rahisi kwao kucheza mashindano ya kimataifa kama wataweza kuchukua ubingwa ambao safari yake hauna michezo zaidi ya kumi ambayo ukifanikiwa kushinda yote mambo yanakuwa safi kwa upande wao.
“Nimeanza kazi kwenye timu niliyokuwa na deni nayo kwa maana msimu uliopita walicheza fainali ya mashindano haya kwa maana hiyo natakiwa kutengeneza timu na mipango thabiti ili kuona nalipa deni hilo kwa kwenda kucheza tena fainali msimi huu ili kupata nafasi ya kucheza mashindano ya kimataifa kwa mara nyingine.
LIGI KUU BARA
Namungo ipo nafasi ya 12, katika msimamo wa ligi mpaka sasa ikiwa na pointi 15, huku wakicheza michezo 11, Morocco anasema ambacho anahitaji ni kuona kikosi chake kinakaa katikati ya timu tatu za juu Simba, Yanga na Azam.
“Tunakazi kubwa ya kufanya kwanza tunatakiwa kuhakikisha tukikutana na timu hizo tatu za juu tunachukua pointi tatu dhidi yao ili kupunguza umbali wa pointi baada ya hapo kutokukubali kirahisi kupoteza dhidi ya timu ambazo zinaonekana ni madaraja ya kati,” anasema.
“Tukifanikiwa katika hilo tutaishi katika ndoto zetu za kuwepo katikati ya wakubwa hao wa ligi lakini kama ikiwa tofauti na hivyo tutaendelea kupambana chini katika msimamo kama tulivyo wakati huu jambo ambalo sitamani kuona linatokea kwa upande wetu,” anasema.
MALENGO YAKE
Katika hatua nyingine Morocco anasema malengo yake kwa muda ambao atafundisha kikosi hiko cha Namungo kinakuwa na mafanikio katika mashindano yote ambayo watakuwa wanashiriki, kuwa miongoni mwa timu ambayo ikicheza inatoa ushindani na si kugawa pointi kirahisi.
“Miongoni mwa klabu ambazo nimewahi kufundisha na wameonekana kuwa sitiazi katika maisha yake ya soka kuanzia wachezaji, masuala ya kiuchumia na mambo mengine yote ni Namungo bado ni timu changa lakini inamaono ya kufanya vizuri na kufika mbali jambo ambalo natamni kutoa mchango wangu ili kulifanikisha hilo.
By THOBIAS SEBASTIAN