KIBANDA UMIZA: Shabiki Simba azima TV kibandani kisa Mayele

Ukisikia utani usioumiza ndio huu sasa. Wakati mechi ya Yanga na Geita Gold inaendelea kule Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza wadau wa kibanda umiza walikita kambi Buguruni Malapa.

Sasa wakati mechi ndio kwanza inaanza na Yanga kupata bao la mapema, baadhi ya mashabiki wa Simba waliokuwa kibandani hawakuwa wamekata tamaa na waliamini kuwa Geita huenda ikasawazisha.

Lakini kadri muda ulivyokuwa unaenda na mchezo kufikia kipindi cha pili, mashabiki wa Simba waliokuwa kibandani mmoja mmoja alikuwa akiondoka.

Kilichokuwa kinajiri wakati huo ni kwamba kila aliyekuwa anaondoka alikuwa akizomewa sana na wengine walienda kuvutwa wasiondoke hadi mchezo umalizike.

Hata hivyo, baadhi yao walikuwa wakijinasua kwa nguvu na kuonyesha hali ya kuhamaki ilhali wengine walikuwa wakichomoka mbio kama mishale.

Sasa kituko kilikuwa kwa mmoja wao ambaye yeye wakati anatoka alikimbia kwa kasi huku watu wakimzomea lakini aliwakomesha kwani alipofika mlangoni tu alizima TV na kukimbilia nje.

Baadhi ya watu waliokuwepo kwenye banda hilo walitoa kauli chafu na wengine walibaki kusonya.