Janeth nusura atengwe na familia, kisa urefa

WANAWAKE ni jeshi kubwa. Ukitaka kujua hilo fuatilia vitu vikubwa wanavyovifanya sawa na wanaume, licha ya jamii yao baadhi kuwa na mtazamo tofauti dhidi yao.

Hata kwenye michezo, hususan soka, kuna kina mama ambao wanajitoa kupambana kufanya kazi ambazo zinaonekana kuwahusu zaidi wanaume ikiwemo kazi ya uamuzi (marefa) kwenye soka.

Janeth Balama, ni miongoni mwa waamuzi wa soka ambao wanachezesha Ligi Kuu Bara ambaye ana beji ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), amefanya mahojiano na Mwanaspoti ambapo ameeleza mambo mbalimbali juu ya kipaji chake.

Janeth, mzaliwa wa Mkoa wa Iringa, anasema miaka ya hivi karibuni dunia imekuwa ikithamini mchango wa kazi zinazofanywa na wanawake na kuzipa kipaumbele, jambo ambalo linawatia moyo wanawake kupambana zaidi.

Anasema awali ilionekana kwamba kazi kubwa ya wanawake ni kulea familia, huku kazi za ofisini na nyinginezo zinazohitaji nguvu kubwa zikitambuliwa kuwa ni za kufanywa na wanaume.

Mwanamama huyo anasema hivi sasa vichwa na akili za wanawake wengi vimefunguka japokuwa kuna baadhi yao bado hawajaona fursa ya kuonyesha vipaji walivyojaliwa na Mungu, ili kuwa miongoni mwa watu muhimu katika ujenzi wa taifa.

“Lazima kila mwanamke anayesikia kwa mfano siku ya wanawake ajione bora, kwa sababu anaamini ni wa thamani na mwenye kupendwa, kiukweli tuna nafasi kubwa katika maendeleo ya taifa tofauti na mwanzo ambapo ilikuwa inajulikana kwamba mwanamke kazi yake ni kulea familia tu,” anasema Janeth.

“Sasa hivi ukiangalia tuna uwezo wa kufanya mambo makubwa kama wanavyofanya wanaume na pengine kuwazidi hata wanaume pale wanapofikia kiuwezo ama utendaji wa kazi.”


ALIINGIAJE KWENYE UREFA?

Janeth anasema katika familia yao ya watoto wanne wa hayati mzee Balama hakuna aliyekuwa anacheza soka wala kujihusisha na mambo ya michezo.

Anasema, lakini yeye michezo aliipenda tangu akiwa mdogo na alitamani alipokutana na watu hususan wanaume wakifanya mazoezi aliotaka kuungana nao.

Mwamuzi huyo anasema 2007 ndipo alianza kujihusisha rasmi na masuala ya mpira, akijikita kwenye uamuzi na mambo yalimnyookea na kufanya vizuri.

“Kwa sababu nilikuwa na dhamira tangu nikiwa mtoto sikutaka kujinyima haki yangu ya kutimiza ndoto ambayo inaonekana kwa sasa, niliamua kuthubutu, sasa nimekuwa miongoni mwa waamuzi wenye beji kubwa katika nchi yangu.”


CHANGAMOTO

Janeth anataja changamoto kubwa kwamba wakati anaanza kazi ya uamuzi, wazazi na ndugu zake walikuwa hawapendezwi na kazi hiyo kabisa, lakini aliamua kukaza kambi hadi walipomuelewa nini alikuwa anamaanisha.

“Walichukizwa sana na kazi hiyo, hata wakati nikiwa mdogo nilikuwa nazuiwa kucheza mpira, hivyo haikuwa kazi rahisi kupambana hadi kufikia hatua ya kukubaliana nami - sio baba, mama wala ndugu niliozaliwa nao,” anasema.

Janeth anaeleza kuwa, “Mafanikio yangu ni makubwa na familia yangu imeelewa na kutambua mchango wangu katika kazi ninayoifanya, lakini nitakuwa nimekosa fadhila kama sitalishukuru Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB), kwa msingi walionijengea hadi kuwa mwamuzi wa kutegemewa tena beji kubwa ya Fifa.”

Anasema semina na mafunzo yanayotolewa na TFF vimemuongezea wigo mpana na anakuwa mwepesi wa kwenda kujifunza na kufuatilia vitu ili kufika mbali zaidi.

“Kuna mafunzo na kozi huwa tunapata kutoka TFF, lakini kwa muda niliopo katika kazi hii nimeongeza elimu hadi kupata beji ya Fifa, kwa sasa familia imeelewa vizuri kuhusu kazi hii,” anasema.

Mwanamama huyo anasema mbali na changamoto ya kifamilia, lakini hata mechi ya kwanza kuchezesha Ligi Kuu Bara 2013 akisimamia mchezo kati ya Azam FC na Kagera Sugar ilimpa presha, lakini alitiwa moyo na wenzake na viongozi wa Bodi ya Ligi.

Anafafanua kuwa tangu ameanza kazi, licha ya changamoto za hapa na pale, lakini hakuna tukio kubwa lililowahi kumpata isipokuwa baadhi ya timu kulalamika baada ya kupoteza michezo.

“Sijawahi kupatwa na tatizo kubwa kama kupigwa, isipokuwa timu huwa zinalalamika baada ya kupoteza mechi, hii nayo ni changamoto lakini naiona ndogo, naendelea kupambana nazo kuona ni namna gani soka letu litakuwa bora zaidi.”


NDUGU WASHAWISHIKA

Janeth anasema kuwa kutokana na mafanikio aliyonayo, sambamba na ndugu katika ukoo ambaye ni Mapinduzi Balama anayekipiga Yanga, wamewashawishi wengine kupenda kazi ya soka na kuiona kuwa sio ya kihuni. “Ukifanya kitu kikawa na faida lazima watu wakipende, kwa hiyo mafanikio yangu na Mapinduzi yule wa Yanga yameweza kuwaamsha hata ndugu wengine kutamani soka,” anasema Janeth ambaye hajaolewa wala kuzaa mtoto.


NENO KWA WANAWAKE

Mwamuzi huyo anawashauri wanawake wenzake kujitambua na kujishughulisha ili kuendeleza tunu zao katika ujenzi wa taifa, lakini akiwataka zaidi kutochagua kazi.

Anasema hakuna kazi isiyo na faida au hasara, lakini kwanza lazima wajitume na kupenda wanachoweza kujishughulisha nacho kwa faida yao na taifa kwa ujumla.

“Hakuna kisichowezekana kwa sababu kwa sasa mambo yamebadilika, niwashauri hata hawa wasichana wajitokeze kwenye michezo, fursa ni nyingi, kimsingi kumtanguliza Mungu.”