DATA ZAKE: NEYMAR: Bonge la Bwana

Tuesday August 22 2017
ney

NEYMAR da Silva Santono Junior. Alizaliwa Mogi das Cruzes huko Sao Paulo, Brazil. Baba yake ni Neymar Santos na mama yake ni Nadine da Silva. Amerithi jina la baba yake, ambaye pia alikuwa mwanasoka na sasa ndiye mshauri wa mwanaye. Alizaliwa Februari 5, 1992 na kimo chake cha sasa ni futi 5 na inchi 9.

Mwaka 2003, Neymar na familia yake walihamia Sao Vicente na huko ndiko alikoenda kuanza kucheza mpira wakati alipojiunga na timu ya watoto ya Portuguesa Santista kabla ya kunaswa na Santos FC. Santos FC ndiko maisha ya soka la kulipwa yalikoanzia kwa upande wa Neymar na kisha akatua Barcelona na sasa Paris Saint-Germain, ikimnasa kwa pesa iliyoweka rekodi mpya kwenye uhamisho wa wachezaji duniani, Euro 222 milioni.

Katika maisha yake ya soka, Neymar amekuwa mtu wa pesa tu. Saini yake haipatikani kirahisi kama unavyodhani. Mwaka 2010, Santos iligomea ofa ya Pauni 12 milioni kutoka kwa West Ham United waliokuwa wakimtaka mchezaji huyo. Chelsea nao mwaka huo huo walipeleka ofa ya Pauni 20 milioni, nayo ikapigwa chini na Santos. Kwa maana haikuwa ikitosha kupata saini ya staa huyo. Miaka mitatu baadaye, Barcelona walifanikiwa kukamata saini ya Neymar. Saini ya Neymar imeripotiwa kuigharimu Barcelona hadi Euro 86.2 milioni. Mwanzoni ilielezwa kwamba dili hilo lilikamilika kwa Euro 57.1 milioni. Lakini, kulikuwa na nyongeza kibao za pesa ikiwamo mkwanja aliolipwa baba yake karibu Euro 40 milioni. Mara ya kwanza tu Neymar aliponaswa na Barcelona akasainishwa mkataba wa miaka mitano na mkataba wake uliwekewa kipengele cha Euro 190 milioni kwa timu itakayohitaji kuvunja huo mkataba. Neymar baadaye alisainishwa mkataba mpya huko Barcelona na hapo kipengele hicho cha kwenye mkataba wake kiliboreshwa zaidi na sasa kikawa Euro 222 milioni na hakika ndizo ilizolipa Paris Saint-Germain kupata huduma yake. Akiwa na Barcelona, Neymar alipiga pesa za kutosha tu, kabla ya sasa kutua huko Ufaransa ambako amekuwa mmoja wa wanasoka wanaolipwa mshahara mkubwa kabisa duniani na kukaa anga moja.

Advertisement