Waziri Bashungwa, Chamudata wamlilia Waziri Sonyo

Waziri wa Habari, Utamuduni, Sanaa na  Michezo, Innocent Bashungwa ameeleza kupokea  kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mwanamuziki wa dansi Waziri Sonyo  kilichotokea Kibaha mkoani Pwani.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, ilyoitolewa leo Jumatano Februiri 24, 2021, Waziri Bashungwa amesema kifo cha mwanamuziki huyo ni pigo katika sekta ya Sanaa kwa ujumla.

“Hili ni pigo katika tasnia kwa kwani  Sonyo ni mmoja wa wasanii waliochangia kukuza tasnia ya muziki wa dansi nchini ambao ni miongoni mwa mtindo wa muziki unaopendwa,”amesema.

Kutokana na msiba huo, Bashungwa ametoa pole kwa familia, chama cha Muaziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA), wasanii, wadau wote wa tasnia ya Sanaa, ndugu jamaa na marafiki na kuwaombea wote wapate nguvu na moyo wa ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu.

Kwa upande wake Chamudata kupitia katibu wake, Hassan Msumari, amesema watamkumbuka Waziri Sonyo kama moja ya wasanii wa kizazi kipya katika muziki wa dansi walioleta mapinduzi na kuufanya muziki huo kuwa wa kisasa na kuendelea kupendwa.

“Kama unakumbuka kipindi cha jina la Sonyo lilipokuwa juu, ndio kipindi waliibuika wasanii kama wakina Banza Stone, Jose Mara na wengine wa kizazi chao ambao waliendeleza gurudumu la muziki huo na kufanywa kupendwa na wengi wakiwemo vijana,”alisema Msumari.