Wasanii wa Hip Hop walioimba na wa Taarabu

KWA mtazamo wa watu wengi muziki wa Taarabu ni aina ya muziki inayopendwa zaidi na wanawake. Dhana hii imekuwepo muda mrefu licha ya kwamba maeneo ya Pwani, Taarabu ni aina kuu ya muziki tangu enzi na inasikilizwa na jinsi zote.

Kwa upande mwingine, mtazamo wa watu wengi kuhusu muziki wa Hip Hop, ni muziki unaopendwa zaidi na wanaume. Dhana ambayo pia inajengeka kwa sababu idadi kubwa ya wasanii wanaofanya aina hiyo ya muziki ni wanaume.

Mitazamo juu ya aina hizi mbili za muziki imesababisha Taarabu na Hip Hop kuonekana ni aina mbili ya miziki tofauti kabisa kiasi kwa haraka haraka ni kama ladha zake haziwezi kuchanganywa.

Hata hivyo, bila kujali mitazamo hiyo, kuna wasanii wa Hip Hop na Taarab waliamua kuangana na kutengeneza kazi pamoja na kushangaza wapenzi wa muziki nchini.


Chid Benz vs Mzee Yusufu

Rashid Makwiro A.K.A Chidi Benz aliwashangaza mashabiki wa muziki baada ya kumshirikisha mfalme wa Taarabu, Mzee Yusufu katika wimbo wake wa ‘Mashallah’.

Wimbo huo wenye vigezo vyote vya kuitwa ‘classic’ uliachiwa mwaka 2012 na kufanya ionenake ni kitu kirahisi kuchanganya muziki wa Taarabu na Hip Hop.

Jukumu la Mzee Yusufu kwenye wimbo huo ilikuwa ni kuimba kiitikio pamoja na kibwagizo. Wakati Chidi Benz yeye aliimba beti mbili zilizoshiba.

Zaidi ni Mzee Yusufu alijaribu kwenda nje ya mipaka yake kwa kutumia maneno ambayo labda huwa hayatumiki sana kwenye taarabu. Maneno kama vile ‘msela’ na ‘wazushi’; ‘Labda ni macho yanayowazuzua, ndo maana masela hawaishi kupakazia’.


Fid Q ft Bi Kidude

Mwaka 2009 Fid Q aliachia albamu yake ya kuitwa Propaganda, wimbo nambari tatu ndani ya albamu hiyo ulikuwa unaitwa Juhudi za Wasiojiweza na alikuwa amemshirikisha nguli wa taarabu Afrika, marehemu Bi Kidude.

Kilichoshangaza zaidi ni katika wimbo huo Bi Kidude hakuimba taarabu au hata kuimba kwa mtindo unaofanana na taarabu, badala yake alichana mashairi kwa mtindo wa ‘spoken words’ huku ubeti wake ukiwa na mistari migumu inayohitaji kujua lugha na kutuliza akili kuilewa.

Sehemu ya mistari ya Bi Kidude inaimbwa; Mzoea Punda hapandi farasi, hapandi farasi kwake si mzuri, nguo za hariri kwake si fahari, kwake si fahari huona najisi, huona najisi kweli nakwambia.

Hata hivyo, wimbo huo ulikuja kuwa maarufu zaidi mwaka 2013 baada ya Fid Q kuuachia kama singo baada ya kifo cha Bi Kidude ambaye jina lake halisi ni Fatma binti Baraka — Bi Kidude alifariki Aprili 2013.


Fid Q ft Isha Mashauzi

Msanii wa taarabu Isha Mashauzi amewahi kukiri yeye ni shabiki mkubwa sana wa FId Q. Ili kuthibitisha hilo, Isha amewahi kutumia mistari ya Fid Q kutoka kwenye wimbo wa Progranda kama kibwagizo kwenye wimbo wake wake wa Sura Surambi. Mistari hiyo inasema; Tunachukiana kwa sababu tunaogopana, tunaogopana kwa sababu hatujajuana, hatujuani kwa sababu tunatengana, dunia ni nzuri walimwengu hawana maana.

Mwaka 2019 Fid Q aliamua kumshirikisha shabiki yake Isha Mashauzi kwenye wimbo wa kuitwa Bam Bam. Katika wimbo huo Isha aliimba ubeti wa pili pamoja na kiitikio, pia hakushikishwa peke yake, alikuwepo Rich Mavoko na Big Jah Man.


Bonge la Nyau ft Khadija Kopa

Mwaka 2018 rapa bishoo kutoka Kariakoo Bonge la Nyau aliachia wimbo wake wa kuitwa Nipe Matamu. Katika ngoma hiyo ya mapenzi Bonge la Nyau alimshirikisha mama yake na Zuchu, malkia Khadija Kopa.

Khadija aliimba kiitikio cha kisasa cha kibongofleva kwa kukinakshi na ladha za taarabu wakati bonge la nyau alishambulia biti kwa verse mbili zilizoshiba.


Weusi ft Khadija

Ngoma ya kwanza mwaka huu kutoka kwa wawakilishi wa A City inaitwa Penzi la Bando, zaidi ni kwa mara ya kwanza wagumu hao kutoka Arachuga wameamua kufanya na msanii wa Taarabu, Khadija Kopa.

Katika wimbo huo wasanii wa Weusi yaani Joh Makini, Nikki wa Pili, Lord Eyez na G Nako wamechana kwenye verse nne wakati malkia wa mipasho, Bi Khadija kopa ameimba Kiitikio.

Iadha katika wimbo huo msanii Jux amefanya sauti za nyuma (back vocal) na kufanya kuwa ni wimbo wa kwanza kukusanya sauti nyingi zaidi kwa mwaka 2021.