Wasanii kuanza kukopeshwa mwaka huu wa fedha

Dar es Salaam. Serikali imesema kuanzia mwaka huu wa fedha , wasanii wataanza kukopeshwa fedha kwa ajili ya kurahisisha kufanya kazi zao.
Hayo yamesema jana Jumapili Mei 9, 2021 na Katibu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Hassan Abbas, katika hafla ya uzinduzi wa tamthilia ya ya ‘We Men’.
Dk Abbas amesema fedha hizo watazipata kupitia mfuko wa  utamaduni wa wasanii, ambao unaanza kufanya kazi rasmi mwaka wa bajeti 2021/2022.
“Tayari mfuko huo wa wasanii umepangiwa bajeti yake na kuanzia mwaka huu wa fedha  wasanii mtaweza kunufaika nao ikiwemo kupata mikopo ya kuboresha kazi zenu.
“Hivyo ni wakati sasa wa wasanii kuwa karibu na vyama vyenu na taasisi zinazowasimamia wakiwemo Basata, Cosota na Bodi ya filamu, ambao hawa watahusika kwa karibu katika kuratibu suala hili.
Katibu huyo amesema kurejesha mfuko huo kutaondoa yale malalamiko ya mtu kuwa wazo na kushindwa kuliwazua kisa hana fedha.
Mfuko huo ulianzishwa Novemba 2019 katika kongamano la Sanaa la Mwalimu Nyerere lililofanyika mkoani Dar es Salaam, ambapo Waziri Mkuu siku hiyo aliuchangia Sh5 milioni huku Hayati  John Magufuli aliahidi kuuchangia Sh100 milioni katika uanzishwaji wake.
Katika hatua nyingine, Katibu huyo aliitaka StarTimes kampuni ambayo itaonyesha tamthilia hiyo ya ‘We Men’ kuongeza vipindi vya Kiswahili na kueleza kuwa kwa sasa kazi za sanaa nyingi zimeboreshwa.
“StarTimes iendelee kuingia ubia na wadau mbalimbali, kuna vipaji vingi, kuna filamu nyingi, hivyo naamini vipindi vingi vya kitanzania vitaonyeshwa kwenye kisimbusi chenu. kwani naamini tumetoka kwenye ile ya jambazi kuvua viatu,” anasema Dk Abbas.
Naye Meneja masoko StarTimes, David Malisa, amesema wamejipanga katika kukuza kazi za Sanaa hapa nchini, ambapo kwa mwaka 2020 katika kampuni hiyo jumla ya filamu 104 zimeonyeshwa huku Sh280 Milioni  zikiwa zimewekezwa kwa shughuli hiyo.
Kwa pande wake Max Rioba ambaye ni muandaaji wa tamthilia, amesema wamejitahidi kuiandaa filamu hiyo katika kiwango cha kimataifa na wanaamini italeta mapindusi katika tasnia ya filamu kwa ujumla.
Wasanii waliopo katika filamu hiyo ni pamoja na Max mwenyewe, Wema Sepetu, Shilole, Hemed Suleiman na Grace Mgonjo ambaye ni mke wa Profesa Jay.