Wasafi waweka sharti jipya

Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz ambaye pia ni bosi wa tamasha la Tumewasha linaloandaliwa na Wasafi Media amesema tamasha lao halitafanya kazi na msanii ambaye hajasajiliwa Baraza la Sanaa Taifa (Basata).

Diamond ambaye anatamba wa wimbo wa Waah aliomshirikisha Koffi Olomide kutoka DRC Congo amesema hayo wakati akitoa ratiba ya tukio la mwisho la tamasha hilo litakalofanyika Januari 30, Dar es Salaam katika Uwanja wa Uhuru kuanzia saa sita mchana.

"Agizo hili tumepewa na Basata wenyewe. Wamesema msanii yoyote ambaye hajasajiliwa asipande jukwaani. Kwahiyo na sisi hatuko tayari kuona tunafungiwa tamasha eti kwa sababu ya mtu mmoja." Amesema Diamond.

Aidha, Diamond amesema kwa msanii ambaye hajasajiliwa labda kwa sababu ya kushindwa kumudu gharama za usajili Basata anaruhusiwa kufanya mazungumzo na wao Wasafi kisha watamlipia gharama za usajili halafu watawakata kwenye malipo yao ya utumbuizaji.

"Kwahiyo hata wasanii ambao hawajasajili labda kwa sababu ya gharama za usajili, na ikiwa sisi tunawataka kwenye tamasha letu, tunayo option ya kuwalipia gharama za usajili na kisha tutakata kwenye malipo ya kufanya shoo." Amesema.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu Ofisa Sanaa Muandamizi wa Basata, Abel Ndaga amebainisha kuwa gharama za msanii kujisajili ni kiduchu kiasi kwamba haiwezi kuwa sababu ya msanii anayefanya kazi kushindwa kujisajili.

Ameeleza kuwa gharama ni Sh 45,000 tu na hapa anaeleza mchanguo wake;

"Elfu tano unalipia fomu, elfu ishirini unalipia gharama za usajili na elfu ishirini inayobaki ni malipo ya kibali cha kufanya sanaa ambacho utakuwa unalipia kila mwaka. Kwahiyo mtu akijisajili leo Januari 19 atalipia tena mwakani siku kama ya leo. Amesema.

Aidha, kabla ya tamasha hilo kufanyika, Wasafi watafanya kongamo na wasanii ambalo litawakutanisha wataalamu wa sekta ya burudani na sanaa nchini kwa ya kupeana A, B, C za namna ya kuwa msanii bora na mwenye ushawishi sokoni.