Ukistaajabu ya Ma Dangote utayaona ya Harmonize

BASI bwana!, Mama mzazi wa msanii Diamond Platnumz, Bi. Sandra maarufu kama ‘Mama Dangote’ akaamua kupindua meza ya Harmonize kibabe kwa madai, Mzee Abdul Juma Issack si baba halisi wa Diamond kama inavyofahamika bali ni baba mlezi.

Mama Dangote anaeleza hilo baada ya miaka 31 kupita kitu kilichoibua mjadala mzito mtaani na hata kwenye mitandao.

Kwa mujibu wa mama huyo asiyeishiwa visa vya uswahilini, Baba halisi wa Diamond ni Salum Iddy Nyange. Hata hivyo hilo limepingwa vikali na Mzee Abdul ambaye ameeleza kushangazwa na kauli hiyo.

Je, lakini kwanini hayo yanajiri sasa baada miaka 31? Kipi kipo nyuma ya pazia? Ni swali linalowaumiza wengi vichwa na kubaki kustaajabu hayo ya Mama Dangote. Hata hivyo, ukistaajabu ya Bibie huyo, basi utayaona ya Harmonize kwa wepesi zaidi. Kwanini?

Takribani wiki mbili zilizopita Harmonize aliachia wimbo wake uiitwao ‘Wapo’ ambao unadaiwa kuchokonoa mambo katika famili ya Diamond hasa jinsi wanavyoishi na Mzee Abdul.

Wimbo huo ulikuja baada ya kusambaa kwa picha za Mzee Abdul zikimuonyesha katika hali ya uchovu akipanda daladala huku akiwa ameninginiza gunia begani. Wengi wakahoji inakuwaje baba mzazi wa msanii maarufu Afrika ambaye anavuna fedha nyingi kwenye muziki na miliki biashara kuishi maisha yale.

Lakini pia wimbo huo ulikuwa ni kama jibu kwa Diamond baada ya kudaiwa kutupa madongo ya nguvu kwa Harmonize kupitia nyimbo mbili za ‘Shusha na Bado Sana’ alizoshirikishwa na Baba Levo na Lava Lava.

Inasemekana hasira hiyo ya Mondi ni kutokana na kile kinachoelezwa kuwa Konde Boy alimchana vikali kwenye wimbo wake, ‘Ushamba’.

Wakati hilo bado linatokota, Harmonize akiwa anatumbuiza katika fainali ya Mapinduzi Cup iliyowakutanisha Simba SC na Yanga SC visiwani Zanzibar akaamua kutumbua jibu.

“Mama na Baba ndio nguzo ya dunia watunze, sio Baba Dangote analia, Mama Dangote anacheka” aliimba Harmonize akiwa amechomea majina hayo ambayo hayapo kwenye wimbo halisi.

Hilo likatoa mwanga kuwa mstari huo katika wimbo huo ulikuwa rasmi kwa Diamond jinsi anavyoishi na wazazi wake ambapo mara nyingi ameonekana kuwa karibu zaidi na mama kwa kila hali kuliko baba.

Hazikupita siku nyingi, ndipo Mama Dangote akaamua kupindua meza, kama Harmonize alikuwa anatumia hilo kama upepo kwa kutembelea baharini, basi Mama Dangote kasimamisha kimtindo Jahazi la Konde Boy.

Hapo ndipo Mama Dangote anastaajabisha zaidi. Je, kwanini aibue hayo aliyoibua siku chache baada ya kauli ya Harmonize?, alichoshwa na kilele hizo?. Pengine kama sio Harmonize asingeibuka na kufichua hilo liloteka mazungumzo kila kona ya mji na kuwaongezea siku wapenda ushubwada.

Sasa baada ya kustaajabu hayo ya Mama Diamond, karibu uone ya Harmonize anayechokonoa ya wenzake. Kumbe naye ana mambo, si haba. Kijana na visa huyo!.

Desemba 2020 Harmonize aliibuka mtandaoni na kumtambulisha mtoto wake wa kike aitwaye, Zuu ambaye alidai kumpata nje ya ndoa yake na mke wake, Sarah. Zuu alitambulisha tayari akiwa na umri wa mwaka mmoja na miezi saba.

Harmonize alienda mbali zaidi na kumuomba msamaha Zuu kwa kutokuwa na muda naye hata kushindwa kumjuli hali kipindi alichokuwa akiumwa ili kulinda ndoa yake kitu ambacho kimekuwa kikimtesa.

Ikumbukwe Harmonize na Sarah alifunga ndoa Septemba 2019, hadi kufikia Desemba 2020 ni takribani miezi 16 hivi. Zuu akaibuliwa akiwa na umri wa mwaka mmoja na miezi saba, sawa na takribani miezi 19. Hii inaonyesha Harmonize alifunga ndoa wakati Zuu ndio amezaliwa, pengine akiwa na umri wa kama miezi mitatu au minne hivi.

Kwa muktadha huo ni kwamba Harmonize alikuwa akimsaliti mchumba wake Sarah kwa wakati huo, huku mbele ya vyombo vya habari na mitandao akionyesha kumpenda na kumjali. Wakati Sarah akisubiria mahusiano yao yapande Ligi Kuu (ndoa) wacheze wote, kumbe Konde Boy anakipiga huko kwenye Ndondo hadi kupata medali na kuificha kwa Bibie maana itakuwa msala.


Imeandikwa na Peter Akaro