TUONGEE KISHKAJII: Siku ya Mondi inavyokuwa kutwa nzima

DIAMOND Platnumz ndiye msanii aliye bize kuliko wote Tanzania. Kwa mwaka anafanya shoo zaidi ya 730. Hiyo ni sawa na wastani wa shoo mbili kila siku. Wasanii wengine hawawezi huo mchakamchaka. Na hapo bado anatakiwa kufanya intavyuu, kuzitembelea familia zake ambazo zipo nchi tofauti, vikao vya kampuni anazomiliki, kuandika nyimbo, kuingia studio kurekodi, kusikiliza ngoma za Zuchu na Mbosso na kuamua zipi ziingie kwenye EP na zipi zitoke kama singo.

Leo nitakusimulia siku ambayo alirekodi wimbo wa Yataniua alioshirikishwa na Mbosso ilivyokuwa. Siku hiyo aliamka saa 4 asubuhi. Na kama kawaida kwanza hupiga tizi kwenye gym nyumbani na hufanya mazoezi huku anasikiliza muziki na mara nyingi husikiliza ngoma anazozipenda za Kinaijeria au amapiano, na anachofanyaga ni kwamba, wakati anapiga tizi huweka playlist yenye ngoma nyingi za aina hiyo. Lakini siku hiyo kuna ngoma moja ilipigwa ikambamba sana akaamua kuacha kusikiliza playlist nzima, badala yake akawa anarudia wimbo huohuo.

Basi akapiga mazoezi na wimbo mmoja mpaka alipomaliza. Akaenda kuoga na siku zote haogi bila muziki. Wakati anaoga akawa anasikiliza wimbo uleule. Alipomaliza akapiga zake msosi kisha akazama kabatini na kuchomoka na code za kutupia siku hiyo. Alipovaa akatoka mpaka parking akamkuta baunsa wake. Wakaingia kwenye Rolls Royce mpaka Wasafi Media huku njia nzima wakiwa wanasikiliza wimbo uleule.

Alipofika akapiga vikao viwili vitatu, mara akaja Baba Levo wakapiga stori kisha akaishia zake kwa S2keezy kwenda kurekodi wimbo na Mbosso ambao utakuwa kwenye EP ya Mbosso iliyotoka juzi inayoitwa Khan. Akiwa njiani alikuwa anasikiliza wimbo uleule.

Alipofika studio akakuta Mbosso a’shaingiza vocal. Diamond naye akaingiza vocal, akaimba hivi: “Na watakoma aisee, hili party nyama choma ajeee, ajeee. Muziki mangoma jeee, cha arusha nitakichomajee, ajeeee” Kabla hajamaliza kurekodi S2keezy akamwambia: “Braza Mondi umeimba verse kali kinyama sema nini? Hii melody kama naijua. Hii ni ngoma ya Asake wa Nigeria inaitwa Peace Be unto You. Tukiacha ngoma itoke hivi watu watasema umeiga.” Diamond akagutuka kwamba kweli maana wimbo ndio alioupenda alipokuwa gym na akausikiliza siku nzima. Basi akamwambia S2keezy: “Lakini Zombi, unajua Watanzania hawamjui Asake. Hawatajua kama tumeiba. Tuachie tu hivi hivi”. S2keezy akawa bado na wasiwasi. Basi Diamond akamwambia: “Hebu ngoja tumpigie mama dangote tumuulize kama anamjua Asake, akisema hamjui basi ujue Watanzania wote watakuwa hawamjui.” Diamond akampigia Mama Dangote, akamuuliza: “Unamjua Asake?”. Mama Dangote akasema hapana, simjui. Akamuuliza hadi Uncle Shamte ambaye alikuwa amekaa pembeni anakula. Uncle Shamte akasema pia hamjui.

Basi Diamond akamgeukia S2keezy akamwambia: “Mdogo wangu turekodi itasaidia kubusti EP.”

Basi wakamalizia kutengeneza wimbo kisha Diamond akarudi zake home kupumzika. Hiyo ikiwa ni saa 6 za usiku. Na hiyo ndiyo siku ya Mondi.