TUONGEE KISHKAJI: Wasanii wanahitaji mbinu za imani, vaibu na miujiza

NAPITA mtaani, naona nguzo moja ya umeme imejaa vipeperushi vya matangazo. Moja linasema MGANGA KUTOKA HANDENI, safisha nyota, dawa ya mvuto, heshima ya ndoa, kufaulu darasani, pete ya utajiri kisha chini kuna namba ya simu. Lingine linasema BLING BLING BAND! Mangoma hadi majogoo, ndani ya Golden Star Night Club. Ni tangazo la bendi hilo, hapo lina maandishi mekundu na picha za wasanii wote wa hiyo bendi, wako kama nane hivi. Kiingilio kinywaji.

Kisha kwa upande mwingine wa msitimu kuna kipeperushi ambacho kidogo kimechanikachanika, kinaonekana cha zamani kidogo na kinasomeka, Imani, Upendo na Miujiza.

Ninapokisoma nacheka, nakumbuka hili lilikikuwa tangazo la kongamano kubwa kuwahi kutangazwa Tanzania. Nasema kuwahi kutangazwa kwa sababu sijui hata kama lilifanyika au laa, lakini ninachofahamu ni kwamba, hakuna mkazi wa Dar es Salaam ambaye alikuwa hajui kuhusiana na hiyo mbanga.

Nakumbuka lilikuwa ni tamasha lililofanyiwa matangazo ya kishindo. Vilimwaga vipeperushi kibao, vingi sana, kiasi kwamba ilikuwa kila unapopita Dar lazima uvione, na sio kuviona tu, lazima uvione kwa fujo.

Yaani ilikuwa ukipita kwenye kituo cha basi, unakuta kituo kizima kimejaa makaratasi ya njano yenye maneno matatu Imani, Upendo na Miujiza. Na ninaposema kituo kizima namaanisha kwamba ni kituo kizima.

Daladala zikipita ni Imani, upendo na miujiza, kuta zote mitaani Dar es Salaam zilikuwa zinasema Imani, upendo na miujiza. Usipokuwa makini ilikuwa unaweza ukaingia gheto kwako ukakuta kitanda kimebandikwa vipeperushi vya amani, upendo na miujiza.

Ukiniuliza mimi, nitakwambia washkaji waliofanya promo ya lile tukio ni maprofesa wa kujitangaza. Wale washkaji wana uwezo wa wakakufanya mwanaume ujue bei ya lipstick, ujue zinauzwa wapi wakati wewe huzitumii wala sio mfanyabiashara wa kuuuza lipstick.

Na ukinuliza maoni yangu kuhusu wale washikaji nitakwambia wale ni watu wabaya pengine kila lebo ya muziki hapa nchini, kila kampuni ya filamu hapa Tanzania na kila msanii anastahili kuwa na timu na bajeti inayoweza kufanya matangazo ya fujo namna ile.

Wenzetu waliotupiga ‘gepu’ kwenye kwenye hii tasnia ya sanaa na burudani sio kwamba wao wanaimba sana kuliko sisi, sio kwamba wao wanaigiza sana kuliko sisi, wao wamejua kujitangaza tu.

Mabango kila unapopita, ukiingia Youtube kabla hujatazama wimbo wa Marioo, kwanza linapigwa tangazo la wimbo wa Davido. Hiyo ndo kasi na kelele ambazo wasanii wetu wanatakiwa kuzifanya.

Tunajua ni gharama, tunajua sio kila mtu anaweza lakini mwisho wa siku kutafuta sababu ya kushindwa hakukusaidii kwenye ulimwengu wa mashindano ya kibiashara.