TUONGEE KISHKAJI: Vipi, tumpe Lamata mabegi ya Kanumba?

TUONGEE KISHKAJI: Vipi, tumpe Lamata mabegi ya Kanumba?

KWENYE tasnia ya filamu Tanzania tunayoiita Bongo Movie hakuna mtu aliyewahi kuonyesha njaa ya kutoboa kumzidi Kanumba. Ukikaa, ukiwaza ndio unajua pengine ndiyo maana mshikaji alizikwa na mamilioni ya Watanzania pale alipofariki dunia miaka 10 iliyopita.

Na tukisema hivi hatumaanishi tunawavunjia heshima wasanii wengine, hapana. Tunaheshimu walichofanya na mchango wao kwenye tasnia, lakini tukisema ukweli tu - yule mshikaji alikuwa na njaa ya kutoboa.

Ukiangalia hatua zake utaona. Jinsi alivyoanza kama mwigizaji mdogo wa tamthilia katika kundi la Kaole akaanza kupata nafasi kubwa. Mara akajitosa kwenye filamu akaanza kufanya na watu kisha baadaye akaanzisha kampuni yake mwenyewe na kuwa anatengeneza filamu zake. Filamu zake za mwanzo zilikuwa za kuungaunga sana wakati mwingine picha, sauti na stori mbaya, lakini kila siku alikuwa anaboresha.

Alipoona amesimama kwenye soko la ndani akaanza kuangalia nafasi za nje ya Tanzania. Akakimbilia Nigeria na Ghana ambapo filamu zao kwa kipindi hicho zilikuwa zinasumbua sana Bongo. Kanumba akaenda huko na kuanza kupiga kazi na mastaa wa huko japo kazi za kiwango cha chini cha ubora lakini tayari zilikuwa zina wasanii wenye majina maku-bwa ndani yake na zikampaisha zaidi.

Baadaye akagundua sasa anawamudu mastaa wa Nigeria. Kilichobaki ni kitu kimoja tu, kushirikiana nao kwenye kazi kubwa. Hapo ndipo akaja kutengeneza Bongo Movie yenye kiwango kuliko bongo movie yote kwa kipindi kile, Devil Kingdom. Na humo ndani akamshirikisha staa mkubwa kutoka Afrika Magharibi, Ramsey Nouah. Yale yalikuwa ni mapinduzi ya Bongo Movie, lakini kwa bahati mbaya kabla hajatuonyesha jambo lingine kubwa Mungu akamchukua.

Tangu Kanumba afariki duni kumekuwa na watengenezaji filamu wengi wakifanya kazi zao chini ya kivuli cha Kanumba. Wengine mpaka wamejiita Kanumba wa pili, Kanumba mdogo na kadhalika lakini kiukweli hawakuwa wakitosha kwenye hilo jina. Wengi walikuwa wanaonekana ni watengeneza filamu tu sio watengeneza filamu wenye njaa ya kutoboa kama alivyokuwa Kanumba.

Lakini kwa sasa naamini tumepata mtu wa kumpa mabegi ya Kanumba asaidie kuyalepeka yalipokuwa yanakwenda. Mabegi ya kuivusha Bongo Movie kwenda kwenye mipaka mingine. Mabegi ya kuifanya Bongo Movie isiwe ni filamu za bajeti ndogondogo tu na za kuungaunga.

Leah Mwendamseke a.k.a Lamata, dairekta wa tamthilia inayobamba kwa sasa ya Jua Kali. Huyu Bi mkubwa ni mtu m’bad sana. Bi mkubwa ana njaa ya kutoboa sio poa. Bi mkubwa inaonekana hapendi vitu rahisi hata kidogo.

Wakati wenzake wanatengeneza tamthilia za kawaida tu kama tulivyozoea yeye anasema hapana “mimi nitatengeneza tamthilia kwa kishindo”. Kwenye tamthilia yake amekwenda kushuti Kenya, amekwenda Nigeria, na sasa yuko nchini Afrika Kusini. Na kote huko alikokwenda ameshuti na wasanii wakubwa kwenye hayo mataifa. Ameshuti na Van Vicker, Patience Ozokwor, Sho Madjozi na zaidi.

Unaweza ukachukulia poa hizo jitihada, lakini amini kwamba Bi mkubwa ana ndoto moja kubwa ya kutengeneza mashabiki Afrika nzima. Na kuwa na ndoto kama hiyo kunahitaji mawazo makubwa na uthubutu wa kufanya mavituzi kama aliyokuwa nayo Kanumba. Kongole kwako Lamata!