TID awapa tano Basata ukaguzi wa nyimbo

Msanii aliyewahi kutesa na kibao cha Zeze, Khalid Mohamed ’TID’ amewapa tano Baraza la Sanaa la Taifa(Basata) kwa maamuzi yake ya kukagua nyimbo kabla hazijakwenda kwa walaji.

Ukaguzi wa kazi za muziki utekeezaji wake umeanza rasmi Mei 1 mwaka huu ikiwa ni katika kukazia kusimamia Sheria namba 23 ya mwaka 1984 ya Baraza la Sanaa la Taifa pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2019 na kanuni zake za mwaka 2018,

TID anakuwa mmoja wa wasanii wachahe maarufu ambao wanaunga uamuzi huo mkono, baada ya siku mbili hizi kuibuka mjadala na mvutano wa suala hilo huku wengi wakionekana kuuponda.

Ni kutokana hayo tayari serikali imeingilia kati ambapo kesho ina mpango wa kuwakutanisha Basata na Wasanii kuweza kulizungumzia hilo.

Hata hivyo TID yeye katika ukurasa wake kwenye mtandao wa Instagram kuhusu jambo hilo, ameandika”Hapa kuna tatizo kila mtu ana chuki yake na Basata kwa kuwa hawafanyi kazi yao.......

“Kwa kifupi hawasaidii chochote sisi ambao ndio tumeufikisha huu mziki hapa na kwa ujumla sanaa nzima ya Bongofleva lakini kwenye muziki ambayo kimaadili haitakiwi kutangaza  uchafu kuhariri  naona hapo wameanza kufanya kazi labda hawajatoa ufafanuzi wa jinsi gani wataweza kumudu kwa ukubwa,wakilinyoosha hilo naona sasa ndo wakati wa kuyazungumzia mengine.

“Mbali ya hayo wasanii mlikuwa wapi siku zote wengine tunapiga kelele kila kukicha hadi tunajiita Basata tunataka kuchukua maamuzi mikononi?

“Kwenye hili humu naona kuna utashi sababu nani kasema hivi mnafata mkumbo wakati wenye mashairi yenye matusi wenyewe hawajaongea chochote.Basata fanya kazi umeanza vizuri,”ameandika TID.

Hatua hiyo ya Basata mbali na kuungwa mkono na TID,  pia mwimbaji taarabu Mzee Yusufu, ambaye alieleza kwa ufupi kuwa watu wanapaswa kuhoji kwa nini kelele ya kulipinga hilo Zinatoka zaidi kwa wasanii wa Bongofleva na kubainisha kuwa wao ndio waimbaji wakubwa wa nyimbo za matusi.

Mzee Yusufu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Waiambaji taarabu nchini, amesema atayasema mengi zaidi kesho katika kikao chao na Basata na viongozi wa serikali.