Tanasha avunja ukimya, nililala hotelini

Monday February 01 2021
tanasha pic
By Nasra Abdallah

Moja ya maswali ambayo watu walikuwa wanajiuliza kuwa mzazi mwenza wa msanii Diamond Platnumz alivyokuja nchini Tanzania ni, alilala wapi?
Tanasha na Diamond walibwagana Machi mwaka jana, ambapo dada huyo waliyebahatika kuzaa mtoto mmoja na msanii huyo aliamua kurudi kwao nchini Kenya.
Hata hivyo mwenyewe ameamua kuvunja ukimya huo, baada ya jana kuzungumza na vyombo vya habari, alipokuwa uwanja wa ndege.
Ikumbukwe miezi miwili iliyopita mzazi mwingine wa Diamond, Zarina Hassan maarufu kwa jina la Zari, kutua nchini na watoto wake ambapo alionekana akijivinjari nao katika jumba hilo la kifahari la msanii huyo lililopo maeneo ya Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
Kati ya maswali aliyoulizwa ni pamoja na je alilala wapi ukizingatia kwamba alikuwa akionekana nyumbani kwa Diamond hadi nyakati za usiku.
Akijibu swali hilo,mrembo huyo kutoka pande za Kenya,alisema alilala hotelini japo mara kwa mara alikuwa anaenda nyumbani kwa Diamond kwa kuwa mtoto wake alikuwa huko na baba yake.
“Nilikuwa ni mtu wa kwenda Mbezi Beach kwa baba watoto wangu na kurudi hotelini kwa kuwa mtoto wangu alikuwa mara nyingi yupo na familia upande wa baba yake,”amebainisha Tanasha.
Wakati kuhusu tetesi za kurudiana na mkali huyo wa kibao cha Waah!, Tanasha amesema hakuna kitu kama hicho.
Hii ni kutokana na namna walikvyonekana kuwa na ukaribu siku ya ‘After Party ya Tumewasha Tour’ pale ukumbi wa Element maeneo ya Masaki.
Katika hili Tanasha alisema kwanza hakutegemea siku hiyo kama angeitwa na Diamond kupanda jukwaani, ilikuwa ni jambo la ghafla sana kwake, na wakati anamgeukia kumuuliza kwa nini amefanya hivyo, ndipo hapo wapiga picha walivyotafsiri kila mtu kivyake ikiwemo hilo la kurudiana.
“Mimi nipo single kwa sasa, suala la kurudiana na Diamond halina ukweli wowote, hata ile siku ya party wala sikutegemea kupanda jukwaani lakini ndio yakatokea yaliyotokea.
“Pia mimi sio mtu wa kuonyesha namna ninavyopendana na mpenzi wangu mbele ya kamera kila mtu aone kama nataka kufanya hivyo nitafanya nikiwa naye peke yangu,”amesema Tanasha.

Advertisement