Rayvany ahojiwa polisi kwa saa sita

Msanii Raymond Mwakyusa maarufu kwa jina la Rayvanny amehojiwa katika kituo polisi kanda maalum Dar es Salaam  kwa saa sita leo Alhamisi Aprili 15, 2021.

Chanzo cha kuaminika kutoka kituoni hapo kilisema Rayvanny alifika kituoni hapo saa tatu asubuhi na kuwa katika mahojiano na maofisa upelelezi.

Mwananchi iliyokuwa imeweka kambi nje ya kituo hicho ikisubiri kujua nini kinaendelea, ilimshuhudia msanii huyo akitoka kituoni hapo saa 9:30 alasiri.

Rayvanny aliyekuwa amevalia shati la drafti ya rangi bluu na nyeusi na suruali nyeusi alitoka ndani ya kituo hicho akiwa na wanaume wawili.

Alipomaliza kushuka ngazi za kituoni hapo walinzi wake waliokuwa wakimsubiri kwa nje walimfuta na kuongozana nao hadi kwenye gari ya rangi nyeusi  aina yaTX Prado lililokuwa limeegeshwa nje ya geti la kituo hicho.

Hata hivyo sio yeye wala watu aliokuwa nao, hakuzungumza chochote na waandishi waliokuwepo eneo hilo.

Katika hatua nyingine hatua chache toka kwenye geti hilo,alikuta wanafunzi wakimshangalia na kufuata gari lake barabarani  hali iliyomlazimu kufungua vioo na kuanza kusalimiana naye kwa muda wa dakika tatu  kabla hajaondoka eneo hilo.