Queen Mugesi kuiwakilisha Tanzania, Miss East Africa 2021

Tuesday November 16 2021
miss pic
By Herieth Makwetta

Dar es Salaam. Maandalizi ya mashindano ya kimataifa ya urembo ya Miss East Africa 2021 yako katika hatua za mwisho ambapo mrembo Queen Mugesi ataiwakilisha Tanzania katika kilele kitakachofanyika Desemba 17, 2021 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Queen ambaye aliwashinda warembo zaidi ya 2,600 wa Tanzania walioomba kuiwakilisha nchi kwa njia ya mtandao, alichaguliwa katika mchakato ulioendeshwa na wataalamu wa mambo ya urembo kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Akizungumza leo Novemba 16, 2021 Makamu wa Rais wa mashindano hayo, Jolly Mutesi alisema tayari nchi zinazoshiriki katika mashindano hayo zimeshatuma wawakilishi wake na washiriki hao kwa sasa wapo katika maandalizi ya mashindano hayo makubwa katika ukanda huu wa Afrika.

Amesema nchi zilizokwisha tangaza wawakilishi wake ni pamoja na Kenya, Uganda, Rwanda, South Sudan na Somalia huku zingine ni Reunion, Ethiopia, Malawi, Burundi na Mauritius.

“Tanzania itawakilishwa na mrembo Queen Mugesi ambaye aliwashinda warembo zaidi ya 2,600 wa Tanzania walioomba kuiwakilisha nchi kwa njia ya mtandao,” amesema Mutesi na kuongeza;

“Warembo wanaoshiriki katika mashindano hayo wanatarajiwa kuanza kuwasili Novemba 26, 2021 na fainali ya mashindano hayo itafanyika tarehe Desemba 17, 2021 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam kuanzia saa 12 jioni.”

Advertisement

Amesema, mashindano ya Miss East Africa ambayo yaliasisiwa na Mtanzania Rena Callist mwaka 1996, yanasubiriwa kwa hamu kubwa na wapenzi wa mambo ya urembo na yanatarajiwa kuangaliwa na zaidi ya watu milioni 200 moja kwa moja LIVE kupitia katika TV na wengine wengi zaidi wataangalia kupitia mtandao duniani kote.

Amesema Mashindano ya Miss East Africa yanaandaliwa na kampuni ya Rena Events LTD ya jijini Dar es salaam.

Advertisement