Ommy Dimpoz kwenda Macca, Sheikh Alhad atia neno

SIKU moja baada ya msanii Ommy Dimpoz kuonekana akiwa Macca , Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum, ametia neno katika safari hiyo ya ibada kwa msanii huyo.

Ommy ambaye jina lake halisi ni Omar Nyembo, jana Jumapili Mei 9, 2021, alitupia picha kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram akionekana yupo eneo hilo takatifu la Macca ambapo watu huenda kuhiji.

Katika maelezo yake aliyoambatanisha na picha aliyovaa mashuka meupe, ambayo wanaume huyatumia wanapofika eneo hilo, ameandika;

".......Alhamdulilah. Mwaka Juzi nilitamani kuwa Mahali hapa kwaajili ya ibada takatifu ya Umrah lakini kwa mapenzi yake Mwenyezi Mungu haikuwezekana nikaishia kulazwa tena kitandani.

"Lakini sikufa moyo kwani Mwenyezi Mungu yeye ndiye mpangaji wa kila jambo na anapokupa mitihani basi jua ni kipimo cha imani yako kwake.

“Sina Mengi zaidi ya Kujiombea Dua na Kuwaombea Watu wote Allah atujaalie kila jema tunalomuomba, atupe afya na Uzima, atuondolee dhiki atupe na faraja, atuzidishie ridhiki, atusamehe madhambi yetu, apokee funga zetu, atuzidishie upendo miongoni mwetu Inshaallaah.”

Akifafanua alichokifanya Ommy, Sheikh Alhad amesema kbada aliyoenda kuifanya kipindi hiki msanii huyo haina tofauti sana na ile ya hija kwa masharti na thawabu zake.

"Hija na Umrah zote ni ibada za kwenda kujitakatisha kwa Mola, ambapo Hija hufanyika kabla ya sikukuu ya Idd El Haji, wakati ibada ya Umrah hufanyika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Hata hivyo, amesema mara baada ya kurejea hatarajii kumuona msanii huyo akionekana tena kwenye mambo ya muziki na badala yake ajikite zaidi katika kumtumikia Mwenyezi Mungu.

Alipoulizwa mbona wasanii wengine walishawahi kwenda na waliporudi waliendelea na kazi zao za sanaa; Katika hilo Sheikh Alhad amesema hiyo inaonekana wazi kwamba hija zao hazikupokewa.

Ommy Dimpoz anakuwa msanii wa tatu kwenda Macca, akitanguliwa marehemu King Majuto na mwimbaji muziki wa taarabu, Mzee Yusufu ambao wote hawa baadaye walirejea kwenye kazi zao za sanaa.