Nyuma ya pazia afya ya Celine Dion

Muktasari:

  • Mwimbaji kutoka Canada, Celine Dion ambaye hivi karibuni alitimiza miaka 54 amekuwa midomoni mwa mashabiki wakihoji nini sababu ya afya yake kuzorota. Dada yake, Claudette akizungumza na Jarida la Ufaransa, Voici, alisema kinachotokea kwa Celine kinasikitisha na kushangaza.

Mwimbaji kutoka Canada, Celine Dion ambaye hivi karibuni alitimiza miaka 54 amekuwa midomoni mwa mashabiki wakihoji nini sababu ya afya yake kuzorota. Dada yake, Claudette akizungumza na Jarida la Ufaransa, Voici, alisema kinachotokea kwa Celine kinasikitisha na kushangaza.

Celine aliolewa Desemba 17, 1994 na Rene Angelil ambaye pia alikuwa meneja wake, katika ndoa yao walijaliwa kupata watoto watatu ambao wote walipatikana kwa njia ya upandikizaji ijulikanao kama In Vitro Fertilization (IVF).

IVF ni utaratibu wa kutoa mayai kwenye ovari ya mwanamke na kukutanishwa na mbegu za kiume nje ya mwili ili kuunda kiini tete ambacho hukuzwa kwenye maabara kwa muda fulani na kuja kuwekwa kwenye mfuko wa uzazi wa mwanamke.

Kutokana na tatizo la uzazi kwa Celine walilazimika kufanya hivyo mara kadhaa na kujaliwa mtoto wao wa kwanza, Charles Januari 25, 2001. Mei 2010 alitangaza ana ujauzito wa wiki 14 wa watoto pacha baada ya majaribio sita ya IVF. Oktoba 23, 2010 alijifungua pacha hao kwa upasuaji na kuwapa majina ya Eddy na Nelson.

Januari 14, 2016 mumewe, Angelil alifariki kwa saratani ya koo wakati pacha wao wakiwa na miaka sita, mazishi yake yalifanyika katika kanisa la Notre-Dame Basilica.

Ni kama nyota huyo wa muziki wa muda wote alikuwa akiandamwa na jinamizi, kwani siku mbili baada ya kifo cha mumewe, kaka yake, Daniel naye alifariki kwa saratani akiwa na umri wa miaka 59.

Vifo vya kufuatana, kulea watoto peke yake bila mumewe vinatajwa miongoni mwa mambo yaliyozorotesha afya yake, lakini kikubwa zaidi Celine anasumbuliwa na tatizo la kukaza kwa misuli, kitaalamu linaitwa (muscle spasms) ambalo limemfanya kuonekana kama mzee sana ghafla au mtu aliyesumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu.

Hata hivyo, kwa mujibu wa mtaalamu wa mazoezi ya kupunguza uzito wa mwili na afya ya wanawake wa nchini Italia aliyetoa maoni baada ya mahojiano ya Celin Dione na ‘voici’, Dk Guiseppe Aragona kufanya mazoezi kupita kiasi (over-exercising) kunaweza kusababisha tatizo la kukaza misuli endapo mhusika hajinyooshi vya kutosha kabla na baada ya aina yoyote ya mazoezi ya mwili.

“Kwa kuwa Celine ni mwigizaji, labda anafanya mazoezi mara kwa mara, hivyo kuna uwezekano mkubwa kwamba mtindo wake wa maisha ndio unaosababisha hilo, anaweza kuwa anasumbuliwa na uchovu wa misuli,” alisema Dk Aragona.

Dada yake Celine, Claudette katika mahojiano na Shirika la habari ABC la Canada alisema linapokuja suala la misuli ya Celine, anajua alilazimika kufanya aina ya mazoezi ili kuwa sawa kila siku na anaamini kuna kipindi mwili wake utazoea.

Kwa upande wa daktari wa misuli wa timu ya Yanga, Dk Jacob Sospeter Onyango anasema kuwa inawezekana kabisa aina ya mazoezi anayofanya mhusika yakasababisha kukaza kwa misuli.

Anasema licha ya mazoezi kuwa na taratibu zake za ufanyaji, ikiwamo uanze na nini na umalize na nini, pia kuna muda. Hivyo ukifanya mfululizo ni rahisi kuhatarisha afya au kukaza misuli ya mwili.

Anasema kukimbilia kufanya mazoezi mazito bila kuuandaa mwili siyo tu unasababisha misuli kukakamaa, bali pia unaweza kupata maradhi ya kiharusi.

“Kabla ya kuanza mazoezi lazima uuandae mwili, ukianza moja kwa moja mazoezi magumu ina maana unafungulia moyo kusukuma damu kwa wingi, lakini mishipa inakuwa haijafunguka hivyo madhara ni makubwa inaweza hata mishipa ya damu ikachanika. Ndiyo maana kuna wachezaji wanachanika nyama za mapaja,” anasema Dk Onyango.

Anasema moyo unaposukuma damu inatakiwa ifike hadi katika ncha ya miguu, kisha irudi inayostahili, lakini inapokwama mahali hurudi nyingi na kuupa shida moyo ambayo madhara yake ndiyo hayo misuli kukakamaa au kupata kiharusi.

Anasema mara nyingi anashauri kama kuna mtaalamu anasimamia mazoezi ni vema akaanza kwa kuchua misuli ya miguu kuanzia juu mpaka chini na kufanya mazoezi ya kujinyoosha nyoosha kisha kuendelea na mazoezi mengine.

“Wengi hawalijui hili, kukimbilia kufanya mazoezi magumu kama kukimbia, kuendesha baiskeli, kuinua vyuma, kuruka kamba bila kuuandaa mwili ni hatari kwa afya ya misuli na mwili kwa ujumla,” anasema.

Dk Onyango ambaye pia ni mshauri wa mazoezi anasema: “Nashauri hata uvaaji wa soksi tuuangalie, aina nyingine zinakuwa na mipira migumu ambayo inabana misuli ya miguu hivyo inazuia damu, inawezekana usiyaone matatizo mara moja, lakini baadaye inakuwa shida.

Mbali na hilo, hata ufungaji wa kamba za viatu unachangia madhara ya misuli. Kuna wanaozifunga nyuma kwenye tendoni, kuna uwezekano mkubwa kuugua kisigino au kiuno kwa sababu mawasiliano yanatoka juu.

Akilielezea hilo, Dk Ahmed El Muntasar aliyebobea katika masuala ya urembo, hususani mwonekano wa mwili, ambaye hutoa elimu kupitia ukurasa wa Instagram (@theaestheticsdoctor), anasema kiwango kikubwa cha msongo wa mawazo kinaweza kusababisha misuli kukaza kutokana na kuzalishwa kwa wingi homoni ya cortisol kutoka kwenye tezi za adrenal.

Celine, ambaye anasumbuliwa pia na tatizo la upotevu wa sauti, amekuwa akiahirisha matamasha yake mengi, Januari 15 kupitia tovuti yake alitangaza kusogeza mbele ziara yake ya kimuziki aliyopanga kuanza Amerika Kaskazini.

Shoo 16 zilisitiswa, alisema alikuwa na matumaini ya afya yake kuimarika na kujumuika na mashabiki wake, lakini analazimika kuwa mvumilivu na kufuata kile anachoshauriwa na madaktari wake.

Aprili, 2022 Celine alihamia kwenye jumba lake lenye thamani ya Dola1.2 milioni huko Nevada, Las Vegas, anapumzika huko na watoto wake watatu baada ya kuaihirisha shoo zake nyingi.

Celine anamiliki nyumba nyingi, lakini alipouza jumba lake la kifahari huko Florida kwa Dola45 milioni kulizua uvumi kwamba atakuwa akiishi Las Vegas kwa wakati wote kutokana na afya yake.

Kumpoteza mume wake, kaka yake, kukaza kwa misuli, upotevu wa sauti na kulea watoto mwenyewe vinatajwa kumpa sana msongo wa mawazo kiasi cha kuhatarisha afya yake, ingawa mwenyewe hapendi kuweka wazi hilo.

Akizungumza na gazeti hili, Dk Joachim Mabula kutokea Barrow Neurological anasema msongo wa mawazo una nafasi kubwa ya kudhoofisha hali ya mtu kiafya, lakini ni vigumu kusema ndio unapelekea kukaza kwa misuli.

“Msongo wa mawazo unaathiri afya kiujumla, ina maana furaha yake na uwezo wa mtu kujumuika na watu wengine, kwa hiyo itaathiri pia ratiba ya kula, lakini sio kwamba moja kwa moja inasababisha kukaza misuli,” anasema.

Mwaka 2019 Celine akizunguza na ABC News alisema: “Ni kweli mimi ni mwembamba kidogo, kila kitu kipo sawa, hakuna kitu kipya, ninafanya hivi kwa ajili yangu, nataka kujisikia mwenye nguvu na mwanamke mrembo zaidi,” alisema Celine.


Mfahamu Celine Dion

Huyu ni mwimbaji wa Pop, Rock, R&B, Gospel na Classical Music, alizaliwa Machi 30, 1968 huko Charlemagne, Quebec nchini Canada, akiwa mtoto wa mwisho katika famili ya watoto 14.

Celine akiwa na miaka 12 alikutana na Rene Angelil ambaye alivutiwa na kipaji chake na kuanza kumsimamia hadi kuachia albamu yake ya kwanza, ‘La voix du bon Dieu’ mwaka 1981. Alipofikisha miaka 19 wakachumbiana, kufikia mwaka 1994 wakati Celine akiwa na miaka 25 wakafunga ndoa.

Ametoa albamu tisa za Kirafansa na anashikilia rekodi ya msanii wa Kifaransa aliyeuza zaidi wakati wote, baada ya kujifunza Kiingereza, alijiunga na Epic Records nchini Marekani mwaka 1990, alitoa albamu yake ya kwanza ya lugha ya Kiingereza, ‘Unison’ iliyompa mafanikio makubwa hadi kushinda tuzo ya Grammy.

Nyimbo zake tangu wakati huo zimekuwa za Kiingereza na Kifaransa, ingawa pia ameimba Kihispania, Kiitaliano, Kijerumani, Kilatini, Kijapani na Kichina.

Baada ya kuachia albamu zake ‘Falling into You’ (1996) na ‘Let’s Talk About Love’ (1997) zilizouza nakala zaidi milioni 30 Marekani, alipata umaarufu mkubwa duniani huku akitikisa na nyimbo kama ‘The Power of Love’, ‘Think Twice’, ‘Because You Loved Me’, ‘It’s All Coming Back to Me Now’, ‘My Heart Will Go On’ na ‘I’m Your Angel’.

Celine aliendelea kutoa albamu za Kifaransa kama ‘D’eux’ (1995) ambayo inashikilia rekodi ya kuuza zaidi wakati wote, huku albamu nyingine kama ‘S’il suffisait d’aimer’ (1998), ‘Sans attendre’ (2012) na ‘Encore un soir’ (2016) zikifikia rekodi nzuri ya mauzo.

Anatambulika miongoni mwa wasanii waliouza sana duniani akiwa ameuza rekodi zaidi ya milioni 200, anachukuliwa kuwa mmoja wa waimbaji wa Pop waliofanikiwa zaidi. Ameshinda tuzo tano za Grammy, ametunukiwa shahada mbili za heshima za udaktari wa muziki kutoka Chuo cha Muziki cha Berklee na Université Laval.

Mnamo 2008, Celine alitambuliwa kama msanii wa kimataifa aliyeuza zaidi nchini Afrika Kusini, kufikia mwisho mwa 2009, Celine alitambuliwa na Los Angeles Times kama msanii aliyeingiza fedha nyingi zaidi kwa muongo huo, kikiwa ni kitita cha Dola748 milioni, wastani wa Sh1.7 trilioni.

Celine ambaye anakadiriwa na Jarida la Forbes kuwa utajiri wake ni Dola470, wastani wa Sh1.09 trilioni, mwaka 2008 yeye na mumewe, Rene walitumia Dola7 milioni kununua jumba la kifahari kwenye kisiwa cha Jupiter huko Florida Kusini, Marekani.

Agosti 2013 alitaka kuuza eneo lake la ekari 6 kwa Dola72.5 milioni, lakini hakupata mnunuzi hata baada ya kupunguza bei hadi Dola65 milioni, kisha Dola45 milioni, lilikuja kupata mnunuzi Aprili 2017 kwa Dola38.5 milioni. Mwaka 2016 Celine aliuza kisiwa chake chenye ukubwa wa ekari 20 nje ya Quebec kwa Dola25 milioni.