Ndani ya boksi: Toka Bishanga, Kanumba mpaka Gabo...

Muktasari:

  • Jumatatu nipo zangu Dodoma mjini. Nahaha kusaka usafiri wa kurudi Dar. Nilitaka kuhesabiwa nikiwa kitaani kwangu. Yes! Nipo stendi ya mabasi ya Shabiby, sauti za totozi za Kigogo zikiita abiria wanunue zabibu.

Jumatatu nipo zangu Dodoma mjini. Nahaha kusaka usafiri wa kurudi Dar. Nilitaka kuhesabiwa nikiwa kitaani kwangu. Yes! Nipo stendi ya mabasi ya Shabiby, sauti za totozi za Kigogo zikiita abiria wanunue zabibu.

Nakumbuka pisi ya Sinzani, iliomba nirudi na zabibu. ‘Sinaga’ ubwege wa kubeba vitu safarini, hata nguo mara chache sana. Mie ni simu na chaji tu ndio vitu vya muhimu. Ni utaratibu wangu tangu na tangu.

Nalazimika kuvunja utaratibu wangu huu kwa sababu ya aina ya kiumbe aliyeagiza. Ni pisi ambayo ikiomba figo, naipa na ini. Usinione mi bwege ukisoma hapa, ukimuona huyo Shani wangu. Utashangaa!

Ni mrembo sana mpaka urembo nao unamshangaa jinsi alivyo mrembo sana. Mimi nani? Wazazi wenyewe akiwepo mama yake, hushangaa jinsi alivyoumbika. Hawaamini! Utotoni walitaka kumsusa wakidhani jini.

Nagundua sina mkwanja wa kutosha mkononi. Upo kwa simu. Naangaza kusaka chimbo la miamala ya pesa. Naelekezwa na dada muuza zabibu, sehemu nikatoe pesa. Namshukuru huku nachapa lapa.

Bandani mhudumu wa kike. Nauliza kiasi ninachotaka kutoa jibu ni “Toa”. Fasta natoa! Wakati nasubiri ujumbe ufike ili anipe changu. Nautumia huo muda kudadisi urembo wa mhudumu yule. Aiseeee!

Najiuliza nibebe zabibu nipeleke kwa Shani, au nimbebe mhudumu nirudi naye Dar? Kuna majaribu hatarishi na majaribu tatanishi. Hili ni jaribu lenye vyote, yaani tatanishi na hatarishi. Ni hatari sana kwa afya ya akili.

Maji ya kunde, lipsi pana, meno safi yamepangika kama kwenye tangazo. Huijui theluji ya Mlima Kilimanjaro? Basi tazama macho ya huyu mtoto. Meupe pee, siyo kama Ray C ila yana ukubwa wake. Nyiiiie!

Nakamkumbuka Siti Binti Kasri katika mchezo wa runinga wa Tausi.

Nikawakumbuka Aisha na Lilly wa Mambo Hayo. Kuna Kissa wa Kaole naye akaja akilini. Vuta picha ya Nora yule wa Kaole, ndio rangi ya dada huyu muhudumu.

Waigizaji wa zamani hawakuhitaji kiki ili wabambe. Hawakubadili ngozi wala wanaume ili wapate umaarufu. Walifanya kazi ya uhakika iliyovuta hisia za mamilioni ya watazamaji. Hii leo wengi feki, hawaishi maisha halisi wana ‘feki’ sana. Hiki ndicho kiliwaponza mpaka kwenye soko lao la filamu. Kuuaminisha umma kuwa ni matawi ya juu na wana pesa nyingi wakati ndivyo sivyo.

Hili ni kosa kubwa kwa sanaa yao. Ingawa wengi hawajui na hawajui. Unaweza kujikweza ikiwa ni kweli. Ukijikweza unafanya watu wakupandishe bila kukushikilia mwisho unaanguka.

Ugonjwa wa kujikweza una undugu na wasanii. Mfano mfumo wa kodi za TRA ni chanzo cha mauti ya soko lenyewe. Kwa sababu soko halikuwa kubwa kama ilivyonekana kwa watu kutokana na majigambo ya wasanii wenyewe.

Msanii anajitapa kuwa ana nyumba ya milioni mia nne. Na chanzo chake cha kipato akisema ni filamu pekee. Unategemea watu walionaje soko la filamu? Huwezi kuwalaumu TRA kwa mfumo huo mpya wa kodi.

Waliambiwa uongo, taarifa hazikuwa sahihi, hata wasanii hawana hizo taarifa. Taarifa sahihi zilikuwa zipo kwa msambazaji na familia yake. Ndio wamiliki wa filamu zote, wasanii ni waajiriwa kama wengine.

Hawakuwa wazi wasanii wote. Ndio maana hakuna msanii anayemiliki filamu yake. Hadi leo hii mifupa yake ikiwa pale Kinondoni, Steven Kanumba hakuna taarifa za kuwahi kumiliki filamu. Amekwenda na kila kitu chake na kubaki jina tu.

‘JB’, ana filamu moja anayoimiliki. Ray na Johari wana moja tu. Nyingine ni haki ya wasambazaji. Biashara ya filamu ilianza kuchanua, huu mfumo mpya wa kodi ulifanya wasambazaji watoweke.

‘Ishu’ ni utozaji kodi kwa stika. Msanii analipia kodi kwa nakala elfu tano, na siyo chini ya hapo, kabla hajaiingiza filamu sokoni. Bila kujua soko likoje. Kama wateja ni elfu mbili au elfu moja tu. Atajua mwenyewe.

Mfumo huo ukafanya wasambazaji wasite kuingiza filamu nyingi sokoni. Kwa sababu hawakujua mwenendo wa biashara utakuwaje. Na malipo kwa wasanii yakaporomoka ghafla ‘automatikale’.

Kuporomoka kwa malipo kukazalisha kazi za kanjanja. Wakibeba wasanii wasio na uwezo, na wenye uwezo wakichezeshwa sehemu ndogo kwa malipo kidogo. Ili picha zao tu ndio zitumike kwenye kasha na kuingiza sokoni.

Wakatumia nguvu nyingi kwenye makasha ya uongo ili wauze na kukwepa gharama kubwa. Watu nao utawadanganya mara moja siyo kila siku. Uhuni huu ukachokwa machoni kwa wateja wa filamu na kujikita kwa Wakorea.

Filamu zinapitia mabadiliko ya soko kuendana na wakati. Marekani na Ulaya walibadilika kitambo. Hawapo kwenye hizo CD & DVD, wapo kwenye majumba ya sinema na mitandaoni (online). Sisi hatukujiandaa kibiashara baada ya CD & DVD kutoweka.

Tasnia ilikuwa changa. Mabadiliko kwa wenzetu yalikuwa maili nyingi mbele yetu. Hatuna wawekezaji wa mitaji mikubwa, ufahamu wa soko na kufanya mabadiliko. Matokeo yake biashara ikadoda na kuporomoka kabisa.

Mfumo wa kodi hawakupanga TRA peke yao. Wadau ambao ni wasanii wenyewe walihusika. Ili waonekane wako vizuri kipesa walishindwa kuwa wakweli. Wakaiaminisha TRA kuwa soko la filamu ni kubwa.

Wasanii waliamini uwepo wa stika kwenye makasha utaua biashara haramu. La idadi ya nakala za kulipia kodi kabla wakalipuuza. Kwa nini hizo nakala elfu tano lazima zilipiwe kodi kabla ya kuingia sokoni?

Ni hivi. Stika hutengenezwa Ulaya kwa gharama kubwa. Chini ya nakala hizo haiwezekani ni gharama kubwa zaidi. Na stika zinaagizwa baada ya msanii husika kutoa ‘oda’ yake. Na ili kuwa nafuu lazima uanzie elfu tano.

Filamu zetu zilikuwa bado kuingia kwenye mfumo huo kwa sababu soko lao lilikuwa bado. Kujikweza mpaka kwenye vitu vya msingi kwa maisha yao kuliwaponza. Wasanii wakakimbilia siasa.

Filamu mbili za mwisho za Kanumba ziliuzwa bila familia kupata senti. Yalikuwa malipo ya deni alilokuwa anadaiwa na wasambazaji wa filamu zake. Lakini alifariki ikiaminika ndiye msanii tajiri sana Tanzania.

Hii leo wasanii hata hawana habari na filamu. Wote wamejazana kule kwenye ‘Sinema Zetu’ Azam. Huko ndipo walikotuama, wanaturudisha nyuma enzi za kina Mashaka (R.I.P). Walipotukusanya sebuleni.

Wabongo tulitekwa na michezo ya runinga mwishoni mwa miaka ya 90. Wakati huo kina Bishanga wakiwa ni staa wakubwa zaidi Bongo hii. Vijana kwa watoto walitamani kuwa Seki au Mona. Huku Mambo Hayo, Wakenya wakikimbiza na Tausi.

Baadaye filamu zikaua michezo ya runinga. Kila msanii akawa prodyuza, dairekta, lokesheni meneja, scripti raita na bosi wa kampuni. Hapo kina Kanumba wakawa nyota. Wakapiga pesa ya mdosi bila kubeti.

Nini kilichopo? Michezo ya runinga imerudi kwa kasi iliyoondoka nayo. Wasanii wapo kwenye tamthilia, michongo ya filamu imekufa. Kwenye hizi mishe kina Mafufu wameshika utawala.