NDANI YA BOKSI: Diamond anahitaji akili mpya ‘Kubust’ aliyoanza nayo

Sunday July 31 2022
diamond pic
By Dk Levy

Pisi ya zamani ukikutana nayo leo, kama haina kitambi basi ina rangi ya pili. Nimejiuliza hili swali, nimekosa jibu. Pisi za Afrika kwa nini zinakataa asili yao? Zipo tayari kununua kila kitu bandia na kukivaa mwilini.

Ngozi, nywele, kope, shepu, nyusi, kucha, midomo, hipsi, kalio hata jina. Na wale wa kuitwa ‘slei kwini’ ndio wameendelea zaidi. Wao huvaa nguo feki, sauti feki, hisia feki, utembeaji feki, pozi feki, penzi feki na jina feki.

Amina kawa Myner, Aisha muite Isher, Sikitu na Mwajabu hukataa majina yao. Huko insta unaweza kudhani hakuna Wabongo wenye akaunti. Kumbe wana majina feki. Tabata kuna dem anaitwa Vivica? Na wenye kufuru zaidi hugawa hata watoto feki kwa baba feki. Tukipima vinasaba (DNA) kinguvu, wallah hapatakalika. Unaweza kutoka Bunju hadi Chamazi ukakosa pisi yenye nywele za asili, ni wigi na katani vichwani.

Na kama kweli ni dhambi kukosoa uumbaji, basi totozi zitajaa motoni kuliko peponi. Unafanya upasuaji mpaka wa kuchonga pua, mara ujikwatue rangi, tatizo ni nini?

Ni ushamba wa kiwango cha SGR, kubadili mwonekano. Tuamini kwa tulilojaaliwa tupige goti na kushukuru kwa yote. Macho hudanganya moyo, endapo ubongo utasahau majukumu yake. Umenisoma?

Una nywele feki, kope feki, shepu feki, simu feki, nguo feki, lugha feki, pochi feki, kucha feki, jina feki na ngozi feki. Halafu unasema “Sorry nahitaji mwanamume mkweli.” Kila kitu cha uongo unataka mume mkweli?

Advertisement

Tena insta kuna kila aina ya watu, hayawani, zuzu, wazimu, tutusa, zoba, matapeli, mbumbumbu, dunya na wajasiriamwili. Wachunga kondoo na maustaadh baadhi, wanasiasa na wasanii wapo huko.

Wenzetu hutumia mitandao kifaida. Sisi huku ni kuumizana na kulalamika kama wake wenza. Kila kitu lawama. Jana tulilia na joto, leo tunalia baridi, juzi tulilia tozo. Utaona kesho tunalia na Manara.

Tunaondoa maana ya tunachopokea. Kama dini tunafikia kuuana. Kama siasa waliotuletea wanatushangaa. Kibaya zaidi tunawalilia wao ndio watusuluhishe. Tunalialia kuanzia viongozi na raia.

Mitandao tumeipokea kama dini na siasa. Lengo la waanzilishi tofauti na tunavyoitumia sisi huku. Familia zinasambaratika, ndoa zinavunjika. Watu wanapoteza, kufukuzwa au kuacha kazi kisa mitandao.

Mitandao iko mingi, lakini insta ndiyo kituo kikuu. Huko ndio akili mbovu zina makazi yao. Posti zao utajihisi peke yako ndio una njaa nchi nzima, kumbe wanafeki.

‘Ene wei’ achana na ‘drama’ za insta na pisi za ‘tauni’. Konde Boy, gemu lote la muziki alichezea atakavyo. Na uwanja unainuka kwake. Kwa macho ya wazi na wao wanakiri kushindwa kwenye hili.

Yupo kileleni kikamera mtandaoni na kumiliki mchezo. Karata anazichanga kibabe na wanafuata nyuma yake. Ni ‘denti’ aliyesoma vyema na kulielewa somo kiki akiwa kwa walimu wake kule WCB.

Kuna viumbe matomaso, hawawezi kuelewa hili. Wapo wazima wenye utimamu na vilaza wa oya oya! Konde ni mkuu wa msafara kwa sasa, kwa mbinu na zile njia zao za biashara ya muziki.

Sanaa imekuwa kama ‘shoorumu’ ya wadwanzi. Inatendwa na kulipwa baya kwa jema. Sanaa kama sanaa haina kosa, ila kosa ni kwa wasanii. Baadhi tu kati ya kundi kubwa la sanaa na wasanii.

Wakati long time kwenye game walipokezana vijiti, hawa wa leo wanapokezana kiki. Ndio mchongo uliopo mezani kwa wengi wao.

Imekuwa maiki, gitaa, tarumbeta, ngoma, kinanda, filimbi na kinubi. Wanatuaminisha hilo kwa matendo na maneno na zinavuka mipaka ya utu. Kiki zimejifungua kitoto kiitwacho chawa. Ndani ya kiki kuna chawa na ndani ya chawa kuna kiki. Wakati kiki ni tendo au tukio, chawa ni utu wa mtu kupitia kiki.

Wapo tayari kwa lolote. Wana nguvu na sauti kuliko wazazi wa wasanii. Uchawa ni Mahakama ya migogoro ya wasanii. Wanataka kuwa Basata, visemeo vya sanaa na wasanii.

Na bingwa wa michongo hii tangu na tangu ni Mondi, ndiyo masta wa pigo hizi. Hii sumu kaisambaza kwa vijana wake wanapita kwenye mikono yake. Kwake ndio ‘homu switi homu’ ya kiki.

Huenda ana akili mpya. Ila ubongo upo kwenye fuvu la zamani. Ni wazi Mondi anahitaji akili mpya kwa sasa. Kuna pahala kaatamia na kubaki pale pale. Kulijua hili, unahitaji akili mpya pia.

Amekuwa kama ‘braza’ ambaye ni tajiri kwenye ukoo. Anasikilizwa yeye tu. Mtu wa hivi hawezi kupokea lolote kutoka kwa ndugu zake.

Familia zetu ukiwa nazo utaaminiwa kwa pesa na akili. Usemalo kwao hewala, ndiyo, inashallah, haina shida n.k. Hupati mawazo mbadala toka kwao ya kupinga au kukusahihisha. Hii mbaya sana!

Unabaki kuwa jipu kubwa lisiloguswa, watu wakisubiri litumbuke lenyewe. Ndo Mondi! Kabaki peke yake pale juu anaelea tu kisanaa. Ukimgusa au kumshauri familia (mashabiki) huona unamharibia ‘taita’ wao.

Ukimkosoa tegemea maelfu ya adui kwako. Mashabiki wanamtegemea yeye kwa kila kitu. Akisema kulia au kushoto wao ni twende. Anakosa ‘busta’ ya kumsisimua kisanii kwani anatazamwa yeye tu.

Anajikuta kazi yake ndo kioo cha kazi yake mpya. Hana wa kumtazama kama mshindani wake, bila shaka hata masela wanaomzunguka pia wanamuaminisha hivyo. Mondi sasa anahitaji abustiwe.

Matokeo yake denti wa chuo chake kageuka kuwa ‘Jasiri muongoza njia za kiki’ zake. Konde ni mwanafunzi aliyefaulu vyema mafunzo yao ya kutengeneza kiki na chawa mjini. Anachofanya walimu wanafuata.

Kuanzia chawa wake, walibebwa na ‘ticha’ wake ‘dairekti au indairekti’. Kwa vyovyote familia ya ‘ticha’, iliona kuna haja ya kumiliki jeshi la Konde. Wakabeba chawa wenye nguvu ya kichawa kweli.

Konde akaja na kiki ya Kajala. Licha ya Mondi kuja na mishe za Mtoni na kina Snoop Dog. Bado stori mjini zilikuwa ni bango la Kajala, hapa Konde alifunika na chawa waliohama kambi.

Wapo chawa ambao walijikuta bila kutegemea wakitembea na kiki ya bango la Kajala. Hii ilikuwa ni akili ya denti wa chuo cha WCB, aliyefuzu vizuri somo la kiki mjini. Chawa wale walikosa mvuto.

Kwa sasa mitandao huchafuka kwa picha za Konde na Kajala. Pamoja na Mondi kuibuka na mikato yake ile ile ya zamani kwa kiki yake na Zuchu. Lakini bado Konde Boy na Queen K, wamewaacha mbali.

Konde Boy kutoka kusimamiwa na Mondi. Mpaka kujisimamia na kuwa mshindani wa ‘ticha wake’, kwake ni ushindi mno. Haikuwahi kutokea Mondi Bin Laden kukimbizwa kwa kiki mjini.

Yeye anabaki kuwa msanii mkubwa sana Afrika Mashariki. Sioni mantiki ya kuishi katika mtazamo wa kiki zilezile za enzi za Sepenga. Bila shaka akili iliyomfikisha hapa sasa imegota.

Inahitajika akili mpya ya kuendelea naye huko juu. Hata timu ikipanda daraja huacha kocha na wachezaji walioipandisha na kusajili wachezaji na kocha mpya. Kwa daraja hili la Mondi anahitaji akili mpya.

Advertisement