Mwana FA, Babu Tale wampa tano Rais Samia suala la mirabaha

Mbunge wa Muheza mkoani Tanga Hamis Mwinjuma maarufu Mwana FA na Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamis Taletale maarufu Babu Tale ambaye ni meneja wa staa Diamond Platnumz wamempa tano Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa wasanii kuanza kulipwa mirabaha pindi kazi  zao zitakapochezwa kwenye redio na kuonyeshwa kwenye TV.


Kauli hiyo ya Rais Samia aliitoa jana mjini Mwanza alipokuwa akizungumza na vijana  ambapo amesema  ulipaji huo utaanza rasmi Desemba mwaka huu.


Akitoa maoni yake, Mwana FA amesema amefurahishwa kauli hiyo ya Rais kuhusu suala la mirabaha na limempa moyo.


“Kwa muda mrefu nimekuwa kwenye harakati  za kutaka watu walipwe kwani kuna sehemu nyingi kazi hizi za Sanaa zinapaswa kulipwa.


“Mimi naliona mbali zaidi kwa sababu hili haliendi kuwanufaisha tu wasanii bali na serikali na ukweli ni kuwa  hali za wasanii nchi hii ni mbaya,hali za kiunchumi za  maprodyuza ni mbaya, watunzi ni mbaya zaidi.


'Hivyo kulipwa mrabaha kutakuwa na mgawanyo kila mtu ambaye ameshiriki kwa namna moja au nyingine ktengeneza kazi ya Sanaa anatakiwa kufaidika.


Tukienda mbali zaidi tukaanza kukusanya kwenye sehemu za umma zinazotumia kazi za Sanaa kutakuwa na hela nyingi sio tu kwa wasanii bali na serikali kupata kodi yake, lakini juu ya yote wasanii mchango wao unatakiwa kuonekana moja kwa moja kwenye mapato ya nchi hii.


Kwa upande wake Babu Tale amesema kila siku Rais Samia anazidi kuwafurahisha watu wa sekta ya Sanaa na kuonyesha mchezo huo anaupatia kwani suala la mirabaha ni jambo walilolipigania miaka kumi iliyopita.


Hata hivyo katika kutekeleza hili, Tale ameomba katika Chama cha Hakimiliki (Cosota) ambao ndiyo wasimamizi wa  malipo hayo kuwepo pia na wasanii kwa kuwa hawa ndio wanajua wanayoyapitia wasanii.