Mwana FA asomba Kijiji Mbeya Tulia Marathon

Muktasari:

  • Leo ndio hitimisho kwa mbio za Mbeya Tulia Marathon ambazo kwa mara ya kwanza mwaka huu zimetumia siku mbili tofauti na nyuma.

Mbeya. Msanii wa Hip Hop, Hamis Mwinjuma 'Mwana FA', ametumia dakika tano pekee 'kukusanya kijiji' wakati alipopanda stejini kukumbushia kipaji chake katika muziki.

Staa huyo ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Muheza mkoani Tanga, alipanda jukwaani kwa dakika tano akipanga mistali kadhaa na kujikuta 'akivamiwa' na nyomi ya wananchi waliokuwa pembeni.

Mwana FA hakuwa na mambo mengi baada ya kukaribishwa na mshereheshaji ili kutoa burudani katika mashindano ya mbio za Mbeya Tulia Marathon inayoendelea katika uwanja wa Sokoine jijini hapa.

Msanii huyo baada ya kupewa kipaza sauti na kutoa mistali yake, ghafla wananchi na viongozi waliokuwa jukwaa kuu wakiongozwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson walijaa stejini kumuunga mkono.

Mbio za Mbeya Tulia Marathon ni msimu wake wa tano ambapo leo ndio kilele kwa mbio ndefu za Km 42, 21,10 na tano baada ya jana kukamilika kwa zile fupi za mita 100, 200, 400, 800 na 1500.