Mngereza aagwa nyumbani, kesho Karimjee

Mamia ya watu wamejitokeza kutoa heshima za mwisho nyumbani kwa Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa la Taifa (Basata),  marehemu Godfrey Mngereza.
Mngereza alifariki Desemba 24 katika hospitali ya mkoa wa Dodoma  baada ya kujisikia vibaya ghafla akiwa katika shughuli za kikazi mkoani humo.  
Mwili wa Mngereza uliwasili kwenye uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere saa 3:00 asubuhi kisha kupelekwa nyumbani kwake Kibamba Luguruni, jijini Dar es Salaam ambapo kulifanyika ibada fupi na kisha watu kuruhusiwa kuaga.
Akitoa salamu za rambirambi,  mwakilishi kutoka Basata ambaye pia ni Mwenyekiti wa bodi ya baraza hilo Dk Emmanuel Ishengoma,  alisema Basata imepoteza kamusi ya sanaa.
Dk Ishengoma amesema Mngereza ameondoka wakati Rais akiwataka watendaji wanaosimamia tasnia ya sanaa kufanya kazi na kuhakikisha wasanii wananufaika na kazi zao.
"Mngereza kaondoka kipindi Rais anataka kuona wasanii wanafaidika na kazi zao, inatosha kusema tumepoteza dictionary (kamusi) hivyo yatupasa kujipanga upya, tunaomba Mungu atupatie mtu mwingine atakayeweza kuziba pengo lake. ," amesema DK Ishengoma.
Msemaji  wa familia  Rubeni Mngereza, alisema wamefarijika kuona umati mkubwa wa watu waliojitokeza kuwapa faraja na kuonyesha kwa namna gani ndugu yao alikuwa  muhimu na si tu kwa familia bali na kwa nchi.
Shughuli nyingine ya kuaga itafanyika  kesho Desemba 29  kwenye ukumbi wa Karimjee kabla ya mwili kusafirishwa  kuelekea kijijini kwao Suji Same mkoani Kilimanjaro ambapo maziko yatafanyika keshokutwa Jumatano.