Mitano tena kwa Harmonize

MSANII Harmonize ametimiza miaka mitano tangu atoke na kutambulika rasmi kwenye muziki wa Bongo Fleva.

Wimbo uliomtoa kimuziki uitwayo Aiyola ulitoka Agosti 25, 2015 ukitayarishwa ndani ya studio za Kazi Kwanza Record chini ya Prodyuza Maxmaizer.

Video ya wimbo huo ilifanyika jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini na kutoka Novemba 6, 2015 ikiwa imeongozwa na Director Nick Roux.

Ni wazi kipaji chake kilionekana kikubwa na ndio sababu lebo ya WCB (Wasafi) ya Diamon Platnumz haikuona tabu kutoa fedha kwa ajili ya kufanya video hiyo inayotajwa kuwa ya gharama kubwa kwa msanii ambaye bado hajulikani.

Kwa mujibu wa Diamond, video ya Aiyola iligharimu Sh39 milioni. Hata hivyo uwekezaji uliofanyika hadi jina la Harmonize kuwa kubwa ndani ya Bongo Fleva ni Sh115 milioni.

Wimbo Aiyola ukawa mkubwa kwa kiasi chake na kuvutia wengi ndani na nje ya nchi na haikuwa ajabu pale msanii wa Nigeria, Kiss Daniel kuonyesha kuukubali wimbo huo.

Na huo ukawa mwanzo wa kupata maisha mazuri kupitia muziki kutoka maisha ya kubangaiza katika mitaa ya Kariakoo, Dar es Salaam hadi kuwa staa mkubwa katika muziki.

Mafanikio ya wimbo huo yalichangia Harmonize kushinda tuzo za African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) zilizotolewa Dallas, Texas nchini Marekani katika kipengele cha Msanii Bora Chipukizi mwaka 2016.

Lakini kabla ya Aiyola kutoka tayari alikuwa amesharekodi wimbo uitwao Kidonda Changu ambao hakufanya vizuri kipindi kabla hajasaini WCB.

Wimbo huo (Kidonda Changu) ndio ulisababisha Diamond kuona Harmonize ni mgodi unaotembea sema tu haujashtukiwa na wanaapolo waliopo katika tasnia.

Basi wimbo huo ukampata Harmonize nafasi ya kutumbuiza kwa mara ya kwanza kwenye jukwaa moja na Diamond ndani ya ukumbi wa Dar Live.

Hiyo ni baada ya kumtumia Diamond wimbo huo kupitia mtandao wa WhatsApp na akaupenda, ndipo akampatia namba za Meneja Ricard Momo kwa ajili ya mawasiliano, kisha nafasi hiyo ya kutumbuiza ikapatikana na historia ikaja kuandikwa.

Usiku wa kuamkia Juni 17, 2018 Harmonize alikuwa na shoo yake aliyoipa jina la Kusi Night pande za Dar Live ambapo alisindikizwa na wasanii kama Queen Darleen, Ben Pol, Country Boy na wengineo.

Diamond ambaye hakutangazwa kuwepo kwenye shoo hiyo, alikuja kama ‘sapraizi’ akitokea Next Door Arena ambapo alimsindikiza Davido kutokea Nigeria kwenye shoo yake.

Ujio wa Diamond katika shoo hiyo ulimtoa Harmonize machozi, ghafla alishindwa kutumbuiza wimbo wao ‘Bado’ na kuchuchumaa kuanza kulia.

Kilio hicho cha furaha ni kutokana na kuwa hapo ndipo walikutana kwa mara ya kwanza na ndio sehemu alifanya shoo yake ya kwanza kubwa na Diamond kabla hata hajatoka kimuziki.

Katika shoo hiyo wawili hao walitumbuiza nyimbo mbili walizofanya pamoja ambazo ni Bado na Kwangwaru ambayo ndio ilikuwa kwenye kilele cha mafanikio yake.

Nyimbo hizi mbili ndio zenye mafanikio makubwa zaidi kwenye muziki wa Harmonize kwa muziki wa mtandao wa YouTube.

Katika chaneli ya Harmonize video ya wimbo Kwangwaru ndio inaongozwa kwa kutazamwa zaidi ikiwa imetazamwa (views) zaidi ya mara 75 milioni ikifuatiwa na video ya wimbo ‘Bado’ ikiwa imetazamwa zaidi mara 29 milioni.

Wakati wimbo Kwangwaru ukitoka, tayari Harmonize alikuwa amefanya kolabo na wasanii kutoka nchi mbalimbali barani Afrika miongoni mwao ni Marina (Rwanda), Yemi Alade (Nigeria), Eddy Kenzo (Uganda), Emma Nyra (Nigeria), Willy Paul (Kenya), IYO (Nigeria), OmoAkin (Nigeria), Korede Bello (Nigeria), Sarkodie (Ghana) na kadhalika.

Kutokana na mafanikio hayo kimuziki, haikuwa ajabu kwa msanii huyo kutajwa kuwa miongoni mwa wasanii wa Bongo Fleva wenye fedha nyingi.

Mwanzoni mwa 2018 Diamond akizungumza na kipindi cha The Playlist kilichokuwa kinaruka Times FM, alisema Harmonize ni miongoni mwa wasanii ambao anajua wana fedha nyingi mno katika lebo yake wakati huo.

“Naweza kusema kama wasanii wangu waliokuwepo WCB, msanii mwenye hela ni Harmonize, muziki wake una riziki kubwa,” alisema Diamond.

Inadaiwa tayari Harmonize alikuwa amechukua sehemu ya fedha zake na kununua baadhi ya vifaa kwa ajili ya kampuni ya kutengeneza video ya muziki iitwayo Zoom Production ambayo kwa sasa inajulikana kama Zoom Extra.

Aliamua kufanya hivyo baada ya kuona wanatumia fedha nyingi kwenda nje ya nchi kutengeneza video kwa kampuni zenye vifaa vya kisasa inavyoendana na mahitaji yaliyopo kwenye soko lenye ushindani.

Kuelekea mwishoni mwa 2019 Harmonize aliamua kuondoka kwenye lebo ya WCB Wasafi akiwa ni msanii wa pili kufanya hivyo baada ya Rich Mavoko.

Na hapo ndipo kampuni ya Zoom Production ikahama kwenda Zoom Extra na kuzipa nguvu zile tetesi zilizodai Harmonize alikuwa sehemu ya umiliki wa kampuni hiyo iliyo chini ya WCB.

Kuondoka kwake WCB ukawa ni mwanzo mpya wa Harmonize kupata changamoto nyingine kwenye muziki na kufikia mafanikio makubwa zaidi.

Aliondoka katika lebo hiyo akiwa tayari ametoa Extended Playlist (EP) iitwayo Afro Bongo akiwashirikisha Yemi Alade, Mr. Eazi na Burna Boy.

Hata hivyo, kuondoka WCB haikuwa kazi rahisi, kwa mujibu wa Harmonize mwenyewe alidai kuwa ili kuvunja mkataba wake na lebo hiyo ilimlazimu kulipa Sh500 milioni aweze kuwa huru.

Usiku wa uzinduzi wa albamu ya Afro East, Machi 14, 2020 aliulizwa na Mtangazaji Diva kama tayari amelipa fedha hizo. Jibu la Harmonize lilikuwa ameshamaliza deni ambalo awali alidai lilimfanya kuuza nyumba zake tatu.

Hilo likapita na uzinduzi wa albamu hiyo ukachukua nafasi yake, huku Rais mstaafu Jayaka Kikwete akiwa mgeni rasmi akisikiliza wimbo wa kwanza hadi wa mwisho.

Miongoni mwa wasanii walioshirikishwa kwenye albamu hiyo ni Burna Boy, Mr Blue, Lady Jaydee, Morgan Heritage, Khaligraph Jones, Phyno, Skales, Yemi Alade, Mr. Eazi, Falz na wengineo. Kilichofuata baada ya hapo ni Harmonize kuanza kusaini wasanii katika lebo yake - Konde Music Worldwide aliyoianzisha baada ya kuondoka WCB.

Ibraah ndiye alikuwa msanii wa kwanza kusainiwa na kuachia EP yake iitwayo Steps, kisha akafuata Country Boy ambaye naye aliachia EP ya The Father.

Hadi kufikia sasa Konde Music Worldwide ina idadi sawa ya wasanii na WCB ambayo ukimtoa Diamond kama kiongozi ina Rayvanny, Queen Darleen, Lava Lava, Mbosso na Zuchu - hao jumla yao ni watano.

Kwa upande wa Konde Music ukimtoa Harmonize kama kiongozi kuna Ibraah, Skales, Country Boy, Cheed na Killy - pia hao ni watano.

Kutokana na mafanikio aliyopata Harmonize kwa kipindi cha miaka mitano licha ya changamoto kubwa ‘Kamati Kuu ya Muziki wa Bongo Fleva’ imesema “Mitano tena kwa Konde Boy” aendelee kutoa burudani isiyopimika kwa mizani.

Kazi ni kwake, chama hiki kina imani kubwa na yeye kwamba daima atatenda haki wakati akitekeleza jukumu lake la kutoa burudani ndani na nje ya nchi.


Imeandikwa na Peter Akaro