Mashabiki wamrejesha Cheka Morogoro, amvutia kasi 'mbabe' wa Mwakinyo

BINGWA wa WBF Mabara, Francis Cheka.

Muktasari:

Cheka tangu Desemba 26, 2018 alipochapwa kwa Knock Out (KO) na Abdallah Pazi 'Dullah Mbabe' hakuwahi kupanda ulingoni kuzichapa hadi sasa.

Bondia Francis Cheka amelazimika kuhamishia pambano lake na Shaban Kaoneka mjini Morogoro.

Cheka atazichapa Mei Mosi na Kaoneka bondia pekee nchini aliyewahi kumchapa Hassan Mwakinyo.

Pambano hilo la uzani wa light heavy la raundi 10 awali lilipangwa kufanyika jijini Arusha Aprili 28, lakini waandaaji wamelihamishia Morogoro na sasa litapigwa Mei Mosi.

Cheka amesema amelazimika kurudi Morogoro ambako ndiko alipatia mafanikio kwenye ndondi ili mashabiki wake mkoani humo wakashuhudie kurejea kwake upya ulingoni baada ya miaka miwili kupita akiwa nje ya ulingo.

"Tayari niko Morogoro na nimeanza kambi kujiandaa na pambano hilo," amesema Cheka leo.

Amesema awali pambano lake lilipangwa kufanyika Arusha, lakini kutokana na ombi la mashabiki wake wa mkoani Morogoro, waandaaji wamelazimika kulihamisha.

"Mashabiki wangu wamekuwa wakinihoji ni kwanini sirudi ulingoni, niliamua kukaa kando ili kujipanga upya baada ya kupoteza pambano na Dullah Mbabe, hata hivyo nilipotangaza kurudi, mashabiki wa Morogoro wameniomba nikacheze nyumbani kwanza," amesema bondia huyo na kuongeza.

"Nilipopigwa na Mbabe nilijitafakari na kubaini sikujiandaa, japo sikutarajia kupigwa KO, lakini ngumi ni mchezo kama michezo mingine na una matokeo matatu pia, hivyo narudi upya na sitowaangusha mashabiki wangu kote nchini," amesema.

Kocha wake, Abdallah Salehe 'Comando' amempa bondia huyo miaka minne ya kuendelea kutamba kama atafanya mazoezi na kufuata misingi ya ngumi za kulipwa.

"Cheka hajashuka kiwango, sema alikuwa akizembea mazoezi, kama atatulia na kujifua kwa kufuata misingi ya ngumi, naamini atawashangaza wengi ulingoni," amesema kocha huyo.

Cheka anarudi ulingoni akiwa na rekodi ya kupigana mapambano 48 na kushinda 34 (18 kwa KO), amepigwa mara 13 (8 kwa KO) na kutoka sare mara mbili.