Mambo 10 ya moto kuhusu ‘Only One King’ ya Alikiba

Mambo 10 ya moto kuhusu ‘Only One King’ ya Alikiba

Muktasari:

  • Yes, hakuna ubishi kuwa Alikiba ndiyo mfalme wa muziki wa kizazi kipya kama ambavyo mwenyewe hujinasibu.

Yes, hakuna ubishi kuwa Alikiba ndiyo mfalme wa muziki wa kizazi kipya kama ambavyo mwenyewe hujinasibu.

Amedhihirisha hilo katika hafla ya kusikiliza albamu yake mpya iitwayo ‘Only One King’, mbali ya kuifanyia katika hoteli kubwa ya Serena, pia alialika waimbaji wakongwe. Mbali na kufurahi pamoja naye, pia walimpa pongezi, maoni na ushauri.

Albamu hiyo ya tatu kwa Kiba yenye nyimbo 16, imetoka ikiwa ni miaka 11 tangu alipoachia albamu yake ya kwanza mwaka 2007 ‘Cinderella’ iliyokuwa na nyimbo 15 na ikafuata Ali K4Real 2009.

Haya ni mambo 10 unayopawa kuyafahamu kuhusu albamu hii ambayo hafla ya uzinduzi wake ilifana na pia imepata mapokezi makubwa kutoka kwa mashabiki.

1. Hii ni albamu ya tatu kwa Alikiba, alianza na Cinderella (2007) ikafuata Ali K4Real (2009), na sasa Only One King (2021), hivyo Alikiba hajawahi kutoa albamu mwaka unaogawanyika kwa mbili.

2. Kingine chepesi lakini si rahisi kukibaini kwa haraka haraka ni albamu hii haijamshirikisha msanii hata mmoja wa kike. Pia katika lebo yake hakuna msanii wa kike.

3. Pia hii ni albamu ya pili kutoka mwezi huu (Oktoba), ya kwanza ni ‘Gift of Life’ yake Best Naso.

4. Wasanii wa Bongofleva walioshirikishwa kwenye albamu hii ni kutoka kwenye lebo yake ‘Kings Music’ tu, ambao ni Abdukiba, K2ga na Tommy Flavour.

5. Khalighara Jones toka Kenya ndio msanii pekee wa Hip Hop Afrika Mashariki, aliyeshirikishwa kwenye albamu hiyo. Huyu ndiye Rapa wa mwisho ukanda huo kushinda tuzo ya African Muzik Magazine Awards (Afrimma) 2018 katika kipengele cha msanii bora wa Hip Hop Afrika hadi sasa.

6. Ni nchi tano tu ambazo wasanii wake wameshiriki kwenye albamu hii, ambazo ni Tanzania, Ghana, Afrika Kusini, Nigeria na Kenya ambayo ndio imetoa wasanii wengi.

7. Lugha zilizotumika kwenye albamu hii ni tatu ambazo ni Kiingereza, Kifaransa na Kiswahili ambacho kimechukua zaidi ya asilimia 90, lakini jina la albamu yenyewe ‘On One King’ limetumia Kiingereza na hakuna albamu ya Bongofleva iliyotoka mwaka huu yenye jina la Kiswahili.

8. Kuna makundi mawili ya muziki ambayo yameshiriki kwenye albamu hii, nayo ni Sauti Sol kutoka Kenya na Blaq Diamond ya Afrika Kusini.

9. Albamu hii imeachiwa chini ya Ziiki Media na Kings Music yake Alikiba. Ziiki Media pia ndio walisimamia albamu ya Darassa ‘Slave Becomes A king’ iliyotoka Desemba 2020 ambayo pia Alikiba alishirikishwa.

10. Mara baada ya kuachiwa albamu hii ilifikisha wasikilizaji (streams) zaidi ya 100,000 ndani ya saa sita pekee kwenye mtandao wa Boomplay Music na kuwa ya kwanza Bongo kufanya hivyo. Ni rekodi kwa Kiba, na hiyo ndio maana halisi ya ‘Only One King’.