Mama King Zilla: Nimetapeliwa haki za mwanangu

MWAKA 2019, msanii wa muziki wa kizazi kipya aina ya hip hop, King Zilla alifariki dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi, lakini mama mzazi wa mwanamuziki huyo kalalamikia kutapeliwa haki za mwanaye, akisema inamuumiza zaidi maishani mwake.

Msanii huyo alitamba na nyimbo mbalimbali ikiwemo Get Off My Way.Kifo chake kilitikisa tasnia na wadau waliokuwa wanaukubali muziki wake.

Mwanaspoti lilifunga safari hadi nyumbani kwa mama yake, Marry Charles anayeishi Mbezi Salasala, Dar es Salaam ambaye anadai bado anahisi kama vile yupo ndotoni kwamba mwanaye hayupo naye.

Baada ya kufika waandishi wa makala haya walipokewa na dada yake Zilla aitwaye Joyce aliyeeleza kwamba mama’ke ameenda kanisani, ingawa baada ya muda mfupi aliwasili.

Mama huyo aliingia akiwa na rozali na kitabu cha dini ya Kikristo (Biblia), ukimya ulitawala ambapo alinyanyua mikono juu akilia kwa uchungu akiomba Mungu ampe nguvu na faraja.


HAKI ZA MWANAWE

Mama huyo anasema King Zilla alikuwa na akaunti katika mitandao mbalimbali ya muziki, sehemu ambayo mpaka leo nyimbo zake bado zipo na zinaendelea kusikilizwa.

Kwa upande wa Youtube bado watu wanaendelea kufuatilia nyimbo za msanii huyo na kuingiza pesa kama ilivyo kwa wengine. “Kiukweli sijawahi kupata chochote kutoka katika kazi za mwanangu,wakati wa msiba wapo ambao walichukua laini ya simu ya mwanangu wakasema kuna vitu wanafuatilia ila kimya mpaka sasa hakuna,” anasema.

Anasema hata upande wa haki za mitandao aliwahi kuletewa mkataba lakini aligoma kusaini na kuupeleka kwa mwanasheria anayesali naye aliyemshauri kupangua baadhi ya vipengele. “MX (anayehusika na masuala ya mitandao) alikuja na mkataba lakini kuna vipengele havikukaa sawa kwahiyo tukaomba tuupitie, ila yeye ndio nilimpa mpaka cheti cha kifo kwa ajili ya kuwapelekea sijui wazungu ili tuweze kupata haki za mwanangu, lakini bado kimya,” anasema mama huyo.

“(Mwanaye) alikuwa anaidai kampuni moja ya simu (jina analitaja) lakini deni hilo limekuwa kizungumkuti, rafiki yake wa karibu ni kama hatumuelewi hajawahi kusema lolote.”


EKA 5 ZA ARDHI

Marry anasema mwanaye alibahatika kununua shamba la eka tano lililokuwa Saadani, Bagamoyo, lakini lilitapeliwa.

“Nilienda naye kununua shamba, tulichukua na nyaraka zote tunazo, lakini sasa hivi pale pamechukuliwa na tajiri mmoja ambaye amefungua kiwanda cha sukari,” anasema.

“Hivyo sina sehemu sahihi yoyote ambayo naweza kulalamika, lakini kama mtu yeyote anaweza kunisaidia basi naomba anisaidie.”

Hata baada ya kuulizwa maisha yake baada ya mwanaye kuondoka duniani na kama wasanii wenzake wanamfariji kwa kumtembelea, anabadilika kisha anatoa sauti ya kilio akisema Mungu wake amsaidie

“Ahsanteni hata nyie wanangu kwa kuja kwani ni muda sijawaona watu kama nyie katika nyumba yangu.”

Marry anasema kwa miaka miwili amekuwa akifunga na kusali ili mwanaye huko aliko awe sehemu nzuri. “Kiukweli toka alivyofariki nilianza kufunga na kusali siku zote mpaka leo, ndio maana hata hapa nimetoka kusali,” anasema


MARCO CHALI, FID Q

Kuhusu wasanii na wadau wa sanaa wanaomkumbuka, mama huyo anasema kwamba tangu mwanaye alifariki dunia alimewahi kupokea simu kutoka kwa Marco Chali.

Anasema: “Marco Chali alinipigia simu na baada ya hapo alinitumia nakumbuka ilikuwa ni Sh150,000 ya kutumia, nilishukuru na kumuombea aongezewe alipopunguza.”

“Yaani haya maisha dah, yupo msanii Giddy ni kama ndugu yetu toka zamani, pamoja na rafiki yake marehemu anayeitwa Doreen huwa tunawasiliana mara kwa mara.

“Fid Q alisimamia ahadi ya kuwa na duka la dawa kiukweli ni kwamba nilipata dawa zote, nililetewa kutoka duka la dawa za jumla zikiwa na risiti halali ambazo zililipwa na mwenyewe na aliniambia nisisite kupiga simu kama tumetikisika kwa namna moja ama nyingine.”