Kuenguliwa kwa Rose kushiriki Miss World kwaibua mapya

Kuenguliwa kwa Rose kushiriki Miss World kwaibua mapya

Muktasari:

  • Baada ya kamati ya Miss Tanzania kuanika makosa sita yaliyomtia hatiani Miss Tanzania, Rose Manfere na kumuengua  kushiriki shindano la Miss World, mwanasheria wake  Emily  Laus  amesema alichofanyiwa mteja wake ni kukaidi maagizo ya Serikali ya Tanzania.

Dar es Salaam. Baada ya kamati ya Miss Tanzania kuanika makosa sita yaliyomtia hatiani Miss Tanzania, Rose Manfere na kumuengua  kushiriki shindano la Miss World, mwanasheria wake  Emily  Laus  amesema alichofanyiwa mteja wake ni kukaidi maagizo ya Serikali ya Tanzania.

Sambamba na kutaja makosa hayo sita, pia kamati hiyo imeeleza tayari imepeleka jina la mshindi wa pili, Juliana Rugamisa kwa ajili ya kushiriki shindano hilo badala ya Rose.

Mwenyekiti wa kamati ya Miss Tanzania, Azama Mwangosa amesema wana haki ya kupeleka jina la mrembo wanayemuona anafaa kwa kuwa wao ndio wenye mkataba na Miss World na wanajua wanataka mrembo wa aina gani.

Akizungumza na Mwananchi Digital jana Jumamosi Julai 17, 2021  mwanasheria huyo amesema kilichofanywa ni dharau kwa Serikali kutokana na maagizo yaliyotolewa na  Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) Julai 14,  2021  ya nini kamati hiyo inatakiwa ifanye ikiwemo kusitisha kupeleka jina la mshindi wa pili kwa kuwa bado vikao vilikuwa vinaendelea kuhusu  sakata hilo.

Amesema  kikao  kingine ilikuwa kifanyike Julai 23, 2021 baada ya wajumbe wa kamati kushindwa kutokea katika kikao cha kwanza.

“Hii kamati ilishindwa kuja kwenye kikao Julai 14,  2021 tulivyoitwa tukutane nao na mteja wangu kwa ajili ya kuzungumzia jambo hilo kwa kile walichoeleza kuwa walikuwa wametingwa na majukumu mengine  na badala yake wameagizwa kufika Julai 23."

“Sasa nashangaa hayo maamuzi waliyoyafanya ya kupeleka jina la mrembo  mwingine wakati iliagizwa na Basata apelekwe Rose, hii ni dharau kubwa kwa Serikali ila tutalizungumza vizuri hili baada ya kikao cha Julai 23 ya nini tumeamua na mteja wangu kwa sasa nisingependa kuongea sana,” amesema mwanasheria huyo.

Katika kikao cha Julai 14 kilichoitishwa na Basata kuwakutanisha Rose na kamati, baraza hilo lilitoa  maagizo manne  ikiwemo jina la Rose   lipelekwe kushiriki Miss World na sio Juliana.

Maagizo mengine ni kupeleka jina la mkurugenzi mwingine baada ya aliyekuwepo, Basilla Mwanukuzi kuteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Korogwe na kupeleka uthibitisho wa makosa anayotuhumiwa Rose.