KINGPUSI ALIVYOPENYEA KWA MARIOO

Saturday May 01 2021
KINPUS PIC
By Nasra Abdallah

WAPO watu ambao kwa sababu ya sura na muonekano wao mzuri wamejikuta ghafla ni wasanii na wapo ambao walishikwa mkono na mastaa hadi nao wakatoa.

Na wapo pia ambao wamefanya kituko kimoja cha ajabu hichohicho kikawabeba na kujikuta maarufu kuliko hata mastaa waliokutangulia kitambo.

Hii haiko mbali sana na msanii Ibrahim Walumona maarufu kwa jina la kisanii, Kingpusi ambaye alipata umaarufu zaidi alipoonekana katika video ya Chibonge.

Wimbo huo uliotoka mwaka jana umeimbwa na mtayarishaji maarufu wa muziki Abbah na kuwashirikisha wasanii wengine akiwemo Marioo, G Nako na Byter Beast.

Video ya wimbo huo imenogeshwa vilivyo na msanii Kingpusi ambaye aliunganishwa kufanya dili hilo na Marioo na kujikuta ndio unamfungulia njia ya mafanikio aliyonayo leo.

Mwanaspoti imepata wasaa wa kufanya mahojiano na Kingpusi ambaye ameeleza mengi kuhusiana na safari yake mpaka kufikia alipo.

Advertisement

Kingpusi anasema safari yake ya sanaa ilianzia mkoani Kigoma sehemu alikozaliwa na akiwa na umri wa miaka kumi alishaigiza na kuchekesha kwenye shughuli mbalimbali.

Ni katika safari hiyo alikuwa akichukuliwa hadi na baadhi ya makanisa kuigiza maigizo ya kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo kuelekea siku ya Sikukuu ya Pasaka.

Hata hivyo, ilipofika mwaka 2010 alijiingiza katika makundi ya kudansi kwa kucheza kwenye majukwaa mbalimbali ambapo alikuwa akivaa matambara tumboni kuonekana mtu mwenye kitambi fulani.

“Licha ya kubadili upepo na kuingia kwenye sanaa hii hii ya kudansi kwangu bado ilikuwa hainilipi na kiu yangu ilikuwa kusogeza sanaa yangu mbele na nikawa na hamu hata ya kwenda Dar es Salaam kwa kuamini kule kuna wasanii wengi huenda wakanishika mkono,” anasema.

Anasema alikuwa akimsimulia ndoto hiyo ya kwenda Dar rafikiye aitwaye Ali Kadu, na siku moja mwaka 2015, rafikiye huyo akaona kwa jirani kuna msiba na hapo ndipo alipopata wazo la kumwambia Kingpusi ajaribu kutumia gari litakalosafirisha msiba kwenda Dar.

“Wazo la rafiki yangu sikulipinga, hivyo nikajibebea nguo mbili tatu, na ilipofika saa 11 jioni safari ikaanza, na kule kwenye gari alishazungumza na dereva mchongo mzima hivyo sikupata tabu ya kuulizwa maswali.

“Safari yetu ilituchukua siku mbili na tulipofika maeneo ya Mbezi, Dar es Salaam ndipo msiba ulipokuwa hivyo gari likaishia hapa na sisi ikatupasa kutembea kwa miguu hadi Ubungo.

“Wakati huo kumbe mwenzangu alikuwa kuna mtu ameshaongea naye alikuwa amekwenda kwa ajili ya kazi ya kupaka rangi kucha na ameambiwa aende peke yake.

“Hivyo alichokifanya kwangu ni kunipa Sh. 20,000 na akapotea mazima mpaka leo sina mawasiliano naye na hivyo kuanza kutafuta malazi na hapo ndipo nikajikuta nakwenda stendi mabasi ya kwenda mikoani ya Ubungo na kuwa ndio makazi yangu.” anasema.

Anasema aliishi kwenye stendi hiyo ambayo kwa sasa imehamishiwa Mbezi Luis, kwa muda wa miezi mitatu na kueleza chakula alichokuwa akitegemea ni makombo waliokuwa wakibakiza wasafiri kwenye mabasi.

Akiwa huko stendi ya Ubungo alikutana na mtu anaitwa Beko na kutokea kumpenda na kumueleza kuwa ana saluni, hivyo kama ataweza anaweza kuwa anaenda kufanya usafi pale kila siku ili kuweza kupata shilingi ya kumuwezesha kuishi, jambo ambalo alimkubalia.

Akiwa huko jirani kulikuwa na mama ana baa, akamhurumia maisha aliyokuwa anaishi ya kulala stendi, hivyo akamruhusu jioni akishafunga awe analala kwenye baa yake hiyo na mwisho wa siku akamfungulia kijiwe cha chipsi.

Aliishi hapo kwa muda wa mwaka mmoja huku akiwa anatengeneza chipsi, pia akiendelea na harakati zake za kutafuta watu wa kumsaidia kisanii na ndipo siku moja akakutana na wasanii wanaocheza kwenye kampeni ya uchangiaji damu maeneo ya Magomeni.

“Nilipowaona wasanii hao niliwafuata na nikawaeleza mimi pia nina kipaji hicho, mmojawapo anayeitwa Ally akanikabidhi redio na kuniambia niwe napita mtaani napaka masinzi usoni na kutengeneza tumbo kubwa la vitambaa niwe nacheza sitakosa Sh2,000.

“Wakati nikiwa nafanya shughuli hiyo, siku moja nikakutana tena na wasanii wanaocheza kwenye magari ya matangazo ya bidhaa nikaweleza mimi ni mchekeshaji ambapo walinielekeza kwa bosi wao, ambaye naye alinipa mtihani niende nikajirekodi tangazo la moja ya kinywaji halafu nimpelekee CD yake.

“Hapa nako ilikuwa mtihani kwangu kwani siku na pesa ya kurekodia hilo tangazo ila kwa kuwa pia kwenye chipsi nilikuwa nikicheza mchezo wa upatu, nikaomba kutafuta mtu achukue jina langu na hela nilizokuwa nimeshawekeza nirudishiwe.”

Fedha hizo anasema ndizo zilimwezesha kwenda kurekodi tangazo hilo japokuwa aliyemtuma kufanya hivyo hakufanikiwa kumuona mpaka leo na alisota ofisi za hicho kinywaji bila ya mafanikio.

Aliendelea na harakati zake za kucheza muziki mtaani mpaka siku moja alipokutana na wasanii wa bendi ya Malaika, Petie Mauzo na Fabic Mauzo ambao hawa walimpa hifadhi mpaka siku ameanza kutoboa na kujitegemea.

“Nakumbuka siku moja Malaika Band walikuwa wamealikwa kwenye shoo ya Miss Kinondoni, ambapo walinichomeka nikapata nafasi ya kufanya shoo ya kuchekesha na hapo ndipo nilipowaeleza pia ukweli wa maisha yangu na kunionea huruma na kuamua kunichukua na kuishi nao,” anasema.

Katika kuishi nao maeneo ya Magomeni, anasema alikuwa akiwafanyia shughuli mbalimbali ikiwemo kuwapikia na kuwafulia, ilimradi tu apate sehemu ya kula na kulala.

“Baadaye mara kadhaa nikapata dili za kwenda kufanya kazi mkoani mwezi mzima za kucheza jukwaani kutangaza bidhaa, kwa siku nalipwa Sh25,000. Miezi ikapita. Nikanunua kamera, boom micrrophone na vifaa vyingine na kuanzisha kikundi changu cha kudansi nikiwa na kinadada vibonge ninao 17 sasa ambao nawalipa kwa mwezi,” anasema Kingpusi ambaye sasa anaishi vyema kiasi tofauti na alipokuja Dar.

Advertisement