Kilichokatisha uhai wa Cpwaa hiki hapa...

Mwili wa msanii wa muziki kizazi kipya Ilunga Khalifa 'Cpwaa' utazikwa leo saa 10 jioni jijini Dar es Salaam.

Akitoa utaratibu wa mazishi, kaka mdogo wa msanii huyo ambaye alikuwa akimuuguza kipindi chote cha maradhi, Murad Omar Khamis amesema kaka yake atazikwa Magomeni jijini Dar es Salaam katika makaburi ya Mwinyimkuu.

"Kaka tutampuzisha leo leo saa 10 katika makaburi ya Mwinyimkuu. Tunasubiri mwili wake ufike kutoka hospitali," amesema Murad

Akielezea kilichopelekea kifo cha msanii huyo, Murad amesema kaka yake alikuwa akisumbuliwa na pnemounia kwa wiki sasa lakini alizidiwa wiki hii na walimkibiza hospitali ambapo alilazwa kabla ya umauti kumfika usiku wa kuamkia leo Januari 17.

"Alikuwa anaumwa wiki mbili zilizopita, na akaja kuishi hapa nyumbani kwa mama yake. Ila Jumatano alizidiwa ndo tukamkimbiza hospitali muhimbili, alilazwa ICU," amesema

Msiba wa Cpwaa uko Magomeni Usalama nyumbani kwa mama yake mzazi, na tayari majirani, ndugu na jamaa wameanza kufika eneo la msiba.