Kamati ya Miss Tanzania, Basata watunishiana misuli

Sunday July 18 2021
basata pc
By Nasra Abdallah

July 14 kuliibuka gumzo baada ya kusambaa kwa taarifa mitandaoni kuwa Miss Tanzania 2020/2021, Rosey Manfere kavuliwa taji na badala yake kapewa mshindi wa pili, Juliana Rugamisa.

Mwakilishi wa kamati ya mandaalizi ya mashindano hayo, Azama Mashango aliliambia Mwananchi kuwa hawajamvua taji mrembo huyo, bali hataenda kuwakilisha nchi katika mashindano ya dunia yanayotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu nchini Puerto Rico, badala yake atakwenda mshindi namba mbili, Juliana Rugamisa.

Azama anasema walifikia maamuzi hayo baada ya Rose kuvunja mkataba kutokana na kukiuka baadhi ya vipengele vilivyomo.


Kilichojificha nyuma ya pazia

Wakati hali ikiwa hivyo na kuwaacha Watanzania na maswali mengi kwamba ni kosa gani kubwa kalifanya Rosey hadi kuchukuliwa kwa hatua hiyo ambayo wanaona ni adhabu kubwa kwake, Mwananchi imedaka baadhi ya makosa yanayodaiwa kuwa ndio yamemtia hatiani.

Advertisement

Baadhi ya makossa hayo ni pamoja na kuingia mkataba na kampuni moja ya urembo bila kuishirikisha kamati, jambo ambalo katika mkataba walioingia naye ni kosa kisheria.

Lingine inaelezwa kuwa mrembo huyo ambaye alipata ushindi huo akiwa ametokea Wilaya ya Kinondoni amekuwa ni mtu wa kuchelewa katika matukio mbalimbali ambayo amekuwa akialikwa.


Basata, kamati wanavyoumana

Baada ya kutokea kwa tukio hilo, Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) liliitisha kikao cha kukutanisha pande zote mbili, yaani Miss Tanzania Rosey na kamati ya maandalizi, lakini wajumbe wa kamati hiyo hawakutokea kwa kile walichoeleza kutingwa na majukumu mengine.

Kikao hicho ilikuwa kifanyike saa nne asubuhi ofisi za Basata Kivukoni Julai 15 mwaka huu.

Licha ya kutotokea kwa wawakilishi wa kamati hiyo, kikao kilifanyika kwa kumsikiliza Miss aliyekuwa ameongozana na mwanasheria wake na mwisho wa kikao maamuzi yaliyoafikiwa ni kutengua maamuzi ya kamati hiyo na kuagiza jina la Rosey kupelekwa kwenye mashindano ya Miss World.

Hata hivyo, saa chache baada ya kutolewa kwa maamuzi hayo, kupitia ukurasa wao wa Miss Tanzania, waliandika “Mashindano ya Miss Tanzania yanaendeshwa kwa sheria, taratibu na kanuni. Tunawasihi warembo mnaotafuta nafasi adimu ya kuwa warembo wa Taifa mzingatie sheria na kanuni.

“Maelekezo ya kamati ambayo mengi ni ya kukuongoza wewe kuilinda heshima yako na taji, ukizingua maana yake utazinguana na wahusika na sheria itachukua mkondo wake.”

Andiko hilo liliendelea kueleza kuwa... “Utaelekezwa ukikaidi hatutasita kumpa mshindi wa pili kwa muujibu wa kanuni na sheria zetu.

“Kwa kifupi kama una makucha yafiche hadi urudi Miss World, vinginevyo hakutakuwa na wa kumlaumu. Ukimlaumu aliyechukua nafasi yako wakati alikupongeza wakati wewe unashinda utakuwa ni ubinafsi.

“Sheria imempa nafasi ni haki yake, ushauri wa bure kwa warembo wa Tanzania.”

Ukiachilia mbali andiko hilo, bado wanaendelea kupiga kampeni ya kumtangaza Juliana kama mwakilishi kwa kuweka picha zake na kuonyesha shughuli mbalimbali za kijamii ambazo anaendelea nazo. Gazeti hili lilipomtafuta Mwenyekiti wa kamati ya mashindano hayo kufafanua hili alisema: “Kila kitu kipo kama nilivyozungumza awali, mkataba wa Miss Tanzania unajieleza.

Advertisement