Kali 10 Albamu mpya ya Darassa

MWIMBAJI mkali wa muziki wa kizazi kipya nchini, Ramadhani Shariff ‘Darassa’ usiku wa kuamkia Desemba 24 alifanya uzinduzi wa albamu yake ya kwanza katika maisha yake ya muziki aliyoipa jina la Slave Becomes a King ikiwa na nyimbo 21.

Darassa anakuwa msanii wa nne Bongo kati ya wale wanaofanya vizuri kufanya hivyo mwaka huu. Lakini albamu hii ina maana gani hasa? Makala haya yanakuleta mambo 10 ambayo unapaswa kuyafahamu kuhusu albamu hiyo.

1. Kubwa kuliko

Slave Becomes a King ndio albamu pekee iliyotoka mwaka huu ndani ya Bongofleva ikiwa na idadi kubwa ya nyimbo na kupindua rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na albamu ya Harmonize, Afro East ilitoka Machi, mwaka huu.

Albamu ya Darassa ina nyimbo 21 ikiwa imepishana tatu na ile ya Harmonize, Afro East yenye nyimbo 18, lakini kwenye baadhi ya mitandao kama Tidal, Amazon, Deezer, Yandex na YouTube Music ikionekana kuwa nyimbo 17 baada ya wimbo wake, Your Body uliochukua vionjo vya wimbo wa Papa Wemba uitwao Show Me the Way kuondolewa. Nafasi ya tatu inakamatwa na albamu ya kundi la Navy Kenzo, Story Of The African Mob yenye nyimbo 12 ambayo ni idadi sawa na ya Barnaba iitwayo Refresh Mind. Mwisho ni albamu ya DJ rasmi Mwimbaji wa Diamond Platnumz, Romy Jons ‘RJ The DJ’ inayokwenda kwa jina la Changes yenye nyimbo 11.

2. Kiswahili aisee

Ujio wa albamu ya Darassa, Slave Becomes a King umekuja kukidondeshea tena kitu kizito kichwa lugha ya Kiswahili licha ya nyimbo zake kutumia lugha hiyo. Kivipi? Hii ni kutokana na jina la albamu hiyo ni la lugha ya Kingereza, na ikumbukwe albamu zote zilizotoka mwaka huu ndani ya Bongo Fleva majina yake yametumia lugha hiyo.

Ebu tazama, Afro East ya Harmonize, Story Of The African Mob ya Navy Kenzo, Refresh Mind ya Barnaba na Changes ya Romy Jons ‘RJ The DJ’. Majina yote hayo ni ya kuja na meli, ni tofauti na kipindi cha nyuma unakuta msanii mkubwa kama Juma Nature anatoa albamu anaipa jina la Ugali. Maisha yapo kasi sana.

Pia, nyimbo 12 zinazopatikana katika albamu ya Slave Becomes a King zina majina ya Kingereza, huku tisa ndizo zimeambulia majina Kiswahili, hata hivyo nyingine zikiwa na mchanganyiko. Mathalan wimbo namba sita ambao amemshirikisha Dogo Janja umepewa jina Size Yao.

3. Kampa, kampa tena

Mkali wa miondoko ya RnB Bongo, Ben Pol ndiye msanii pekee aliyeshiriki katika nyimbo mbili zinazopatikana katika albamu hiyo, huku wengine wakipata nafasi moja pekee. Ben Pol ameshikiri wimbo namba nne ‘Nimetumwa Pesa’ ambao pia yupo Billnass.Pia sauti yake imesikika katika wimbo wa 20 unaoitwa ‘Boss’.

Ikumbukwe Ben Pol ndiye aliyeimba kiitikio cha wimbo, Sikati Tamaa ambayo ndio ulimtoa Darassa kimuziki, pia alishiriki katika wimbo ‘Muziki’ wenye mafaniko makubwa kuliko wimbo wowote wa rapa huyo. Ndani ya miaka minne video ya wimbo ‘Muziki’ imetazamwa (views) zaidi ya mara milioni 17 kwenye mtandao wa YouTube na kuwa wa kwanza na wa pekee hadi sasa kwa msanii huyu kufikia mafanikio hayo.

4. CMG yahusika

Slave Becomes a King imetoka rasmi chini ya usimamizi wa lebo yake inayokwenda kwa jina la Classi Music Group (CMG) aliyoianzisha Juni 2016. Tofauti na zilivyo lebo nyingine katika Bongo Fleva, CMG haijawahi kumsaini msanii yeyote zaidi ya kusimamia kazi za msanii huyo na hadi sasa imefanikisha ujio wa albamu.

Ikumbukwe Darassa ni miongoni mwa marapa Bongo wenye lebo zao, wengine ni Fid Q inayosimamia Cheusi Dawa Entertainment, huku Joh Makini akiwa na Makini Records aliyoianzisha Oktoba, mwaka huu.

5. Ni Sho Madjozi pekee

Licha ya Darassa huko nyuma kutoa nyimbo nyingi zilizofanya vizuri na zenye maana kubwa katika maisha yake binafsi na kimuziki, lakini ni wimbo mmoja pekee uliowahi kutoka ambao umejumuishwa kwenye albamu hii. Wimbo huo ni I like It ambao amemshirikisha rapa wa kike kutoka Afrika Kusini, Sho Madjozi. Lakini kwa nini ni wimbo huu pekee? Kuna sababu kadhaa zinazochangia. Mosi; I like It ndio ulikuwa wimbo wa mwisho kwa Darassa kuutoa kwa mwaka huu kisha kufuatia kimya kirefu kwenye muziki, mitandao na vyombo vya habari hadi alipoibuka juzi na kuachia albamu hiyo. Pili; Utakumbuka toka Agosti 12, 2017 hadi Septemba 9,2018 Darassa alikuwa hajafanya muziki kabisa, aliporejea akaachia nyimbo kama Relax, Leo na Juju alizomshrikisha Jux, Shika na Tumepoteza akiwa na Maua Sama, Yumba akimshirikisha Harmonize, na huo I Like It aliyomshirikisha Sho Madjozi.

Hata hivyo, wimbo I like It ndio unaonekana kupata mafanikio makubwa zaidi kuliko hizo nyingine zote. Video ya wimbo huo imetazamwa (views) YouTube zaidi ya mara Milioni 7.2, ikiwa ni video yake ya pili kupata kutazamwa zaidi ukitanguliwa na video ya Muziki.

6. Ziiki Media

Hii ni kampuni ambayo imeshirikiana na Darassa katika kuhakikisha albamu hiyo inatoka ikiwa na kiwango cha juu kabisa cha ladha ya aina yake. Inaelezwa imeanza kufanya kazi na msanii huyo kwa zaidi ya miaka mitatu ingawa sasa ndio imeonekana. Ziiki Media ambayo makao yake makuu ni Afrika Kusini inafanya kazi na wasanii zaidi ya 50 kutoka Tanzania, Kenya na Nigeria.

7. Abbah Music

Licha ya Prodyuza kufanya kazi ya kutayarisha muziki, lakini albamu hii ya Darassa imewashirikisha Maprodyuza wawili, Abbah na Mr. T Touchez kama wasanii. Ni katika wimbo namba nane uitwa Blessings

Kubwa zaidi ni msanii anayechipukia aitwaye Jaiva kutoka Abbah Music ambaye ameshirikishwa katika wimbo namba 11, Lock Me Down yaani mtu na Bosi wake wameweka chungu kimoja na Darassa.

8. Makosa

Bila shaka ulikosekana umakini kabla ya cover ya albamu hiyo kutoka, ukiitazama vizuri utaona kuna makosa yamejitokeza hasa kwenye majina ya baadhi ya wasanii.

Mfano, jina la Marioo limeandikwa Mario, wameweka ‘o’ moja mwishoni badala ya mbili, jina la Barakah The Prince limeandikwa Barakah De Prince, katikati ni ‘The’ na si ‘De’, jina la Mr. T Touchez limeandikwa Ttoch, hata kama ni ufupisho, kuna tofauti kubwa sana ya neno ‘Touch’ na ‘Toch, ni vitu viwili tofauti kabisa.

Athari zake ni kwamba jina la msanii ndio chapa yake (brand) popote pale, sasa unapoliandika kimakosa inaleta ukakasi. Kwa lugha rahisi kama majina hayo yangekuwa ni Neno Siri (Passwords) la kufungua au kupata huduma fulani, basi Darassa angeikosa hadi pale atakapoandika kwa usahihi. Timu ya Darassa ina nafasi ya kurekebisha hilo kabla ya kuingiza albamu hiyo kwenye mitandao mikubwa ya kuuza na kusikiliza muziki duniani.

9. Media Friendly

Kwa sasa muziki wa Bongo Fleva umegawanyika sana, si ajabu kukuta msanii mmoja kazi zake zinachezwa sana na chombo kimoja cha habari (redio/TV), huku kingine hakifanyi hivyo hata kutaja jina lake ni mwiko, nao wanakuwa na msanii wao. Hili limepelekea baadhi ya wasanii kushindwa kufanya kazi na wasanii wengine kwa kuhofia kazi zao kutopata nafasi sehemu ambazo wale wanaotaka kufanya nao kolabo kazi zao hazichezwi.

Bila shaka Darassa kazingatia hilo kwa maslai mapana ya muziki wake, wasanii ambao wanatofauti na baadhi ya vyombo vya habari hadi kupelekea kazi zao kutopata nafasi za kuchezwa, hawajapata kushirikishwa kwenye albamu hii, Slave Becomes a King.

10. Uchokozi kwa Alikiba

Darassa anajitambulisha kama Mfalme ambaye kipindi cha nyuma alikuwa Mtumwa, hiyo ni kwa mujibu wa maana ya jina la albamu hiyo, Slave Becomes a King. Kama naye amekuwa Mfalme sasa itakuwaje maana kuna baadhi ya wasanii Bongo wamekuwa wakijiita Wafalme. Miongoni mwao ni Alikiba (King Kiba) hadi kuamua kuipa lebo yake jina la Kings Music kutilia msisitizo hilo.

Kiutaratibu hakuna himaya ambayo inatawaliwa na afalme wawili, iwapo atajitokeza wa pili wakati ya kwanza bado yupo mamlakani, basi huo utakuwa ni uchokozi. Je, tuseme Darassa kamchokoza Alikiba?.

Uzuri ni kuwa Alikiba ameshiki-rikishwa na Darassa kwenye wimbo wa Proud of You.


Imeandikwa na Peter Akaro