Kajala na Paula wakamatwa na kuhojiwa

Tuesday April 20 2021
kajala pic
By Nasra Abdallah

Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam limethibitisha kuwakamata na kuwahoji msanii Kajala Masanja na mtoto wake Paula.

Tetesi za kukamatwa kwa wawili hao zilisambaa jana katika mitandao ya kijamii.

paula pic

Akizungumza na MwanaSpoti leo Jumanne Aprili 20,2021, Kamanda wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema wawili hao walikamatwa na usiku wa kumkia jana na kuhojiwa na ilipofika saa 1:30 usiku waliachiwa baada ya kupata dhamana.

Mambosasa alitaja makosa wanayotuhumiwa nayo kuwa ni makosa ya kimtandao ya kusambaza picha za utupu mitandaoni huku mlalamikaji akiwa ni msanii Rajab Abdul maarufu kwa jina la Harmonize.

“Ni kweli tumemkamata Kajala na Paula tukawahoji baada ya mlalamikaji Harmonize kuleta malalamiko kituoni lakini tayari tumeshawaachia kwa dhamana,” amesema Kamanda huyo.

Advertisement

Hata hivyo amesema wataendelea kuripoti Polisi mpaka hapo jalada la upelelezi wa kesi yao litakapokamilika na kuweza kufikishwa mahakamani kwa kuwa kesi za aina hiyo huchukua muda mrefu kuzifanyia uchunguzi.

Katika hatua nyingine Kamanda Mambossa amesema wasanii Rayvany, baba Levo na Juma Lokole, nao ni moja ya watuhumiwa waliolalimikiwa na Harmonize kwa kosa hilo la kusambaza picha za utupu ambao nao tayari wamehojiwa na Jeshi hilo na upelelezi bado unaendelea.

Wasanii hao watatu kwa pamoja walifika kituo cha Polisi Kati Aprili 15, 2021 kwa ajili ya mahojiano hayo.

Siku tano zilizopita Harmonize kupitia Instagram yake aliapa kuwaburuza mahakamani na kudai fidia kwa wale wote wanaohusika kumchafua jina lake kwa kusambaza picha za utupu zinazodaiwa kuwa ni zake.

Advertisement
​