JAY STYLES: Mbunifu wa vazi la Harmonize lililozua gumzo kila kona

Monday May 03 2021
vazi pic
By Nasra Abdallah

KWA jina la kibiashara anajiita Jay Styles. Huyu ndiye mbunifu wa vazi la vijiko, umma na visu alilombunia msanii maarufu wa muziki wa Bongo Fleva, Harmonize.

Vazi hilo ni mojawapo ya mavazi ambayo Harmonize amevaa kwenye wimbo wake mpya wa ‘Attitude’ aliouimba kwa kumshirikisha Awilo Longomba kutoka DR Congo pamoja na H.Baba na limeibua gumzo kwa wadau wa muziki nchini.

vazi harmo

Ni kutokana na mvuto wake kuna ‘challenge’ zinaendelea za watu kurekodi video zao na kuonyesha kuvaa vazi kama hilo huku wengine wakijiongeza kwa kuweka birika, sufuria, chujio yaani kwa kifupi watu wamehamishia jikoni mwilini mwao.

Mmoja wa waliofanya hivyo ni mchekeshaji maarufu nchini Kenya, Mammito Eunice, jambo lililochangia wimbo huo kuzidi kupata watazamaji wengi huko YouTube.

Kama hujui wimbo huo mpaka juzi ukiwa ndio una siku ya sita, ulikuwa umeshatazamwa zaidi ya mara milioni 6 na kukamata nafasi ya kwanza kati ya nyimbo zinazotrend takribani siku tatu mfululizo.

Advertisement

Hata hivyo, Mwanaspoti lilimtafuta mbunifu wa vazi hilo, Jay Styles na kufanya naye mahojiano na alielezea namna alivyotengeneza vazi hili na jinsi Harmonize alivyolipokea.

Jay ambaye jina lake halisi ni Exuperius Evodius, anasema ilikuwa wiki chache zilizopita baada ya msanii huyo kumwita ofisini kwake na kumtaka ambunie nguo atakayovaa kwenye wimbo huo.

“Ujumbe huu wa Harmonize kwa kweli awali ulikuwa mgumu kwangu ukizingatia nilikuwa nimetoka kumbunia nguo nyingine alizopigia picha kwenye video ya wimbo wake mwingine ambao bado haujatoka, shughuli aliyoifanyia visiwani Zanzibar.

“Mbaya ni kazi hiyo nilikuwa nimeharibu kwa kumchanganyia na nguo za dukani na aliligundua hilo na kunichamba kwelikweli hivyo nilikuwa nina wakati mgumu kurudisha imani.”

Anasema ilimchukua takribani siku mbili kumpa majibu kama ataweza kufanya kazi hiyo au la lakini mwishowe iliwezekana.


Alivyokuna kichwa kulipata

Anasema katika kulipata vazi hilo, wazo lilikuja baada ya siku moja kupata chakula kwa mamalishe.

Akiwa huko anasema alidondosha kijiko kwa bahati mbaya, na wakati mhudumu anataka kwenda kumletea kijiko kingine alimwambia aache atatumia hicho hicho.

Mwenzie ambaye hushirikiana kwa karibu katika kuzifanya kazi hizo za ubunifu mavazi, aliyekuwa akipata naye chakula hicho akamuuliza unapenda sana vijiko wewe.

“Hapo ananiuliza, hivyo bado tunakuna kichwa vazi la Harmonize tunafanyaje, hapo ndipo nikapata wazo na kumuuliza hivi kwa nini tusimtengenezee msanii huyo vazi la kijiko.

“Kama haitoshi vyombo hivyo vilinikumbusha maisha niliyopitia na mama yangu alinilea kupitia kazi ya mama lishe, nilichezea sana vijiko, hivyo nilivyounganisha yote hayo, nikaona nina kila sababu ya kulitengeneza vazi hilo kwa kutumia vifaa hivyo vya jikoni,” anasema Jay.


Mtihani mzito kutengeneza

Akizungumzia changamoto alizozipata katika kulitengeneza vazi hilo, Jay anasema ni pamoja na upatikanaji wa malighafi hususani kitambaa cha koti na kulazimika kukiagiza nje ya nchi.

Hata hivyo, kwa upande wa vijiko anasema ilikuwa rahisi kwani kuna rafiki yake anafanya biashara ya kuuza vyombo hivyo alichofanya ni kunyanyua simu na kumuagiza ampelekea seti nne za kisu, seti nne za uma na seti nne za vijiko.

“Wakati hali ya upatikanaji wa vifaa ikiwa hivyo shughuli nyingine ilikuja kwenye namna tutakavyoweza kutoboa vijiko vile ili tuweze kuvining’iniza kwenye koti.

“Mara ya kwanza tulienda kwa mtoboa vioo, tukachemka kwani kwenye matundu kulikuwa kunaonekana kama uchafu, mara ya pili tukaenda kwa wanaochomelea vyuma napo hali ikawa hivyohivyo tukachemka na tukaja kufanikiwa kwa kutumia misumari flani hivi ya iana mbili tuliyoinunua kwenye duka la vifaa vya ujenzi.

“Hatimaye vazi likakamilika na ilinichukua siku nne kufanya kazi hiyo hadi kuisha kwake ilitugharimu Sh 3 milioni,” anasema Jay.


Alivyolipokea Harmonize

Anasema siku ambayo amempelekea vazi hilo ofisini kwake huku akiwa hajiamini kama atalikubali au la, alipolitoa kwenye mfuko wake na vyombo vile kuanza kupiga kelele, Harmonize alicheka sana.

Hata hivyo, anasema msanii huyo baada ya kulijaribisha alilipenda japokuwa ilibidi akalifanyie marekebisho ya kuliondoa mikono na kuwa la kata mikono.

Anasema katika maisha yake hatamsahau Harmonize kwani mbali ya kufanya naye kazi mbalimbali lakini hii ya vazi la vijiko amemsaidia kumvusha zaidi ikiwemo kupokea simu kutoka kwa wadau mbalimbali za kumpongeza na wengine kutaka awashonee.

Pia anasema kitendo cha msanii huyo ‘kumtag’ kuwa ndiye aliyetengeneza vazi lile, kumemwongezea wafuasi huko mitandaoni ambao anaamini kupitia wao watazidi kumtangaza na kazi zake huku akiwaahidi kutowaangusha kwani malengo yake pia ni kuitangaza Tanzania kimataifa katika tasnia hiyo ya ubunifu wa mavazi.

Advertisement