Haya ndiyo maisha ya Paula

Muktasari:

BAADA ya kufanya vibaya katika mitihani yake ya kidato cha nne, mtoto Paula Paul aliamua kurudia masomo yake katika Shule ya Sekondari St. Anne Maria.

BAADA ya kufanya vibaya katika mitihani yake ya kidato cha nne, mtoto Paula Paul aliamua kurudia masomo yake katika Shule ya Sekondari St. Anne Maria.

Paula ni mtoto wa msanii wa filamu nchini Kajala Masanja aliyezaa na mtayarishaji maarufu wa muziki, Paul Matthysse ‘P Funk Majani’.

Katika mitihani yake ya kuhitimu kidato cha nne mwaka 2018 ambayo matokeo yake yalitoka Februari mwaka 2019, Paula alifeli, jambo ambalo lilizua gumzo ukizingatia rafiki yake wa karibu ambaye ni mtoto wa msanii Monalisa, alipata daraja la kwanza.

Baadhi ya watu walionyesha kumlaumu mama yake na kusema ni matokeo ya malezi aliyokuwa akimlea ya kutwa kumuonyesha kwenye mitandao ya kijamii huku picha zingine zikiwa kama sio mtoto ambaye ni mwanafunzi.

Hata hivyo maneno ya watu hayakumfanya Paula kukata tamaa kwani alikwenda kurudia masomo yake mwaka jana, 2020.

Mwanaspoti ilizungumza na Mkuu wa shule hiyo, Gradius Ndyetabula alieleza walivyompokea Paula ambaye alikaa hadi Novemba na kufanya mitihani ya kidato cha nne.

“Alipofika shuleni hapa alihitaji kurudia masomo matatu ambayo ni Historia, Kiswahili na Uraia na matokeo yalipotoka alipata yote alama C, huku malengo yake yakiwa ni kwenda kusoma mchepuo wa HKL,” alisema mwalimu.


Walivyoishi naye

Mwalimu huyo anasema walipokuwa na Paula katika kipindi chote alitii sheria na taratibu za shule.

“Sisi maisha ya ustaa na rekodi zake zingine huwa zinaishia nje geti, akifika ndani ya shule anakuwa sawa na watoto wengine,”.

Mwalimu huyo anatoa wito kwa wazazi na jamii kutowakatia tamaa watoto pale wanapofanya vibaya kwenye mitihani yao kwa kuwa nafasi ya wao kufanya vizuri ipo kikubwa ni nia ya mtoto mwenyewe kutaka kuendelea kusoma.


Je anaweza kuendelea kidato cha tano?

Swali linakuwa ni je anaweza kuendelea kidato cha tano ukizingatia sasa hivi tayari wanafunzi wameanza kupangiwa shule na serikali.

Jibu ni ndio, lakini yeye hataweza kupangiwa shule za serikali badala yake ataenda shule binafsi.

Ofisa Uhusiano wa Baraza la Mitihani Tanzani (NECTA), John Nchimbi, anasema tofauti na wasanii waliotoka shule moja kwa moja mtu kama Paula anaweza kuamua kwenda kusomea masomo mengine ambayo alikuwa na kiu ya kuyasoma akiwa huko kidato cha tano. Lakini ikifika wakati wa kufanya mitihani atafanya kama mtahiniwa wa kujitegemea kwa kufanya masomo hayo ili cheti chake cha kidato cha nne na sita viendane licha ya kuwa mitihani yote ya aliyetoka shule moja kwa moja na hao wanaofanya kama wanafunzi wa kujitegemea husahihishwa pamoja.


Alivyoandamwa na mabalaa

Licha ya kuwa na umri mdogo Paula mwenye miaka 18, amejikuta akiteka vichwa vya habari ikiwemo lile sakata lake la kuonekana kwa video akiwa katika mapozi ya kimahaba na msanii Rayvvany ambaye anaelezwa kuwa na mahusiano naye.

Hii ni baada ya Rayvanny kuweka video hiyo katika ukurasa wake wa Instagram ikiwa ni siku chache tangu atoke kuachia albamu yake ya ‘Sound of Afrika’ Sakata lilifika mbali hadi kufikishana polisi ambapo hata hivyo baadaye waliyamaliza kifamilia na maisha kuendelea.