Godliver aenda kwa mganga

Monday November 29 2021
God PIC

Muigizaji GODLIVER Gordian ‘Anna’.

By Charity James

GODLIVER Gordian ‘Anna’ anafanya vizuri kwenye tamthilia ya Jua Kali iliyoandaliwa na Lamata na kubeba visa vya kusisimua huku yeye akicheza nafasi ya mateso kwenye uhusiano wa kimapenzi.

Kwenye tamthilia hiyo, mwanadada huyo ameonekana kuumizwa na mapenzi kwa kuanzisha mahusiano na baadaye kuachwa huku akishindwa kujipa muda na kuamua kuingia kwenye mahusiano mengine.

Amezika mchumba mmoja ambaye walifikia hatua ya ndoa, alifariki kwa ajali akielekea kanisani kufunga ndoa wakati wanaume wengine wawili waliishia kumvisha pete za uchumba na baadaye kumtelekeza.

Ilipofikia sasa Anna anaonekana kuingia kwenye mahaba na rafiki yake waliyewahi kusoma wote ambaye amemrudisha kwenye furaha baada ya kumpoteza mwanaume ambaye alitaka kumuoa.

Katika mahojiano na gazeti hili, msanii huyo amefunguka mambo mbalimbali huku akitaja kuwa anachokiigiza aliwahi kukipitia japo sio kwa namna anayoigiza kwa kuingia kwenye mahusiano bila kujipa muda.

“Nilianguka baada ya kuona nimekosea nikamshirikisha mzazi wangu hilo alinisisitiza nimepotea sijafanya kitu sahihi lakini sio mimi ni sauti ilikuwa inanitokea na kuniamuru kuwa ni mwanaume sahihi kumbe sio,” anasema Anna mwenye taaluma ya uandishi aliyeamua kuchagua sanaa ya kuigiza;

Advertisement

“Baada ya kufanya tendo kinyume na maagano ambayo yanasema ni lazima muungie kwenye ndoa ndio mfanye hilo tendo lakini nililifanya kwanza na kushtuka baada ya tukio na baada ya hilo ndipo nilipoanza kuonyeshwa matendo mabaya ya kijana ambaye nilionyeshwa na Mungu kuwa ni sahihi kumbe sio,” anasema

Anasema aliamini Mungu ndiye alimuonyesha na kuamini ndiye mume sahihi kumbe ni akili yake ilitumika kwa kuamini anazungumza naye kwa njia ya sauti.


KWENDA KWA WAGANGA

Mwanadada huyo amekiri wasanii wanakwenda kwa waganga kusafisha nyota huku akithibitisha kuwa na yeye amefika huko.

“Nimeingia kwenye tasnia hii sio kutafuta umaarufu ni kwa sababu ya mapenzi na kazi hiyo kama ningetaka umaarufu ningetumia hata mwili wangu,” anasema

Anasema alifuatwa na msanii mwenzake na kumwambia akienda kwa mganga kuna kitu anaweza kupata zaidi.

“Ukienda kwa mganga utafanikiwa iwapo roho na nafsi yako inakuaminisha hivyo, kuwa kuna mafanikio ila ni imani tu kwani shetani anatoa mmilikiwa, hii dunia ni shetani utakapo jidhihilisha kwake na kumtumikia, siku zote huwa naye anachukua, Mungu anatoa tu lakini huyo mwingine anakupa kidogo na yeye anachukua kidogo.

“Nilifanya lakini sikuwa radhi kujikabidhisha kwenye kile nilichokuwa nakifanya kuna wanaoenda huko wanafanikiwa lakini kwa upande wangu nilichokuwa nataka sikufanikiwa,” anasema.


MIAKA 13 TUZO MOJA

“Nimefanya tamthilia mbili nikianza na Siri ya Mtungi na sasa Jua Kali ambayo ndio imenipa umaarufu mkubwa wakati nilianza kuigiza miaka 10 iliyomita lakini miaka mitatu ya hivi karibuni ndio inanipa umaarufu.

“Pamoja na tamthiliya hizo tayari nimepata tuzo ambayo imetokana na filamu nilifanya kazi hiyo iliyokwenda kwa jina la Aisha haikunikuza sana lakini ilikuwa bora sana kwangu na kunipa tuzo mwaka 2019,” anasema.

Anna amelithibitishia gazeti hili kuwa mwaka huu pia ameingia kwenye kinyang’anyiro cha msanii bora wa kike hii imetokana na uigizaji aliouonyesha kwenye Jua Kali.

Advertisement