Francois Botha kusimamia pambano la Class Dar

Muktasari:

Class ana rekodi ya kushinda mapambano 25, amepigwa mara sita  wakati Mwale hajawaji kupigwa tangu 2017 alipoingia kwenye ngumi za kulipwa, amecheza mapambano manane.

BONDIA nguli wa  zamani wa uzito wa juu Francois 'The White Buffalo' Botha atakuwa miongoni mwa wasimamizi wa pambano  la Ubingwa wa Mabara wa WBF kati ya Mtanzania, Ibrahim Class na Dennis Mwale wa Malawi la uzani wa light.

Botha bondia aliyewahi kuzichapa na mabondia maarufu wa uzani wa juu duniani akiwamo Mike Tyson, Lennox Lewis na Evender Holyfield atasimamia pambano hilo la Januari 29 mwaka huu.

Nguli huyo wa ndondi atawasili nchini sanjari na Rais wa WBF,  Goldberg Howard ambapo wataanza kwa kuendesha mafunzo ya waamuzi Januari 26 na siku tatu baadae watasimamia pambano la Class na Mwale kwenye ukumbi wa Next Door Arena, Masaki jijini Dar es Salaam.

Mratibu wa pambano hilo, Kelvin Twissa wa kampuni ya Jackson Group Sports, amebainisha ujio wa Botha leo Januari 6, 2021 wakati akiwatambulisha mabondia watakaozichapa siku hiyo.

Amesema mbali na pambano la Class, bondia wa uzani juu, Shaban Jongojongo atawania ubingwa wa kimataifa wa WBF wa uzani wa cruiser  dhidi ya  Mmarekani, Shawn Miller.

Class bondia namba mbili nchini, alisema yuko tayari kwa pambano na yuko kwenye mazoezi makali chini ya kocha Habibu Kinyogoli.

"Naamini nitashinda, nafanya mazoezi makali nikipewa sapoti ya sparing 'kupigana ana kwa ana' Salum Mtango kuelekea kwenye pambano, kwa mazoezi ninayotafanya sina shaka ubingwa utabaki nyumbani," amejinasibu Class.

Mbali na Class, mabondia wengine 16 watazichapa kwenye pambano hilo lililopewa  jina la “The Jackson Group Fight Night” kuwasindikiza.

Twissa amesema siku hiyo mabondia hao ni kutoka nchi 10 tofauti ambao wanaendelea na mazoezi.

"Kabla ya pambano, Januari 26 kutakuwa na semina ya waamuzi na majaji ambayo itashirikisha washiriki kutoka nchi za  Botswana, Kenya, Afrika Kusini na Tanzania ili kujifunza sheria mbalimbali.