Fallly Ipupa amtaja Barnaba, mwenyewe afunguka

Fallly Ipupa amtaja Barnaba, mwenyewe afunguka

Muktasari:

  • Mwanamuziki kutoka Jamhuri ya Kongo, Fally Ipupa amesema anafuatilia muziki wa Tanzania kwa karibu na moja ya wasanii anaowakubali ni Barnaba Classic.

Dar es Salaam. Mwanamuziki kutoka Jamhuri ya Kongo, Fally Ipupa amesema anafuatilia muziki wa Tanzania kwa karibu na moja ya wasanii anaowakubali ni Barnaba Classic.

Mwanamuziki huyo ameyasema hayo leo  Alhamisi Oktoba 7,2021 alipotua nchini Tanzania kwa ajili ya kufanya maonyesho yake katika mikoa miwili ya Dar es Salaam na Mwanza.

Baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere pamoja na mambo mengine pia alipata wasaa wa kuzungumza na waandishi wa habari.

Moja ya maswali aliyoulizwa ni kwa namna gani anafuatilia muziki wa Tanzania na ni wasanii gani anawapenda ambapo kati yao alimtaja Barnaba.

"Ni kweli nafuatilia sana muziki wa Tanzania na wasanii wote wanaofanya vizuri mimi nawapenda akiwemo Diamond,Alikiba na huyu mwingine anayeimba na kupiga gitaa,nani huyuu...ndio Barnaba," amesema Fally Pupa.

Kutokana na kutajwa huko,Mwananchi ilimtafuta Barnaba kujua namna alivyochukulia kutajwa na msanii huyo mwenye tuzo nyingi za muziki za kimataifa ikiwemo MTV Africa na BET.

Katika maelezo yake Barnaba amesema anasikia faraja kwa kuwa wasanii wazuri wapo wengi lakini kutajwa yeye ni heshima kubwa.

"Fally Pupa ni kaka yangu,najisikia faraja kunitaja kuwa moja ya wasanii anaowakubali nami pia namkubali sana kwani huyu ni alama ya muziki wa Afrika, tuna kila sababu ya kujivunia kuwa naye" amesema Barnaba.

Hata hivyo amesema amefahamiana na msanii huyo siku nyingi tangu alipokuja Tanzania miaka kumi iliyopita licha ya kuwa hawajawahi kuimba naye wimbo wa pamoja.

Fally Ipupa ni kati ya wasanii wa Kongo waliofanya kolabo na msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz na kupokelewa vizuri kwenye soko ambaye amemshirikisha katika wimbo wake' Inama'.

Wimbo huo mpaka sasa umeshatazamwa mara milioni 97 kwenye mtandao wa YouTube ukiwa unashika namba mbili kwa nyimbo za Diamond alizofanya na wasanii wa Kongo.

Wimbo ambao unaongoza kwa kutazamwa ni wa 'Yope' alioimba na Innos B ambao una milioni 167.

Wakati wimbo wa 'Waah' alioimba na nguli wa muziki nchini Kongo,Koffi Olomide ukiwa umetazamwa mara milioni 87.